RAIS Jakaya Kikwete jana alikwenda nyumbani kwa familia ya marehemu Regia Mtema
(32), Mbunge wa Viti Maalumu Chadema Tabata Chang’ombe jijini Dar es Salaam
kuomboleza msiba wa Mbunge huyo.
Regia alifariki Jumamosi asubuhi katika
eneo la Ruvu mkoani Pwani kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha akiwa na watu
wengine saba akiwemo mama yake Bernadeta Mtema (45). Familia hiyo ilikuwa
ikienda shambani Vigwaza.
Pamoja na Rais Kikwete pia, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda alifika nyumbani hapo kutoa pole kwa familia kwa msiba huo
uliotokea kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu, mkoani Pwani.
Rais
aliwasili nyumbani hapo kabla ya saa saba na baada ya kutoa pole kwa familia
akiwemo
baba wa marehemu Estelatus Mtema, aliwapa pole baadhi ya viongozi wa
Chadema waliokuwepo msibani hapo akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Mara
baada ya Rais Kikwete kuondoka, alifika Pinda nyumbani hapo ambapo aliwafariji
familia hiyo kwa msiba na baada ya kukaa kwa muda, naye aliondoka.
Akizungumzia msiba huo Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema, “Nimepokea
kwa huzuni msiba huu si kwa kuwa ni Mbunge bali kijana jasiri na mkakamavu,
nimemfahamu Regia kabla hajawa Mbunge, wakati huo nikiwa Mwenyekiti wa Chama cha
Wanawake Wabunge, nilikuwa katika mikutano nahamasisha ile hamsini kwa hamsini
bungeni.”
“Regia ni miongoni mwa vijana wa kike waliokuwa wabunge
wakakamavu, nilimtia moyo na kumwambia natumaini kumuona bungeni na kweli
alifanikiwa kuwa Mbunge, alikuwa makini katika kila alichoongea na alijituma,
alijichanganya hata na Wabunge wa CCM, huu ni msiba wa Taifa,” alisema Makinda
kwa huzuni.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema
mbali na kuonesha kukubalika na kupata kura kwa asilimia 45 katika Jimbo
alikowania, ndiye aliyeibua wazo la viongozi wa Chadema kukutana na Rais Kikwete
kuzungumza naye kuhusu Muswada wa Mabadiliko ya Katiba.
“Nitaweka kwenye
mtandao hili, najua watu wengi hawajui lakini ndiye aliyeibua wazo kwenye
mkutano wa chama kuwa viongozi wakutane na Rais kuhusu Muswada wa Katiba,
nasikitika kwa kuwa kuelekea kwenye mchakato wenyewe, tunamkosa mtu muhimu kama
huyu,” alisema Zitto.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
msiba huo si wa familia na chama pekee bali ni wa Taifa hasa wapiga kura wa
Jimbo la Kilombero alikowania Ubunge na kupata kura 38,550 sawa na zaidi ya
asilimia 45 ya kura zote.
“Regia alikuwa mcheshi na jasiri, haogopi
kusema ukweli hata kama utakuumiza, tulimuhitaji sana hasa wakati huu wa
mabadiliko ya Katiba ya kitaifa, hatuwezi kumuhoji Mungu lakini ni masikitiko
makubwa,” alisema.
No comments:
Post a Comment