Nilikwenda kuzungumza naye Alhamisi mchana nikatambua changamoto niliyoipata
muda mfupi kabla ya kuondoka ofisini Mtaa wa Samora, Dar es Salaam, na endapo
nisingekuwa na msimamo katika kile ninachokiamini huenda nisingekwenda huko
hivyo asingekuwa nyota wetu leo. Nilimtafuta kwa sababu naamini wanawake wengi
wanasikiliza kipindi anachokiongoza, Leo Tena, kinachorushwa Clouds FM Jumatatu
hadi Ijumaa saa tatu hadi saa saba mchana, na nilizungumza naye kwa saa mbili
nikitambua kuwa baadhi ya watu wana mtazamo hasi kuhusu yeye kwa fikra kwamba
Dina Marius, ni mbea, na shangingi.
Wakati nakwenda katika ofisi za
kampuni ya Clouds Entertainment, ghorofa ya saba katika jengo la Kitega Uchumi,
Dar es Salaam nilizingatia zaidi uwezo wake kutangaza kuliko maisha yake
binafsi, na nina imani kwamba aliyosimulia msichana huyo mwenye umri wa miaka 25
yanaweza kuwa darasa kwa wengine. Kwa wanaosikiliza kipindi hicho bila shaka
mara nyingi wamekuwa wakimsikia akisema ‘ Mimi naitwa Dina Marius wa ukweli
zaidi’, wakati mwingine hupenda kusema ‘ Ni leo tena ya Clouds FM, naitwa Dina
Marius’ au kibwagizo kisemacho ‘ Dina Marius leo tena’.
Sauti yake
ilianza kusikika katika kipindi hicho Februari 26, 2006, akibeba mikoba ya Amina
Chifupa, aliyekuwa na majukumu mengine katika Bunge la Jamhuri ya Muungano akiwa
Mbunge wa Viti Maalumu. Ni kipindi chenye vionjo vya mambo ya kijamii
yanayotokea katika maisha ya kila siku vikiwamo vya Nyumbani Kwetu Leo,
Chachandu la Leo, Kiburudisho Chako Leo, Heka Heka za Leo, ‘Kitchen Party’ na
‘Movie’ Leo, wengi wa wanaokisikiliza ni wanawake.
Anasema kufanya
kipindi kinachowalenga hasa wanawake ni ‘mtihani’ kwa kuwa amekuwa akitumiwa
ujumbe mfupi wa matusi, na wengine wanampigia simu kumtukana kwa sababu
wanazozifahamu wao. “Unajua kufanya kipindi ukawalenga wanawake ni kazi,
wanawake kama wanawake kuna ambao watakufurahia, kuna wengine mmh,” anasema Dina
na kueleza kwamba utangazaji ndiyo maisha yake, hivyo anailinda hadhi yake.
“’Nimefocus’ (nimelenga) kwenye kazi yangu halafu ‘at the end of the
day’ (mwisho wa siku) ukifanya kazi kwenye media (chombo cha habari) unakuwa
kioo cha jamii,” anasema na kubainisha kwamba, “inabidi ulinde ‘image’
(muonekano) yako kwa msikilizaji. Ukishakuwa mtangazaji huna tofauti na msanii,
uwe wa radio au wa TV, huna tofauti na msanii anayeimba muziki. “Saa nyingine
kuwa mtangazaji pia ni kujinyima uhuru, inabidi ujinyime ili kulinda maslahi
yako,” anasema.
“Kwa hiyo kwa sasa hivi nafanya ‘kui-brand image’
yangu,” anasema Dina na kuongeza kwamba kuna watangazaji ambao si kioo cha
jamii. “Mimi nikiwa hewani namfikiria anayenisikiliza, nikitoka pale nakuwa na
maisha yangu ya kawaida,” anasema na kujigamba kwamba wanawake wengi
wanasilikiza ‘Leo Tena’ kwa kuwa wanajitahidi kubuni vitu vinavyowavutia ikiwa
ni pamoja na kuweka wimbo wa taarabu na wao kuweka vionjo studio.
“Tukitoka pale maisha yanakuwa ya kawaida, maisha yetu ya kawaida
yasiyokuwa na mipasho… mimi naishi kivyangu vyangu, mtaani sina mashoga, sina
mashosti…mimi maisha yangu ya kawaida, sina magroup (makundi),” anasema na
anaamini kwamba ubunifu wa Chifupa ndiyo umefanya nyimbo za taarabu zipendwe
katika vituo vya radio na kwamba hadi leo radio nyingi zinaiga ‘style’ ya
mtangazaji huyo. “Unavyoizungumzia Chachandu (moja ya vipengele kwenye kipindi
cha Leo Tena), unazungumzia wimbo mmoja lakini ‘impact’ yake ni kubwa,” anasema
na kueleza kuwa, nyimbo nyingi za mahadhi hayo huchukua dakika 16 hadi 20 lakini
wao wamebuni namna ya kufanya usichoshe.
Ingawa alikuwa hafuatilii
utangazaji wa Chifupa wanaosema kuwa Dina ni mrithi wake Clouds FM hawakosei kwa
kuwa ndiye aliyepewa jukumu la kuongoza kipindi hicho alichokuwa akikiongoza
msichana mwenzake ambaye sasa ni marehemu, lakini hafahamu ni kwa nini
anafananishwa na mwanasiasa huyo. “I used to like Phina (Phina Mango, ambaye
aliwahi kuwa mtangazaji katika kituo hicho cha redio)...sauti yake,” anasema
msichana huyo asiyevutiwa na vipindi vya televisheni za Tanzania, na anakunwa
zaidi na vipindi vya mahojiano vya Oprah Winfrey.
Anasema hafahamu
amefanana nini na Chifupa, labda sauti, na wengine wanasema sura, ila
anachofahamu yeye katika utangazaji, mtangulizi wake alikuwa juu hivyo katika
hilo si sahihi kuwalinganisha kwa kuwa hawalingani. “Mtu mwingine anaweza
akaangalia picha akaona kama Amina, ni akili ya watu,” anasema mtangazaji huyo
aliyewahi kuwa na ndoto za kuwa daktari.
Msichana huyo anayeishi Kawe,
Dar es Salaam anasema, kuendesha kipindi cha Leo Tena, ilikuwa ni changamoto
kubwa kwake lakini imemsaidia kuongeza upeo wa kuelewa mambo mbalimbali ndani na
nje ya Tanzania. “Amina ‘was big’, mimi nilivyoanza kipindi unajua ‘it was so
hard’ (ilikuwa kazi ngumu),” anasema na kubainisha kuwa, mlengwa wa kipindi
hicho wakati kikiendeshwa na Chifupa ni yuleyule wa sasa ila baadhi ya
yanayozungumzwa humo yamebadilika.
Anasema hatarajii kufanya kazi ya
kutangaza kwa muda mrefu, ila anaweza kubadili aina ya utangazaji, na hata
akiondoka yeye Clouds FM jina la kipindi anachokiongoza halitabadilika.
“Entertainment Industry’ inafika kipindi unakuwa ‘out’” anasema msichana huyo
mwenye kipaji cha kuchora. Alishiriki mashindano ya uchoraji wakati akisoma
katika Shule ya Sekondari Shauritanga mkoani Kilimanjaro.
“Nachora kadi
kwa ‘manila paper’, naipaka rangi na ninaitengeneza namna ambayo mtu anaweza
kuandika , nilikuwa mpaka nauza,” anasema msichana huyo aliyekuwa akicheza ngoma
za utamaduni wakati akisoma Shule ya Msingi Ushindi iliyopo Mikocheni, Dar es
Salaam na Lyalamo ya Iringa. “Kwa sababu radio pia ina mipaka ya umri, ina
mlengwa wake…lakini ‘plan’ yangu kubwa ni kuwa na vipindi kama vile vya kina
Tyra, au Oprah,” amesema mtangazaji huyo anayeshirikiana na Gea Habib, Zamaradi
Mketema, na Antonio Nugas kuendesha kipindi cha Leo Tena.
“Kwa hiyo
naona ‘talk show’ ni nzuri lakini inategemea huko mbele upande wa Tanzania
inakuwaje,” anasema msichana huyo anayeamini kwamba nyota ya mtu haiji tu,
lazima uzungumze na watu mbalimbali, usome au kutazama vitu mbalimbali kuongeza
ufahamu wako na kwamba, ingawa kipindi anachokiongoza kinakwisha saa saba,
huenda nyumbani kati ya saa 11 hadi saa moja usiku.
“Kama sasa hivi
nikitoka lazima nihakikishe kesho nikija kusikosekane kitu… kwa hiyo hata
‘system’ yangu ya maisha imebadilika,” anasema na kubainisha kwamba changamoto
kubwa kwake ni kuhakikisha kuwa anachokisema radioni kiwe na matokeo hasi au
chanya kwa anayesikiliza. Anaamini anafanya kile alichozaliwa kukifanya na ndiyo
maana alikuwa na ndoto nyingi lakini sasa hazipo.
“Yaani iwe na ‘impact’
kwake (msikilizaji), kama alikuwa hajui ajue, kama cha kufurahisha acheke, hiyo
ndiyo changamoto niliyonayo, kila nikimaliza kipindi nakaa na timu yangu,”
anasema na kuongeza kuwa changamoto nyingine ni kuhakikisha kuwa watu
wanasikiliza na amedai kuwa uwezo wa mwanadamu kusikiliza kitu hicho hicho ni
dakika nne hivyo lazima umshawishi aendelee kusikiliza na ndiyo maana ‘Leo Tena’
ina vipengele vingi.
Mtangazaji huyo anayependa kula ndizi nyama, ugali
dagaa na matembele, pilau kuku, firigisi na ugali hajawahi kujuta kutotimiza
ndoto zake na anaamini kuwa si watu wote wanafanya kazi walizopangiwa kufanya
wakati wanazaliwa kwa kuwa wakati mwingine unalazimika kufanya kazi kutokana na
mazingira ya wakati huo.
“Unajua ndoto zinabadilika kadri mtu anavyokua,
mimi nia yangu niliyokuwanayo ni kuwa daktari hivi,” anasema msichana huyo
aliyekuwa akipenda masomo ya Kiingereza, Historia, Kiswahili, Siasa, na Elimu ya
Viumbe wakati akisoma kidato cha kwanza hadi cha nne na alikuwa na uwezo mkubwa
wa kujieleza kulinganisha na wenzake darasani kwao katika Shule ya Shauritanga.
“Mimi kiukweli mpaka namaliza ‘form six’ sikuwahi kufikiria kama
nitakuwa mtangazaji,” anasema msichana huyo aliyehitimu ngazi hiyo ya elimu
mwaka 2005 mchepuo wa masomo ya Historia, Kiswahili, na Fasihi (HKL). Msichana
huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka 1998, hajabadilika ndoto tu, waliokuwa
wakimfahamu miaka ya nyuma wakiomwona leo watamshangaa, amekuwa mnene na
anahitaji kupungua. “Ila chakula kingine ambacho kinaniponza ni chips, kila siku
mchana ninakula chips kwa nini nisinenepe?,” anasema mtangazaji.
“Mimi
kabla sijawa hivi nilivyo nilikuwa mrefu, mwembamba, mweusi, ‘brown colour’
sijui ndiyo ‘chocolate colour’ wanaita,” anasema msichana huyo aliyebainisha
kwamba katika familia yao hakuna mtu mwenye kipaji kama chake. Si shabiki wa
michezo, ni msanii, licha ya kipaji cha kuchora, ni mbunifu wa vitu vya kisanii,
baada ya kuhitimu kidato cha sita alipanga kuendeleza kipaji hicho, akawa
anakwenda katika Nyumba ya Sanaa, Dar es Salaam kujifunza kubuni na kufuma nguo,
shanga na hereni.
Kama asingekuwa anafahamiana na, Fidesia Mwakitalema
(mtangazaji mwingine wa kituo hicho), pengine asingekuwa alivyo leo, mazoea ya
kwenda ofisi za Clouds kumsalimia rafiki yake ndiyo chanzo cha kufanya kazi
anayofanya leo, na wakati huo alikuwa hajafikiria kuwa mtangazaji. Siku moja
alipokwenda katika ofisi hizo mwaka 2005 alikutana na kijana, Daudi Gladis,
wakati wanaongea akamwambia kuwa ana sauti nzuri na endapo angekubali ushauri
huo angemtafutia nafasi ‘Radio Times’ ya Dar es Salaam, alikubali, wakaondoka
Kitega Uchumi wakaenda mtaa wa Lugoda wakamkuta,Taji Liundi, akampa nafasi ya
kufanya mazoezi.
Baada ya muda fulani wa mazoezi alielezwa asiende hadi
atakapoitwa, wakati anasubiri majibu babu yake mzaa mama alifariki dunia akaenda
Arusha msibani, akakutana na Meneja wa Radio Triple A, Bashir Mohamed, kwanza
alimpata nafasi ya kuendesha kipindi cha ‘Lunch time’, baadaye alikiacha,
akaendesha vipindi vya Makala ya Leo, na Taarab. Wakati akiwa Arusha, Meneja wa
Clouds FM Arusha, Charles Mhamiji, alimweleza kuwa anahitajika Dar es Salaam
akachukue mikoba ya Amina Chifupa kuendesha kipindi cha Leo Tena, ndiyo ulikuwa
mwanzo wa kuwa alivyo leo.
“Sasa hivi nakuwa, najifunza, hata upeo wangu
unaongezeka,” anasema na kubainisha kwamba majukumu yake yanamlazimu ajifunze
mambo mengi na kwa kuwa baadhi ya wanaomsikiliza wamemzidi umri, inambidi
atafute vitu vinavyolingana na umri wao. “Kipindi changu mimi siongei siasa,
naongea mambo yaliyopo ndani ya jamii, ‘social issues’ (masuala ya kijamii),”
anasema na kuongeza kwamba “‘for my age’ (kwa umri wangu) nimekuwa nikijikuta
naongea na watu wazima zaidi yangu.”
Ni mtoto wa pili wa, Peter Marius
na Rehema Shaaban Mushi, hafahamu kama asingekuwa mtangazaji leo angekuwa
anafanya kazi gani, ila anakumbuka kwamba aliwahi pia kuwa na ndoto za kuwa
mwanasheria, zikafutika baada kuhitimu kidato cha sita katika Shule ya Mkwawa,
Iringa. Ana kaka watatu, John, Ibrahim, na Marius, mama yao mzazi alifariki
dunia wakati Dina akiwa na umri wa miaka mitano, baba yake alioa tena, mama
aliyemlea.
Anasema licha ya maendeleo kiasi aliyonayo, safari yake ya
mafanikio ndiyo kwanza inaanza, hajafika anapotaka kufika kikazi na kimaisha.
Hajaolewa, hana mtoto, anapenda kupata watoto wawili, kapanga azae wa kwanza
muda si mrefu ujao ila hajui ataolewa lini, na nani atamwoa. “Ndoa naifikiria
lakini mimi sio kama vijana wengine wanaharakisha kuolewa ili mradi tu kuolewa.”
“Unajua sio wanaume wote ni wabaya, kuna wanaume wasikivu, wapole,
lakini bahati mbaya wanaangukia kwa wanawake ambao sio,” anasema na kudai kuwa
si wanawake wote wana sifa za kuwa mama au mke na amedai kuwa yeye atakuwa mke
na mama mzuri na hataki kuzaa mapema kwa kuwa anaandaa maisha ya watoto wake
kwanza. “Nitaolewa na mwanamume ambaye anafaa kuwa mume wangu mimi, na ambaye
anafaa kuwa baba wa watoto wangu mimi,” anasema na kudai kuwa si wanaume wote
wanafaa kuwa mume au baba wa watoto na akasema “ni wanaume tu lakini sio ‘father
material’”.
Anasema si lazima aolewe na ikiwa hivyo huenda wengi
hawatajua, ila akitimiza dhamira yake, atamwomba padre akafungishe ndoa hiyo
studio wakati akiwa katika kipindi cha Leo Tena. Akipata nafasi anapenda
kutazama sinema kwa kuwa anajifunza mambo mengi yanayomsaidia kwenye kazi zake.
Anapenda kusikiliza nyimbo za Kizungu hasa R&B, za dansi, za Kongo DRC hasa
za Koffie Olomide.
“Taarab napenda kama kupenda lakini kuna miziki
mingine ambayo napenda kuliko taarab,” anasema na kuwatuhumu baadhi ya waandishi
wa habari na wapiga picha kuwa wanatumia kalamu na kamera zao vibaya.
Anawashukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Clouds Entertainment, Ruge Mutahaba,
Muhamiji, Meneja wa vipindi Clouds, Sebastian Maganga, Meneja Ubunifu katika
radio hiyo, Ruben Ndege, Daudi Gladis, na wafanyakazi wenzake kwa kumwezesha
kufika alipo leo.
No comments:
Post a Comment