Na Mwandishi wetu
Dawa za Kichina za kuongeza makalio zimeleta kizaazaa cha aina yake kufuatia baadhi ya wanawake waliozitumia kwa lengo la ‘kuwachanganya’ wanaume kukiona cha mtemakuni.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, baadhi ya wanawake hao wakiwemo mastaa wa Bongo sasa wanahaha kutafuta njia za kupunguza miili yao baada ya kubaini uamuzi waliochukua awali haukuwa sahihi.
Imebainika kuwa, kufuatia matumizi ya dawa hizo wapo ambao sasa hawatamaniki kutokana na kuwa na maumbile ‘kichekesho’ hivyo kukosa ule mvuto waliotarajia.
Akizungumza kwa masikitiko, mwanamke mmoja aliyeonekana kuathirika na dawa hizo aitwaye Zaina wa Kinondoni, Dar alisema, awali alidhani kuwa na makalio makubwa kungesaidia kumdatisha mumewe lakini kumbe ndiyo alikuwa anatafuta matatizo.
“Nilikuwa na umbo langu zuri tu, wenyewe wanaita namba nane lakini shoga yangu akanishawishi nitumie dawa hizo akidai eti nitakuwa na kalio litakalomdatisha mume wangu, kumbe ndo’ kaniingiza mkenge.
“Ona nilivyo, kwa kweli najuta kutumia dawa hizi, hapa nilipo nimeambiwa kuna dawa inaitwa Mlonge inayotibu magonjwa mbalimbali, ndio naisaka ili niondokane na hali hii,” alisema mama huyo.
Naye Husna wa Magomeni aliliambia Risasi Jumamosi kuwa, yeye alikuwa akitamani kuwa na kalio kubwa na akashauriwa na marafiki zake atumie dawa hizo za Kichina lakini kwa anachokiona kwa dada yake, hataki kabisa kuzisikia.
“Dada yangu hatamaniki kwa dawa hizo. Alikuwa na umbo zuri lakini baada ya kuzitumia, amekuwa kituko na kila alipopita amekuwa akipata usumbufu kutoka kwa wanaume,” alisema Husna na kuongeza:
“Mbaya zaidi kumbe mume wake alikuwa hapendi mwanamke mwenye wowowo, sasa hivi hakuna maelewano ndani ya ndoa na mume wake amekuwa akimsaliti kwa kwenda kutafuta dogodogo nje, mimi sitaki kuingia huko.”
Tabia ya baadhi ya wanawake kutumia dawa za kuongeza makalio kama wanavyoonekana wanawake walio ukurasa wa mbele imekuwa ikiwaletea matatizo ikiwa ni pamoja na wengine kushindwa kuwajibika vilivyo wawapo faragha na wapenzi wao na kuzomewa wanapokatiza mitaani.
Gazeti hili linawashauri wanawake kukubaliana na maumbile waliyopewa na Mungu kwani kutafuta muonekano mpya kwa kutumia dawa hizo na nyinginezo ni kujitafutia madhara yanayoweza kuathiri maisha yao.
No comments:
Post a Comment