James Magai
MVUTANO mkali baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na
Kampuni ya Dowans, kuhusu hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania
iliyoamuru Tanesco iilipe Dowans zaidi ya Sh 94 bilioni, bado
unaendelea.
Mvutano huo unafautia hatua ya Tanesco kutafuta njia za
kisheria baada ya kuomba kibali cha kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani
kupinga hukumu na kuepukana na malipo hayo, lakini Dowans nayo ikaendelea
kuibana kwa kuiwekea pingamizi ili inyimwe kibali hicho.
Septemba 28
mwaka jana, Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es
Salaam, aliamua tuzo ya Dowans iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya
Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), isajiliwe ili kuwa hukumu halali ya
mahakama hiyo.
Kwa uamuzi huo, Tanesco sasa inatakiwa iilipe Dowans Sh
111 bilioni badala ya Sh 94 bilioni za awali.
Tanesco inapaswa kulipa
fidia hiyo pamoja na riba ya asilimia 7.5.
Hata hivyo shirika hilo la
umeme limeeleea kutokuridhishwa na hukumu hiyo na hivyo kutoa taarifa ya kusudio
la kukata rufaa.
Maombi ya kutaka kibali cha kukata rufaa hiyo,
yalitarajiwa kuanza kusikilizwa jana na Jaji Dk. Fauz Twaib lakini mahakama
ilishindwa kuyasikiliza baada ya Dowans kuweka pingamizi, ikiomba mahakama
isiipe Tanesco kibali.
Dowans iliiwekea Tanesco pingamizi hilo mwezi huu
ikidai kuwa kwa mujibu wa mkataba baina ya pande hizo, hukumu ya ICC haiwezi
kukatiwa rufaa.
Ni hoja kama hizo ilizozitoa Dowansa wakati wa pingamizi
la Tanesco kutaka Mahakama Kuu isiisajili tuzo yake na baadaye Jaji Mushi
alikubaliana na hoja za Dowans na kuamuru tuzo hiyo isajiliwe.
Jana Jaji
Dk Twaib aliziambia pande hizo mbili kuwa mahakama haitaweza kusikiliza maombi
ya Tanesco kuhusu kibali cha kukata rufaa hadi hapo pingamizi la Dowans
litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Jaji huyo, alizitaka pande hizo,
kuwasilisha hoja zao kwa njia ya maandishi na kwamba pingamizi hilo litaamuliwa
Februari 16 mwaka huu, baada ya kupitia hoja zote.
Ikiwa mahakama
itatupilia mbali pingamizi la Dowans, basi Tanesco itapewa kibali cha kukata
rufaa kupinga hukumu hiyo.
Lakini kama mahakama itakubaliana na
pingamizi la Dowans basi harakati za Tanesco kujinusuru katika malipo hayo kwa
njia za kisheria zitakuwa mashakani.
Hukumu ya Jaji Mushi ilionekana
dhahiri kwenda sambamba na kile alichowahi kukisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), Jaji Fredrick Werema kuwa hakuna uwezekano wowote wa kisheria kuepuka
malipo hayo.
Wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama alisema hadi wakati
hukumu hiyo inatoka, Tanesco ilipaswa kuilipa Dowans kiasi cha Sh 111bilioni
badala ya Sh94 bilioni.
“Fidia ya awali katika uamuzi wa ICC ilikuwa ni
Dola za Marekani 65milioni, lakini kwa sasa ukiweka na riba ya asilimia 7.5
fidia hiyo imeongezeka hadi takribani Dola za Marekani 72milioni ambazo ni kama
Sh111bilioni,” alisema Fungamtama.
Katika hukumu yake Jaji Mushi alisema
baada ya kupitia mwenendo na hoja za pande zote nimebaini kwamba si sawa kwa
mahakama hiyo kuingilia uamuzi wa ICC.
“Hivyo ninaagiza kuwa tuzo hiyo
isajiliwe na iwe huku halali ya mahakama hii,” alisema Jaji Emiliani Mushi
ambaye kabla ya kusoma hukumu hiyo alisema kuwa anatambua kuwa suala hilo
limekuwa na msukumo mkubwa wa kisiasa lakini akabainisha kuwa anafanya kazi kwa
mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment