WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM na CUF wameupinga muswada wa maslahi
ya mafao ya viongozi wa kisiasa na kusema kwamba utawabebesha wananchi wa
Zanzibar mzigo mkubwa.
Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni ambaye pia ni
Katibu wa wajumbe wa CCM katika Baraza la Wawakilishi Salmin Awadh alisema
wananchi wameukubali mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa matarajio makubwa
ya kuimarisha hali zao za uchumi na maendeleo.
Lakini Salmin alisema kwa
mujibu wa hali inavyokwenda inaonesha wazi wazi kwamba matarajio ya wananchi
katika kupiga hatua ya maendeleo yameanza kuyeyuka kidogo kidogo.
“Mimi
siungi mkono mswada huu kwa sababu hauna maslahi ya wananchi wa Zanzibar...huu
si wakati wa kuanza kujipangiya maslahi makubwa ya viongozi wakitaifa wakati
wananchi wetu hali zao ni duni,”alisema Awadh.
Mwakilishi wa Jimbo la
Chonga kwa tiketi ya CUF, Abdallah Juma Abdallah yeye alisema wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi wanavunja Katiba kwa sababu wanatakiwa kuupitisha mshahara wa
Rais lakini kazi hiyo haifanyiw na wajumbe.
“Kwa mujibu wa Katiba,
mshahara wa Rais unatakiwa kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi lakini mimi
nipo mwaka wa 14 sasa sijapata kusikia kuidhinishwa kwa mshahara huo,” alisema.
Alisema wananchi wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ambayo ni ya msingi
ikiwemo huduma za afya na elimu ambazo bado hazijatekelezwa kwa ufanisi.
Mwakilishi wa Viti Maalumu, Raya Suleiman (CCM) alisema huu si wakati muafaka wa
kupitisha mafao makubwa na manene ya viongozi wastaafu wa serikali.
“Tusubiri hadi uchumi wetu utakapokuwa mzuri na kustawi ndipo tuanze
kuwekeana maslahi makubwa ya mafao ya viongozi wastaafu wa serikali ya mapinduzi
ya Zanzibar,” alisema Raya.
Imeandikwa na Khatib Suleiman
No comments:
Post a Comment