JUMUIYA ya madaktari jana iliendelea ‘kuiendesha’ Serikali, tabia ambayo Waziri
Mkuu Mizengo Pinda ameiita dalili ya kuidharau Serikali, baada ya kukaidi kufika
katika kikao chake cha majadiliano huku wakisubiriwa na mawaziri wengine sita
pamoja na watendaji wengine wa juu serikalini.
Katika Ukumbi wa
Karimjee, watendaji kadhaa wa Serikali na waandishi wa habari walikuwepo katika
ukumbi huo kuwasubiri lakini hadi saa sita mchana hakukuwa na daktari hata mmoja
aliyetokea.
Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk. Haji Mponda, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia.
Wengine ni Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi, Waziri wa Mamabo ya Ndani ya
Nchi, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Afya, Dk, Lucy Nkya. Watendaji
wakuu serikalini ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Blandina Nyoni, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, Mganga Mkuu wa
Serikali, Deo Mtasiwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, wakuu
wa Polisi na wakuu wa wilaya.
Ilipotimu saa sita na nusu, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda aliwasili na kuzungumza na waandishi wa habari kuelezea uamuzi ya
Serikali baada ya kuwaita madaktari hao mara kwa mara kuzungumza nao bila
mafanikio.
Walivyoanza dharau
Alisema Januari 20 mwaka huu
jioni, ujumbe wa watu sita ulifika ofisini kwake na kutaka kuonana naye lakini
kutokana na kuwa na ratiba ya kwenda Arusha katika maziko ya Mbunge wa Arumeru,
Jeremiah Sumari, alimtaka Lyimo na Dk. Nkya kuzungumza nao na kumjulisha akiwa
Arusha.
Alisema katika mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Rais wa Chama
cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Mkopi, walifikia maelewano kurudi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuendelea na majadiliano ya madai yao ambapo
walienda kesho yake na kufikia muafaka wa utaratibu wa kuyafanyia kazi.
“Hata hivyo, waliporejea kwa wenzao kutoa ripoti ya matokeo ya
majadiliano na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, yalifanyika mapinduzi ya
uongozi ikaundwa Kamati ya Mpito kushughulikia madai ya madaktari ikiongozwa na
Dk. Stephen Ulimboka,” alisema Pinda.
Alisema alipotoka kwenye maziko
alipokea maombi yao ya kuonana naye na kupangiwa siku iliyofuata yaani Novemba
24, mwaka huu, saa 11 jioni.
Pinda alisema madaktari hao hawakutokea
huku namba za simu walizoacha kwa Katibu Mkuu zikiwa za waliopinduliwa na
hawakuwa tayari kufika tena ofisini. Pinda alisema alipozungumza na wahariri wa
vyombo vya habari Januari 25 mwaka huu, alitumia fursa hiyo kuwaomba waonane ili
awasikilize na kutafuta ufumbuzi wa madai yao akiamini wangefanyia kazi ombi
hilo baada ya kusikia katika vyombo vya habari.
“Pamoja na jitihada zote
hizo, hakuna aliyekuwa tayari kufuata ushauri nilioutoa, kwa hiyo si kweli
kwamba Serikali imetoa taarifa ya muda mfupi ya kutaka kukutana nao kama
walivyodai na kunukuliwa na vyombo vya habari,” alisema Pinda.
Ushauri
Tughe nao watupwa nje
Pinda alisema wakati wakiendelea na vikao vyao,
alikutana na mawaziri kadhaa pamoja na viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa
Serikali Kuu na Afya (TUGHE) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho,
Ramadhani Kiwenge na kukubaliana kutuma ujumbe wa Serikali ili ikawasikilize.
Alisema alituma ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Dk. Mponda, Dk. Nkya na
Ghasia kwenda kuonana nao kwenye ukumbi wa Hoteli ya Starlight Ijumaa iliyopita.
Alisema katika mkutano huo yaliyotokea ni tabu kweli, kulikuwa na dalili za
dharau huku wakipokewa kama siyo viongozi wao wakati waliwasilisha malalamiko
yao kuomba kuonana naye.
Alisema kila mawaziri hao walipotaka kutoa
maelezo ya malalamiko yao, waliandamwa na ghasia na waliporipoti kwake aliwataka
kutokukata tamaa. “Lyimo aliwapigia simu juzi (Ijumaa iliyopita) asubuhi lakini
hazikupokelewa ikabidi aende hadi katika Hoteli ya Starlight alipotafuta sana
ili awaone lakini alibahatika kuzungumza na mwenyekiti wao tu.
“Walikataa ujumbe wangu niliompa Katibu Mkuu kwa madai hawataki kwa
mdomo wanataka kwa barua, na aliponieleza nilimshauri asichoke akaandika barua
na kuwapigia simu wakamtaka awapelekee karibu na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni,” alisisitiza.
Alisema baada ya kupokea barua hiyo wakamwambia
kuwa watamjibu na ilipofika juzi (Ijumaa iliyopita) saa tatu usiku walimpelekea
barua ya kukiri kupata barua ya Waziri Mkuu na kutoa masharti matatu.
Pinda apewa masharti
Kwanza hawako tayari kukutana naye jana
hadi leo ili kuwasubiri wenzao wa mikoani wahudhurie, pili Ofisi ya Waziri Mkuu
iwajibu kwanza kwa maandishi madai yao kabla ya kukutana nao ili wapate nafasi
ya kujadili hoja moja baada ya nyingine. Na tatu, walitaka Serikali itoe tamko
wakati wa kuzungumza nao; kwamba haitatoa adhabu yoyote kwa daktari au mtumishi
wa kada yeyote wa afya kutokana na mgomo huo.
Uwezekano wa kufikia
muafaka
Pinda alisema kutokana na ukubwa wa mahitaji yao hawawezi
kutekeleza mara moja, lakini kutokana na mzungumzo ikiwa wangekutana, wangefikia
muafaka kwani uchumi wa nchi pia unaamua mambo mengi. Alisema kwa kutizama madai
yao, ufumbuzi ungepatikana kwa mazungumzo na siyo kutoa amri ya kutaka ifanyike
mara moja kama posho ya kulala kazini ambayo wanalipwa Sh 10,000 kweli ni ndogo
wangeweza kuiongeza.
Alisema kwa dai la posho ya kufanya kazi katika
mazingira hatarishi, lingeweza kuangalia kwa makundi kwa wale wanaofanya kazi
katika wodi za vichaa, katika mionzi na wengineo kwa kuwa inawezekana. Kuhusu
uhaba wa nyumba, alisema uahaba huo upo kwa sekta nyingi hata polisi na
wanajeshi, lakini kuna juhudi Serikali inafanya kwa kutambua hilo kwa kujenga
nyumba 10 kwa kila wilaya katika wilaya 18 hivyo wangeweza kujadili kutoa posho
bila kujali cheo.
Alisema kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira
magumu Serikali inaelewa na ipo tayari kutoa posho katika ameneo yasiyo na mvuto
kwa watumishi wa kada mbalimbali.
“Kama kuhusu usafiri, utaratibu wa
kukopeshana magari upo serikalini, kama tungekutana tungeona namna ya kuwapa
kipaumbele kwa wanaoishi maeneo yanayolazimu usafiri kwa kuwa mfuko huo
hautoshi,” alisema.
Kuhusu bima ya afya, Pinda alisema ni jambo la
kuangalia na kama fedha ipo, siyo mbaya kutibiwa maeneo mazuri na kuongeza kuwa
alidhani wangetaka kutibiwa bure na familia zao katika hospitali wanazofanyia
kazi. Alisema katika suala la mshahara siyo rahisi kutekelezwa kwa kiwango hicho
kwa mtumishi wa umma kwani ni lazima ufahamike kuwa utumishi wa umma pia unatoa
huduma, hivyo ni vyema kutambua kuwa wako wa kada mbalimbali ingawa wao ni
muhimu lakini kuna haja ya kuwa na uwiano.
Pia alisema kutaka uongozi
wote wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ujiuzulu, siyo jambo la msingi kwani
hawakutoa sababu ya msingi na kama kucheleweshwa kwa posho ni suala la serikali
siyo wizara. Alisema kama upo upungufu mwingine wasioujua serikalini hilo
lingejadilika lakini kuweka uongozi huo wote wa Wizara katika kundi moja kwa
tuhuma zisizojulikana siyo sawa.
Pinda alisema huduma duni kwa wananchi
ni moja ya changamoto kubwa serikalini ikiwa ni sehemu ya changamoto nyingi
zilizopo katika sekta mbalimbali ambazo Serikali wanafanyia kazi hatua kwa
hatua.
Uongozi wa mgomo mamluki
Alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari hao inayoongoza mgomo, Dk. Stephen Ulimboka siyo mtumishi wa Serikali
na hajasajiliwa kama daktari kwa kuwa usajili wake ulisitishwa na Baraza la
Madaktari mwaka 2005 baada ya kuongoza mgomo wa madaktari nchi nzima.
Kwa mujibu wa Pinda, Ulimboka alihitimu Shahada ya Udaktari katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2004 na kupata usajili wa muda wa baraza kisha
kupangiwa mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Alisema
Novemba mwaka 2005, alishitakiwa katika Baraza kwa Ukiukwaji wa Maadili ya
Taaluma ya Udaktari kwa kuitisha mgomo ambao ni makosa kimaadili na kukataa
kufika mbele ya baraza kujibu tuhuma hivyo shauri lake halikumalizika.
Pinda alisema mwaka 2006, Rais alimsamehe na kurejeshewa usajili wa
Baraza na kuruhusiwa kuendelea na mafunzo ya vitendo lakini hakuna taarifa kama
alimaliza mafunzo hayo kwa kuwa hajawasilisha cheti cha kumaliza mazoezi na
haifahamiki anafanya kazi wapi ingawaje inasemekana anafanya katika taasisi
isiyo ya kiserikali (NGOs) inayojihusisha na masuala ya Ukimwi.
“Katika
kumpa taarifa za msamaha wa Rais, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Baraza la
Madaktari kwa nyakati tofauti walimtaka kutojihusisha na mgomo au suala lolote
ambalo ni kinyume cha maadili ya taaluma ya udaktari,” alisema Pinda. Alisema
Ulimboka katika barua yake ya Februari 2, 2007 ambayo ipo serikalini alikiri
kwamba hatajihusisha wala kutoa ushawishi wowote kwa wengine kufanya vitendo
kinyume na maadili ya udaktari.
Akizungumza na gazeti hili, Ulimboka
alikiri kuitwa na Baraza la Madaktari mwaka 2005 na kweli alikuwa kiongozi wa
mgomo huo wa madaktari. Alisema mwaka 2007 alimaliza mafunzo yake ya vitendo
katika Hospitalia ya Mwananyamala na kupewa cheti chake katika Hospitali ya
Muhimbili alipofukuzwa kabla ya mgomo kama utaratibu ulivyo.
Alikana
kuandika barua Serikalini na kumtaka Waziri Mkuu kama anayo, aiweke hadharani
huku akikiri kutokuwa mtumishi wa serikali na kudai siyo sababu ya kumzuia
kutopigania maslahi ya madaktari.
No comments:
Post a Comment