KATIBAmpya ijayo haitakuwa muarobani wa kutibu shida zote za wananchi kama
viongozi hawatakuwa waadilifu na wazalendo kwa taifa lao.
Kauli hiyo
imetolewa juzi na Mbunge wa Kalambo Wilayani Sumbawanga, Josephat Kandege wakati
akifungua mdahalo wa kuhamasisha wananchi kushiriki katika mchakato wa kupata
Katiba mpya.
Mdahalo huo ulioandaliwa na muungano wa asasi zisizo za
kiserikali mkoani Rukwa (Rango) na kufadhiliwa na The Foundation for Civil
Society, ulifanyika katika Tarafa ya Matai wilayani humo.
Kandege
aliwataka Watanzania wasitarajie kupata maendeleo endelevu kwa kupitia Katiba
mpya iwapo viongozi hatakuwa waadifu na wananchi wasipokuwa wazalendo.
“Viongozi na wananchi kwa pamoja wanatakiwa kuwa waadilifu, wazalendo na
watangulize maslahi ya taifa kwanza kama kweli wanataka kuona maendeleo ya kweli
na ndipo hapo tutakapoona faida ya Katiba mpya tunayoisubiri kwa hamu,” alisema.
Aliwahimiza wananchi wa Kalambo kujitokeza kwa wingi mara baada ya tume
ya kukusanya maoni ya Katiba mpya itakapoanza kufanya kazi, ili washiriki katika
mchakato huo na kuacha kulalamika pasipo kuonyesha ushiriki wao.
Alisema
kujitoa na kutoshiriki katika utoaji wa maoni, ni kujisaliti wenyewe kwa kuwa
kutasababisha kuundwa kwa katiba isiyotatua kwa asilimia kubwa changamoto
zilizopo kwenye maeneo yao.
Alilalamikia upotoshwaji unaofanywa na
baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa kuwa Katiba ya sasa haifai
na kuwakumbusha kuwa katiba hiyo wanayoibeza, ndiyo chimbuko la kutukuka kwa
nchi hii.
Alitaka midahalo kama hiyo ifanyike kwa wingi ili wananchi
wajiandae ipasavyo kutoa maoni
yatakayosaidia kupata katiba itakayomjali
kila mmoja na kumlinda.
Pia aliwataka wananchi kutambua kuwa majadiliano
ya Katiba yanapaswa kulenga maslahi ya taifa na si chama chochote cha siasa.
Naye Katibu Mtendaji wa Rango, Stanley Mshana alisema upo umuhimu mkubwa
kwa makundi mbalimbali wakiwemo wazee, walemavu, wanawake na vijana kushiriki
kikamilifu
katika mchakacho wa kupata Katiba mpya.
No comments:
Post a Comment