NJOMBE

NJOMBE

Monday, January 30, 2012

Mwakyembe aibukia kanisani

•  Asema mafisadi wameshindwa kummaliza

HATIMAYE Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa mara ya kwanza ameonekana hadharani tangu atoke India kwa ajili ya matibabu.
Dk. Mwakyembe alionekana jana kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, katika ibada maalum ya kumshukuru Mungu kwa muujiza wa kupona ugonjwa uliokuwa unamsumbua.
Kiongozi huyo alisema kuwa nguvu za mafisadi zimeshindwa kummaliza.
Alisema kuwa hivi sasa anatarajia kuzunguka kwenye makanisa mbalimbali nchini kutangaza kushindwa kwa wabaya wake ambao walipanga kummaliza.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na madai kuwa Dk. Mwakyembe amelishwa sumu, lakini jana hakuweka bayana ni ugonjwa gani unaomsumbua na umesababishwa na nini
“Sikuwahi kuvaa viatu tangu nilazwe nchini India, lakini kwa mara ya kwanza leo nimevaa, shetani alipanga kunimaliza lakini ameshindwa.
Nimepanga kuzunguka kwenye makanisa kumzomea shetani (mafisadi) kwamba ameshindwa na kuwashukuru watu wa Mungu kwa maombi yao,” alisema.
Kikosi cha wapambanaji wa ufisadi
Katika ibada hiyo, Dk. Mwakyembe alisindikizwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; mbunge wa Kahama James Lembeli (CCM); mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM); na Aloyce Kimaro, aliyekuwa mbunge wa Vunjo.
Makada hao waliojipambanua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi walisema kuwa kamwe hawataogopa chochote katika mapambano dhidi ya ufisadi kwa kuwa neema inakuja siku za usoni.
Sitta alisema machozi ya Watanzania hayawezi kupotea bure dhidi ya mafisadi ambao wameamua kuzitumia rasilimali za taifa kujinufaisha.
“Neema inakuja na nchi itarudi kwenye mstari ambao Mwalimu Julius Nyerere alitamani taifa liwe, hakutaka liwe hivi leo ambapo baadhi ya watu wanatumia migongo ya wenzao kupata mafanikio.
Nchi leo imejaa magenge ya waovu ambao wamejipanga kuitafuna bila kujua Tanzania ni ya Mungu, mimi pamoja na kundi langu la kupambana na ufisadi hatuogopi chochote,” alisema Sitta.
Sitta alitumia muda mwingi kuzungumzia unyonywaji unaofanywa na waovu (mafisadi) ambao wamewaacha wananchi wakiishi maisha magumu bila msaada wowote.
Huku akishangiliwa na umati mkubwa wa waumini waliohudhuria kanisani hapo, Sitta alisema viongozi wengi wanatumia dhamana waliyopewa kwa ajili ya kuliibia taifa kitendo kisichokubalika mbele ya Mungu.
Akitumia kifungu cha Biblia (Habakuki 1:2-4) alisema kilio cha Watanzania juu ya maovu na kutotendewa haki kitafutwa hivi punde.
“Hata kwenye nchi yetu wananchi wanalia juu ya shida walizonazo, huku uovu na udhalimu ukiendelea; hakuna pa kukimbilia, haki hakuna kama ipo imelegea na inawanufaisha mafisadi.
Mikopo ya wanafunzi inacheleweshwa makusudi kwa lengo la wanafunzi hao kufukuzwa kwa kukosa ada, nchi inanyonywa, lakini Mungu anaona na iko siku ataingilia kati, hawezi kukubali watu wake wateseke,” alisema.
Alienda mbali zaidi na kusema nchi itapona na uongozi utabadilika.
Ugonjwa wa Mwakyembe
Waziri Sitta amesisitiza kwa mara nyingine kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Harrison Mwakyembe, alilishwa sumu.
“Nilishasema na narudia tena alilishwa sumu; mimi nimekuwa naye muda mrefu akiwa India na madaktari wa kule wanasema alilishwa sumu, kama wanabisha vyombo vya uchunguzi vitoe majibu haraka,” alifafanua.
Alisema miguu ya Mwakyembe ilikuwa kama ya tembo na ngozi yake ilikuwa inatoa unga.
Anne Kilango atema cheche
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, alisema ataendelea kupambana na kamwe hatachoka, kwani amevumilia mengi katika kuwawakilisha wanyonge.
“Naipenda nchi yangu na napenda haki, kiongozi bora ni yule anayetenda haki kwa wananchi wake, nitaendelea kusimamia na kusema kweli,” alisema.
Alisema amezaliwa kwa ajili hiyo na ataendelea kupigania haki ya wanyonge.
James Lembeli anena
Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), amesema licha ya Bunge kuwa ni mhimili wa nchi lakini ndiko kwenye ufisadi mkubwa.
“Wachungaji na viongozi wa dini liombeeni Bunge kwani watenda maovu wako huko, kwani wabunge wengi husimama kwa ajili ya kutetea nafsi zao na kamwe Askofu Josephat Gwajima usikubali mafisadi kuathiri kanisa lako,” alisema.
Kauli ya Aloyce Kimaro
Kimaro naye alisema yote yanawezekana kama Mungu alivyosema na siku zote ukweli unahitajika.
Kimaro aliongeza kuwa ukweli hauchagui mtoto au mkubwa na vigumu kwao kutendewa baya kwa vile Mungu mara nyingi hupenda mkweli.
“Mkiona wala rushwa semeni ukweli, hakuna watakalowafanya; Mungu atawalinda kutokana na kumpenda mtu wa namna hiyo,” alisema.
WAKATI huo huo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amechangisha zaidi ya sh milioni 204 katika harambee ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), lililoko mjini Shinyanga, hivyo kuvuka lengo halisi.
Lowassa ambaye alikuwa mgeni rasmi jana katika harambee hiyo iliyolenga kukusanya sh milioni 115, kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo hatua ya kuezeka, alikuwa kivutio kikubwa kwa waumini ambao wakati mwingi walikuwa wakimshangilia.
Akizungumza katika harambee hiyo, iliyochangisha sh milioni 136 zilipatikana taslimu na ahadi ya sh milioni 68, Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli (CCM), alitoa wito kwa Watanzania kujenga milango mipana ya ushirikiano wa kimaendeleo.
Alisema, Watanzania wanao wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba wanadumisha maradufu ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu kuchangia shughuli mbalimbali za madhehebu ya dini badala ya kutegemea msaada kutoka kwa wahisani.
“Zamani tulikuwa tukitegemea sana Wazungu watusaidie, lakini kwa sasa tunashukuru hali hiyo imeenda inatoweka,” alisema Lowassa ambaye alitumia muda usiozidi dakika nne kuhutubia kwenye harambee hiyo.

No comments:

Post a Comment