ZAIDI ya watu 30 wakiwepo watoto wadogo wanne wamenusurika kuzama katika Ziwa
Victoria baada boti mbili kugongana eneo la Mwikoko karibu na jengo la maofisa
wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Manispaa ya Musoma
mkoani Mara.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 11 alfajiri, ambapo boti ya
uvuvi yenye namba za usajili RMU 5234 iligongana na boti ya abiria iliyojulikana
kwa jina la mv Nyanganira inayomilikiwa na Ramadhan Nyanganira.
'Habarileo' lilifika eneo la ajali na kushuhudia boti hizo zikiwa
zimeharibika huku kukiwa na madai ya watu kutoonekana baada ya baadhi yao
kuokolewa. Baadhi ya mashuhuda na abiria walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni
mwendo kasi wa boti hizo na kutozingatia sheria za unahodha.
“Kabla ya
ajali kutokea kama meta mia moja hivi, abiria walimuambia nahodha aangalie mbele
boti iliyokuwa ikija, lakini alishindwa kumiliki vyema boti hiyo na alipokata
kona tu boti ya uvuvi iligonga katikati,” alisema mmiliki wa boti hiyo,
Nyanganira na kuongeza:
"Hatuwezi kusema kuwa hakuna mtu aliyepoteza
maisha, ukweli utapatikana baada ya siku moja au mbili”. Abiria wa boti hilo
aliyejitambulisha kwa jina la Eunice Maagi, mkazi wa Kiabakari aliyedai alikuwa
akitoka kwenye msiba katika kijiji cha Kibuyi wilayani Rorya, alisema kuwa hadi
alipookolewa na kupata fahamu vizuri, hakuna mtu yeyote aliyelalamika kama
ndugu, jamaa au rafiki yake haonekani.
“Hakuna niliyemsikia analalamika
kuwa amepotelewa na mtu sijui kwa kuwa bado
tumechanganyikiwa na pia
kutojuana kutokana na kila mtu kuwa na safari yake, lakini sisi tulikuwa kama
sita na wote tumeokolewa na tupo salama,” alisema Maagi.
No comments:
Post a Comment