SAKATA la madaktari nchini linazidi kuchukua sura mpya baada ya wataalamu hao
kukataa hoja za ujumbe wa Serikali ulioongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Utumishi, Hawa Ghasia huku wakigoma kusikiliza kauli yoyote kutoka kwa Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii Dk Hadji Mponda
Wakati mawaziri hao wakikumbwa
ana tafrani hiyo tayari wauguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na
ile ya Mkoa wa Dodoma wametishia kusitisha utoaji huduma ifikapo Jumatatu kama
masuala yao hayajapatiwa ufumbuzi.
Vigogo wa Serikali waliofika kukutana
na madaktari hao jana ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na
naibu wake, Dk Lucy Nkya, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni, Mganga
Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
Tukio hilo lilitokea jana kwenye Ukumbi wa
Hoteli ya Star Light, Jijini Dar es Salaam ambako madaktari hao walikusanyika na
baadaye kupewa taarifa kuwa kuna ujumbe wa Serikali utafika kwa majadiliano.
Madaktari hao waliwatimua ujumbe huo baada ya kuusikiliza juu ya wito wao wa
kuwataka wasitishe mgomo ili wafungue ukurasa wa majadiliano, wakajibiwa kuwa
kwa sasa ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo na siyo ahadi.
Ujumbe huo
wa Serikali uliwasili ukumbini hapo majira ya mchana na kukaribishwa na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka ambaye baada ya
kuwawekea viti pembeni mwa jukwaa kuu, aliwatambulisha kwa washiriki. “Ugeni
tuliokuwa tunasubiri umefika, si rahisi sisi wote kuwafahamu ni vema
wangejitambulisha wao kwa majina kisha tuendelee na utaratibu tuliojiwekea,”
alisema Dk Ulimboka.
Mara baada ya kauli hiyo, wageni hao walianza
kujitambulisha. Wa kwanza alikuwa Waziri Ghasia aliyewasalimia madaktari hao na
kujitambulisha kisha kueleza kuwa aliongoza ujumbe huo kuwasilisha taarifa ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Dalili mbaya kwa ujumbe huo, zilianza kujitokeza
walipoitika kwa nguvu salamu ya Waziri Ghasia huku wakiwanyamazia Waziri wa Afya
na maofisa waandamizi wa wizara hiyo.
Baada ya tukio hilo kumalizika, Dk
Ulimboka alitoa taratibu za mkutano kuwa ni kusoma taarifa maalumu iliyoandaliwa
kwa ajili ya kupelekwa kwa Waziri Mkuu. “Sisi hapa tutawakabidhi taarifa
iliyoandaliwa na madaktari ambayo ni maalumu kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na
baada ya kuwasomea, tutawakabidhi kisha tusubiri majibu ya taarifa yetu tukiwa
hapahapa,” alisema Dk Ulimboka.
Dk Ulimboka alisoma taarifa hiyo mbele
ya wageni hao ambayo ilitaja madai yao kadhaa ikiwemo kumtaka Waziri Ghasia
kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwaondoa katika wizara hiyo, Waziri Mponda na
naibu wake Dk Nkya, Katibu Nyoni na Mganga Mkuu, Dk Mtasiwa.
Mara baada
ya kusoma taarifa hiyo alikabidhi barua hiyo kwa Waziri Ghasia huku akisisitiza
kuwa wataendelea na mgomo hadi watakapopatiwa majibu ya hoja
zao.
“Tunaomba taarifa hiyo imfikie haraka Waziri Mkuu, ijadiliwe kwa
haraka na kutoa majibu yatakayotupatia ufumbuzi ili nasi turudi kazini tukaokoe
maisha ya Watanzania,” alisema Dk Ulimboka ambaye kwa kauli yake iliashiria
kufunga mjadala.
Baada ya kauli hiyo, Waziri Ghasia alisimama na
kueleza kuwa wao walifika wakiwa na ujumbe toka kwa Waziri Mkuu hivyo ni vema
wangekubaliwa wauwasilishe ambapo alimtaja Waziri wa Afya Dk Mponda kuwa
angeusoma.
Dk Ulimboka alijibu hoja hiyo akisema “Madaktari hatuna tatizo
na ujumbe toka kwa waziri Mkuu Mizengo Pinda ila ujumbe kutolewa na Waziri wa
Afya Dk Hadji Mponda hatukubali kwasababu hatuna imani naye labda kama kweli ni
taarifa, ungesoma wewe,” alisema Dk Ulimboka na kukaa chini.
Waziri
Ghasia alikubaliana na hoja hiyo na katika kuwasilisha taarifa hiyo, alisema
alisononeshwa kusoma majibu yanayohusu madai ya madaktari hao kwa niaba ya
waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Afya wakati yeye (Dk Mponda) akiwepo.
Ghasia alisema wizara imetafakari kwa kina suala la madaktari waliokuwa
kwenye mafunzo katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili na kuwarudisha kwenye kituo
hicho cha kazi huku ikiahadi kuwalipa stahili zao.
“Wazira imetafakari kwa
kina na imeamua kuwarejesha madaktari wote waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo
katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili na wanatakiwa kuripoti katika vituo hivyo
vya kazi kuanzia Jumatatu,” alisema Ghasia.
Kuhusu madai mengine,
alisema Serikali itaendelea na majadiliano ya pamoja huku akiwaomba warejee
kazini.
“Sisi tuwaombe tu kwamba madai yenu yote Serikali inayafanyia kazi.
Suala la nyumba tayari tumeshapata fedha kutoka Global Fund kwa ajili ya ujenzi
wa nyumba za madaktari ili waweze kukaa karibu na vituo vyao vya kazi,” alisema
Ghasia. Akijibu ombi la kuwataka warejee kazini, Dk Ulimboka alisema hilo
litategemea majibu ya taarifa walioiwasilisha kwa Waziri Mkuu, ambapo
alisisitiza kuwa wao wataendelea na mikutano katika ukumbi huo.
“Sisi
tutaendelea na mikutano kujadili taarifa yenu na pia tungeshauri taarifa hii
mtuletee kwa maandishi, lakini pia tunasubiri majibu ya taarifa yetu
tuliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambayo tumeitoa kwa maandishi,”
alisema Dk Ulimboka. Dk Uliomboa aliwataka wawakilishi hao wa Serikali kutambua
kuwa ujumbe haukuwa wa kushawishiana kurudi kazini bali ni wa kupeana taarifa.
Kauli hiyo iliashiria kwamba hoja ya ujumbe huo haina uzito wa
kuwashawishi kuacha mgomo huku wakikataa hoja zao sasa kujadiliwa na wizara
badala yake walisisitiza Waziri Mkuu kushughulikia suala hilo. Walimtaka
Waziri Mkuu, kutoa majibu ya madai yao kwa wakati ili asiwafanye kufikia hatua
ya kusitisha huduma katika vitengo vya dhararu.
“Mgomo huu unaendelea
nchi nzima hadi majibu ya madai yetu tuliyowasilisha kwa Waziri Mkuu yamepatiwa
majibu.
Tunashauri kazi hiyo ifanywe haraka vinginevyo tusije tukashawishika
kusitisha huduma kwenye vitengo vya dharura,” alisema Ulimboka.
Tishio
la mgomo zaidi
Wakati huo huo, Chama cha Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, kimesema kuwa wauguzi wataendelea kutoa huduma kwa kusuasua hadi
Jumatatu na kama suala hilo litakuwa halijapatiwa ufumbuzi, watasitisha huduma
na kufunga hospitali.
“Sisi tutaendelea kutoa huduma katika mazingira ya
shida hivi mpaka Jumatatu tu,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Paul Magesa.
Habari kutoka katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma zilieleza pia kuwa, kwa
sasa hakuna wagonjwa wapya wanaopokelewa na kuwa waliopo wodini wakitoka,
hospitali hiyo nayo itasitisha kutoa huduma. MWISHO
No comments:
Post a Comment