NJOMBE

NJOMBE

Thursday, January 26, 2012

Mgomo wa madaktari wasambaa mikoani

Mwenyekiti wa Madaktari ,Dk.Ulimboka Steven (katikati) akizungumza wakati wa mkutano wa madaktari kutoka katika Hospitali zote za Rufaa kuhusu kuendeleza mgomo wao kama serikali haitawatimizia madai yao,mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Don Bosco Upanga jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Dk Edwin Chitage na Kulia ni DK Rahma Hingera.
SASA WAINGIA DODOMA, MBEYA, PINDA AWAANGUKIA ATAKA WAZUNGUMZE

MGOMO wa madaktari ulioanza juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), umesambaa na kuingia katika Hospitali za Mwanyamala na nyingine katika Mikoa ya Dodoma na Mbeya.Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ametoa tamko akiwataka wawakilishi wa madaktari hao wafike ofisini kwake wakati wowote ili wazungumze naye na kupata suluhu ya tatizo hilo.Katika hospitali ya Muhimbili, mgomo huo jana uliingia katika siku ya pili huku madaktari wastaafu wanaofanya kazi kwa mkataba, wakipanga kuwasilisha pendekezo kwa uongozi wa hospitali hiyo kutaka kuwapunguzia kazi kwa kuondoa shughuli za upasuaji.
“Tunadhamiria kupeleka pendekezo kwenye uongozi wa hospitali hii ili kuwaeleza dhamira yetu ya kupunguza baadhi ya huduma zinazotolewa ikiwamo upasuaji. Hilo ni kutokana na madaktari wanaotakiwa kufanya kazi hiyo kuwa kwenye mgomo,” alisema mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe.“Sisi katika idara hii tupo wawili tu, wagonjwa wanaokuja ni zaidi ya 150 tutawahudumiaje na wakati huohuo tunaitwa wodini? Alihoji daktari huyo.
Katika chumba cha wagonjwa wa dharura ambako juzi huduma ziliendelea, hali ilikuwa tofauti jana, kulikuwa na madaktari wawili tu ambao wameeleza kuwa wenzao wameingia kwenye mgomo.
Ocean Road
Katika Hospitali ya Ocean Road, wahudumu waligoma kuwapokea wagonjwa wapya, hivyo huduma kutolewa katika kitengo cha mionzi na madaktari bingwa.“Hili ni jambo la kusikitisha na ni aibu kwa Serikali kwani mgomo huo utasababisha vifo vya mamia ya watu,” alisema mmoja wa wagonjwa katika hospitali hiyo, Florence Mushi.
Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alithibitisha wauguzi kutopokea wagonjwa wapya jana na kueleza kuwa ni kwa kuwa madaktari hawapo kazini.“Hatuwezi kuwapokea wagonjwa wakati watu wa kuwatibu hawapo. Hapa huduma zipo kwenye kitengo cha madaktari bingwa, mionzi na wagonjwa walioko wodini tu,” alisema.
Mwananyamala
Huduma katika Hospitali ya Mwananyamala pia zilikuwa za kusuasua jana baada ya madaktari wanafunzi wanaotoa huduma hospitalini hapo kuendesha mgomo baridi.Jana mchana madaktari walionekana wakiingia na kutoka wodini bila kutoa huduma huku ndugu wa baadhi ya wagonjwa wakieleza kusikitishwa na hatua hiyo. Baadhi wa wafanyakazi wa hospitali hiyo walisema kuwa mgomo hospitalini hapo upo ingawa haujashamiri.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Kaliameli Wandwi hakutaka kuzungumza lolote kuhusu mgomo huo, alipobanwa alisema: “Sina muda wa kuongea na waandishi wenzako nimewakatalia tangu asubuhi.”
Mbeya
Mkoani Mbeya madaktari 75 wamegoma katika Hospitali ya Rufaa huku wagonjwa katika kitengo cha Wazazi Meta, wakilalamika kukosa huduma bila kupata maelezo yoyote kutoka kwa wauguzi.Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wagonjwa walisema kuwa mgomo huo ni hatari kwa wananchi ambao hali zao ni duni kumudu matibabu katika hospitali za kulipia.
“Tungekuwa na uwezo kifedha tungekwenda katika hospitali za kulipia lakini sasa ni vigumu kwetu ambao hali zetu ni duni,” alisema Neema Emmanuel.Mgonjwa mwingine Winfrida Rashid alisema: “Hapa rufaa inaonekana kuna huduma zinaendelea kwa baadhi ya madaktari na manesi, lakini kasi imepungua, inawezekana wengine wakafanya kama kuigiza.”
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Eleuter Samky alisema madaktari waliogoma ni 75, kati yao 10 wakiwa waajiriwa na 65 wanafunzi.
Alisema hali ni mbaya kwa wagonjwa kutokana na kuwepo kwa mgomo huo na kwamba wanaofanya kazi ni wafamasia na madaktari bingwa na kitengo cha upasuaji na baadhi ya wauguzi katika kitengo cha mifupa.
Madaktari hao waliogoma, kila walipokutana na waandishi wa habari waliwaonyesha karatasi zilizokuwa zimeandikwa baadhi ya madai yao kwa Serikali.
Dodoma
Mkoani Dodoma nako mambo si shwari baada ya madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Mkoa kugoma na kutumia siku nzima ya jana katika mkutano.Kitengo kilichoathirika zaidi na mgomo huo ni cha wagonjwa wa nje ambako kimsingi hakuna huduma yoyote iliyokuwa inatolewa huku baadhi ya madaktari wakisema kuwa wataendelea na mgomo wao huo hadi Serikali itakapotoa majibu ya madai yao.
“Ndugu yangu amelazwa tangu jana (juzi) asubuhi kwa ajili ya operesheni kubwa na hatakiwi kula chochote tangu hiyo jana (juzi) tukitegemea kuwa angefanyiwa operesheni leo,” alisema ndugu wa mgonjwa mmoja ambaye hakutaka kutajwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia madai ya watumishi wa Afya katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Yahya Magaswa alisema wanaungana katika mgomo na madaktari wenzao nchini kote ili kuishinikiza Serikali kufanyia kazi madai yao ya msingi.
“Tumemweleza Katibu wa Mkoa madai yetu ya msingi na sababu za kuungana na wenzetu katika mgomo ulioanza kote nchini... ameahidi kuyafanyia kazi na sisi tumekubaliana kutoa huduma za dharura tu mpaka kesho jioni tutakapokutana tena kujadili majibu yatakayotolewa na Serikali,” alisema Magaswa.

Pinda ataka mazungumzo
Akizungumzia Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema haoni sababu ya kukwama kwa mazungumzo kati ya serikali na madaktari.Waziri mkuu Pinda alisema Dar es Salaam jana kuwa yuko tayari kukutana na wawakilishi wa wanataaluma hao na kutuma salamu popote walipo wakisikia ujumbe wake, wafike wamwone kabla hajaenda bungeni Dodoma, Jumamosi.
“Kupitia kwenu vyombo vya habari, naomba mfikishe ujumbe huu kwamba niko tayari kufanya mazungumzo na madaktari hao. Sijali kama ni uongozi gani jambo la msingi uwe unawakilisha madaktari,” alisema.
Alisema anaumia roho kuona wagonjwa wanapata shida hospitalini hasa Muhimbili kutokana na mgomo huo ambao unazungumzika na kutatulika.
Alisema akikutana na madaktari hao, atawabembeleza wasitishe mgomo na kuendelea kutibu wagonjwa huku, wao na Serikali wakiendelea na mazungumzo ya kudai maslahi yao.
Alisema kimsingi, madaktari hao ambao wako kwenye mafunzo ya vitendo walikuwa na madai ya msingi baada ya kukosa posho zao za Novemba na Desemba, lakini jambo hilo halifungi mlango wa mazungumzo.
Pinda alisema kinachofanyika kwa madaktari hao ni kulipwa posho ambazo si mshahara hivyo, fedha zake zinatoka katika matumizi ya kawida (OC), ambayo wakati mwingine huchelewa.
Kwingine shwari
Katika baadhi ya mikoa ikiwamo Pwani na Mwanza madaktari walikuwa wakiendelea na kazi kama kawaida.
Wagonjwa waliohojiwa jana katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha walisema huduma ziliendelea kama kawaida hali ambayo iliripotiwa pia katika hospitali nyingine mkoani Pwani kama Kituo cha Afya Chalinze na Hospitali za Wilaya Mkuranga, Rufiji na Bagamoyo.
“Mimi si msemaji wa mkoa lakini kwa vile ni kiongozi wa ulinzi na usalama nakuthibitishia hakuna mgomo ingawaje kuna watu pengine walipenda uwepo lakini leo hakuna,” alisema Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Henry Clemence.
Katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, madaktari waliendelea na kazi. Mmoja wa madaktari waliokuwa kazini, Dk Denis Kashaija alisema wanaendelea kuchapa kazi za kutoa huduma kwa wagonjwa.“Kama unavyoshuhudia, sisi na wauguzi hatujagoma kutoa huduma kwa wagonjwa tunaendelea na kazi labda itokee kuanzia kesho,” alisema Dk Kashaija.
Habari hii imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Kenneth Goliama na Ellen Manyangu, Dar; Julieth Ngarabali, Pwani; Anthony Gervans, Mwanza; Hamisi Mwesi, Dodoma; Brandy Nelson na Godfrey Kahango, Mbeya.




No comments:

Post a Comment