SERIKALI imetangaza kuwafuta kazi madaktari wote watakaoendelea na mgomo huku
ikiviamrisha vyombo vya dola kuwakamata watakaodiriki kufanya mikutano kwenye
maeneo mbalimbali.
Msimamo huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Karimjee
na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana
mara baada ya madaktari kushindwa kufika kwenye mkutano ulioandaliwa kuzungumzia
madai na mgomo wa wataalamu hao.
Pinda aliwaamaru madaktari wanaoendelea na mgomo katika mikoa saba nchini
kurejea kazini mara moja leo asubuhi huku akiweka wazi watakaokiuka agizo hilo
watapoteza ajira zao.
Alisema serikali inatambua madaktari hao wanaongozwa na kamati ya mpito
isiyotaka suluhu licha ya juhudi zilizofanywa za kuwaita kushughulikia madai
husika.
“Serikali tayari imechukua tahadhari ya kukabiliana na hali hii kwa kuagiza
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupeleka madaktari wake katika
hospitali za mkoa wa Dar es Salaam ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini.
Kwa hiyo huduma zitaendelea kama kawaida,” alisema Pinda.
Katika mkutano huo Pinda aliongozana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya; Waziri wa Nchi Ofsi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia; Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussein
Mwinyi; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha; na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika.
Akionekana kukerwa na kitendo hicho cha madaktari hao kushindwa kukutana
naye, Pinda alisema kuanzia leo ameviagiza vyombo vya dola kuzuia mikutano yote
ya madaktari hao, akisema ni kinyume cha sheria ingawa serikali ilikuwa
ikiwavumilia tu.
“Mgomo wao si sahihi kwa sababu haukufuata taratibu za kuuitisha. Wao
walipaswa kutangaza mgogoro na kisha kutoa notisi ya siku 60, jambo ambalo
hawakufanya,” alisema Pinda na kukipongeza Chama cha Wafanyakazi wa Afya na
Serikali Kuu (Tughe) kwa kutambua hoja za madaktari hao lakini wakasema njia
iliyotumika si sahihi.
Pinda ambaye aliwasili ukumbuni hapo saa 6:12 mchana badala ya saa 4:00 kama
ratiba ilivyokuwa, alianza kwa kufafanua chimbuko la mgomo huo na hatua kadhaa
zilizochukuliwa na serikali kuutatua.
Alisema tangu mwishoni mwa Desemba mwaka jana, kulikuwa na madai ya wataalamu
mbalimbali waliokuwa kwenye mazoezi kwa vitendo (interns) kwamba wangeitisha
mgomo kwa sababu ya kucheleweshewa posho zao; alisema juhudi zilifanyika na
wakalipwa madai hayo yaliyokuwa yakifikia sh milioni 876.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya malipo kufanyika, mgogoro ulihama kutoka
kwa interns na kuwahusisha wataalamu wa kada nyingine za afya wakiwemo madaktari
na kwamba kwa kuwa interns hao nafasi zao zilikuwa zimezibwa wakati wakiwa
wamegoma, serikali iliona ni vyema kuwasambaza kwenye hospitali nyinge jijini
hapa.
“Uhamisho huo ulifanywa kwa nia njema ila wenzetu waliutafsiri kama adhabu ya
kuwakomoa interns hao na kupitia Chama chao cha Madaktari (MAT), walileta madai
kuwa tuwarejeshe Muhimbili wakitoa sababu nyingi ambazo kimsingi tuliona zina
mantiki,” alisema Pinda.
Aliongeza kuwa wakati wakiwa kwenye majadiliano ya hoja hiyo na yeye
kuonyesha nia ya kukutana nao, MAT walienguliwa na jukumu hilo kupewa Jumuiya ya
Kamati ya Mpito iliyoongozwa na Dk. Stephen Ulimboka, ambayo ilitoa madai
nane.
Katika madai yao walitaka posho ya kulala kazini ya sh 10,000 kwa siku,
ilipwe kwa kiwango cha asilimia 10 ya mshahara wa mwezi, posho ya kufanya kazi
katika mazingira hatarishi iwe asilimia 30 ya mshahara wa mwezi; na posho ya
nyumba walipwe asilimia 30 ya mshahara wa mwezi.
Madai mengine ni kupandishwa kwa posho ya kufanya kazi katika mazingira
magumu zifikie asilimia 40 ya mshahara, kupatiwa posho za usafiri kwa asilimia
10 ya mashajara iwapo itashindikana wapatiwe usafiri wa kwenda na kurudi
kazini.
“Wanadai mshahara wa sh 700,000 ni mdogo sana kwa daktari anayeanza kazi,
hivyo wanapendekeza alipwe sh 3,000,000 kwa mwezi. Wanataka kupatiwa bima ya
afya pamoja na familia zao kwa kupewa kadi za kijani na wanataka interns
warejeshwe Muhimbili bila masharti yoyote,” alisema Pinda.
Hata hivyo, akichambua madai hayo alisema serikali haiwezi kuyapatia ufumbuzi
mara moja madai hayo ila taratibu za kuyapatia ufumbuzi zinaendelea huku
akikanusha kuwa daktari anayeanza kazi analipwa sh 700,000 bali ni sh
957,7000.
Alisema madaktari hao wamependekeza wanaoajiriwa hivi sasa walipwe mshahara
wa sh milioni 3.5 wakati watumishi wa kada nyingine kama wahandisi wanaanza na
sh 600,000 na wahasibu wanaanza na mshahara wa sh 300,000; kwamba posho zote
wanazodai zikijumuishwa zinafikia asilimia 120 ya mshahara wa daktari mmoja.
“Kwa mujibu wa mapendezo yao ina maana kiwango cha kuanzia mshahara wa
mhudumu wa afya kitakuwa sh 670,316 na mshahara wa juu utakuwa sh mil. 8.1 kwa
mwezi. Utekelezaji wa pendekezo hili utagharimu sh bil 83.5 kwa mwezi ambayo ni
sawa na sh bil. 417.5 kwa kipindi kilichobaki cha miezi mitano,” alisema.
Pinda alifafanua kuwa kwa mujibu wa mapendekezo hayo mshahara na posho,
daktari anayeanza kazi atapata sh mil. 7.7 na daktari mshauri mwandamizi atapata
sh mil. 17.2 kwa mwezi.
“Endapo madai hayo yatatekelezwa kwa mwaka mmoja jumla ya mishahara yao
itakuwa sh bil. 799.7 badala ya sh bil. 222. 2 hadi kufika Juni 2012.
Kiongozi wao si daktari
Katika hatua nyingine, Pinda alisema kuwa katika uchunguzi wao walibaini kuwa
kiongozi wa mgomo, Dk. Ulimboka alihitimu shahada ya udaktari katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam mwaka 2004 na kupata usajili wa muda No. 2022 wa Baraza la
Madaktari mwaka huu na kupangiwa internship Muhimbili.
Alisema kuwa Novemba 2005, aliongoza mgomo wa madaktari nchini na usajili
wake ulisitishwa na kushtakiwa mbele ya baraza hilo kwa ukiukaji wa maadili ya
taaluma ya madaktari kwa kutishia na kufanya mgomo.
Mwaka 2006 Rais alimsamehe na hivyo kurejeshewa usajili na baraza na
kuruhusiwa kuendelea na internship.
“Katika kumpa taarifa za msamaha wa Rais, Wizara ya Afya na Baraza la
Madaktari walimtaka Dk. Ulimboka kutojihusisha na migomo au suala lolote kinyume
na maadili ya udaktari ambapo Februari 2, 2007 alikiri sharti hilo kwa
maandishi.
Hadi sasa hakuna taarifa kama alimaliza internship kwa kuwa hajawasilisha
cheti cha kumaliza mazoezi hayo na hatuna taarifa anafanya kazi wapi ila si
mtumishi wa serikali na hajasajiliwa kama daktari, alisema Pinda.
Dk. Ulimboka anena
Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka,
alisema hakuna sheria ya kumfukuza mfanyakazi asiyeenda kazini kwa siku moja na
hivyo kuwataka madaktari waendelee kukaa nyumbani.
Alisema leo wanafanya taratibu za kisheria ili kesho wakutane kuzungumzia
mgomo huo ambao sasa serikali inaonekana kutaka kutumia nguuvu
kuwasambaratisha.
Alibainisha kuwa sababu ya wao kushindwa kwenda kukutana na Waziri Mkuu jana
ni kuchelewa kupata barua ya wito wa kuitwa kwenye mkutano.
“Sisi tulipata barua saa 11 jioni na tukaandika barua kumjibu Pinda kuwa
hawawezi kukutana leo kwa kuwa wenzao wengine wameshatawanyika, pia tulifanya
hivyo kwa kuwa jana tulitarajia wenzetu kutoka mikoani wangewasili Dar es
Saalam.”
Kuhusu kutohitimu mafunzo ya udaktari, alisema huo ni uongo kwa kuwa
alimaliza mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Muhimbili na kutunukiwa cheti
chake cha udaktari mwaka 2007.
No comments:
Post a Comment