SIKU mbili baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Regia Mtema (Chadema) kuzikwa, Mbunge
wa Arumeru Mashariki, Jeremiah Sumari (CCM) amefariki dunia baada ya kuugua kwa
muda mrefu.
Baadhi ya viongozi akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Spika wa
Bunge, Anne Makinda na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa jana walikwenda
nyumbani kwa marehemu Mbezi Beach kutoa salamu za pole kwa ndugu na jamaa wa
mbunge huyo.
Akitoa taarifa za msiba huo kwa waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema mbunge huyo aliyewahi
kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, alifariki juzi saa nane usiku katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alilazwa.
Alisema kutokana na
msiba huo, ratiba ya vikao vya kamati za Bunge kwa siku ya jana ilivurugika
ingawa kamati nyingine ziliendelea na shughuli kama kawaida.
“Hata
hivyo, tutaendelea na kamati kesho (leo) kama kawaida hadi siku rasmi ya ibada
na kumuaga marehemu,” alisema Dk. Kashililah.
Kwa mujibu wa mtoto wa
kwanza wa Sumari, Sioi Sumari, ratiba ya msiba huo inaonyesha kuwa mbunge huyo,
atazikwa rasmi nyumbani kwao Arumeru Mashariki siku ya Jumatatu na ataagwa
jijini Dar es Salaam kesho na kusafirishwa kwenda Arumeru kesho kutwa.
Ingawa mtoto huyo alikataa kutaja ugonjwa uliokuwa ukimsumbua baba yake
na kuwataka waandishi wa habari kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupata
taarifa hiyo, taarifa za Bunge baadae zilithibitisha kuwa alikuwa akisumbuliwa
na ugonjwa wa saratani ya ubongo.
Taarifa hizo zilieleza kuwa mwili
Sumari utaagwa kesho katika viwanja vya Karimjee kuanzia saa 5 asubuhi na baada
ya hapo atasafirishwa Jumapili asubihi kwenda kijijini kwao Akeri, Meru, mkoani
Arusha kwa maziko yatakayofanyika Jumatatu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,
Sumari alikuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa huo mwaka juzi alipelekwa
nchini India kwa upasuaji na alirejea nchini na hali yake ilikuwa ikiendelea
vizuri.
Hata hivyo mwishoni mwaka jana hali yake ilibadilika ghafla na
kuanza kuwa mbaya na kurejeshwa nchini Januari, 9 mwaka huu na kulazwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.
Kutokana na msiba huo, shughuli za kamati za Jumamosi na Jumatatu
zimesitishwa na zitaendelea tena Jumanne baada ya maziko.
Naibu Spika
Job Ndugai kwa upande wake alisema ofisi ya Bunge imepokea kwa mshtuko taarifa
za msiba huo ambao umetokea siku chache baada ya mbunge Regia kufariki kwa ajali
ya gari hali ambayo alisema ni pigo kubwa kwa Watanzania.
“Kwa kuwa ni
siku chache tu tangu utokee msiba wa Mheshimiwa Regia kila kitu kitakuwa kama
ilivyofanyika katika msiba ule, hivyo kuna uwezekano mkubwa Sumari akaagiwa
Karimjee,” alisema.
Alisema Kamati ya Bunge ya Uongozi inatarajiwa
kukutana leo kupanga ratiba rasmi ya kuaga, ibada na mazishi ya Mbunge Sumari.
Wakizungumzia marehemu, Lowassa alisema amesikitishwa na kifo cha
kiongozi huyo kwani pamoja na kwamba alikuwa mkwe wake lakini alikuwa ni rafiki
yake mkubwa aliyetoa mchango wake kwa watu wa Arumeru.
“Wananchi wa
Arumeru watamkumbuka kwa uchapakazi wake na uadilifu wake, kwa kweli Mkoa wa
Arusha umepoteza kiongozi imara,” alisema.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa alisema marehemu alikuwa mtu
anayependa ukweli na kufanyakazi kwa juhudi kubwa hata kama akiwa mgonjwa.
Alisema pamoja na hayo alikuwa akimpenda Mungu na ndiyo maana alikuwa
mzee wa Kanisa.
“Pamoja na usomi wake alijishusha, alipenda kusali na
alimpenda Mungu, tunamshukuru Mungu kwa kuwa Sumari amekufa katika mazingira ya
kumtegemea na kumuamini Mungu,” alisema.
Marehemu aliyezaliwa mwaka
1943, ameacha mjane mmoja, watoto wanne; wakike mmoja na wa kiume watatu na
wajukuu saba.
Kutokana na msiba huo, Rais Kikwete amemtumia salamu za
rambirambi Spika wa Makinda kutokana na kifo cha Sumari.
“Nimeshtushwa,
nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Sumari,
alikuwa kiongozi aliyewatumikia vema wananchi wa Arumeru Mashariki na Taifa kwa
ujumla katika wadhifa wake wa Waziri kwa umahiri na uhodari mkubwa,” alisema
Rais Kikwete katika salamu zake.
Kutokana na msiba huo, wananchi wa
Arumeru Mashariki wamepoteza kiongozi wa kutegemewa huku Taifa likiachwa na
pengo kubwa ambalo si rahisi kuzibika ikizingatiwa kwamba alikuwa kiongozi
katika Wizara ambayo ni mhimili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
“Kwa
dhati ya moyo wangu, natuma salamu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya
Marehemu Sumari kwa kumpoteza kiongozi na mhimili madhubuti wa familia.
“Ninawahakikishia kwamba nipo pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu
mkubwa, na namuomba Mungu, mwingi wa Rehema aipumzishe roho ya Marehemu Sumari
mahali pema peponi, amina,” alisema Rais Kikwete.
Ameiomba familia ya
Marehemu Sumari kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu
cha maombolezo ya mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake
Mola.
No comments:
Post a Comment