Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema
Aziza Masoud na Ellen Manyangu
WIKI moja tangu kifo cha aliyekuwa Mbunge wa
Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema kilipotokea, mchakato wa kumtafuta mrithi wa
nafasi yake umeanza.
Regia alifariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ajali
ya gari katika eneo la Ruvu mkoani Pwani na kuzikwa Jumatano wiki hii nyumbani
kwao Ifakara, mkoani Morogoro.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana
zinasema tayari maofisa husika ndani ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wameanza
kushughulikia suala hilo la kuziba nafasi ya mbunge huyo kijana ambaye pia
alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC,
Julius Mallaba alisema jana kwamba ofisi yake itatumia orodha ya majina
yaliyopendekezwa na Chadema mwishoni mwa mwaka juzi.
“Nadhani tunayo
orodha ya mapendekezo ya Chadema, basi kwa jinsi taratibu zilivyo, tutarejea
katika orodha hiyo na pale tulipopitisha msitari ndipo tutakapoanzia, lakini
lazima huyo anayefuata katika orodha awe na sifa za kuwa mbunge,” alisema
Mallaba kupitia simu yake ya kiganjani.
Hata hivyo, Mallaba alisema hivi
sasa ni mapema mno kufahamu ni lini uteuzi huo utafanyika na kwamba taratibu za
ndani zikikamilika, mamlaka husika zitaarifiwa ili umma pia uweze
kufahamu.
Awali, Mallaba alikataa kuonana na waandishi wa habari na mmoja
wa maofisa wa Tume hiyo alisema: “Amesema majina yametoka hukohuko Chadema ndipo
yakaja huku kwa hiyo kama mnayahitaji mnapaswa kwenda katika ofisi za Chadema
ili muweze kupata majina hayo.”
Dk Slaa, Zitto wanena
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema chama chake hakifahamu
atakayechukua nafasi hiyo na kwamba hiyo inatokana na ukweli kwamba jukumu hilo
liko mikononi mwa NEC.
“Majina ya wagombea wa viti maalumu yapo NEC na
wao ndiyo wanaoangalia kuchagua nani anayefuata katika orodha iliyopo Tume, kwa
utaratibu, mgombea anayefuata ndiye atakayechukua nafasi hiyo,” alisema Dk
Slaa.
Alisema Chadema kilipeleka NEC orodha ya majina 28 ya wabunge wa
viti maalumu, Desemba 30, 2010 na kati ya hayo majina 25 tayari wameshachaguliwa
ni jukumu la NEC kuangalia jina gani linalofuata kwenye orodha hiyo
iliyopo.
Alisema kati ya hayo majina matatu yaliyobaki yeyote atakuwa na
uwezo wa kuchukua nafasi hiyo kulingana na vigezo vya NEC na kulingana na
utaratibu na Katiba ya Chadema.
“Sina mamlaka ya kujua nani anayefuata
na ofisini kwangu hata majina sina majina yapo NEC mimi nawategemea wao
waniletee jina kwa mujibu wa taratibu zao nitaliangalia kama muhusika bado ni
mwanachama hai nitawajibu na nitawarudishia na ndiyo watalitangaza kwa
wananchi,” alisema Dk Slaa.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi,
jina watakalopewa kama muhusika atakuwa amefukuzwa katika chama, basi jina
litakalofuata baada ya huyo mwanachama ndilo litakaloandikwa na kufanyiwa
kazi.
Alisema si rahisi kwa NEC kumtangaza mrithi wa nafasi hiyo bila
kuwasiliana kwanza na chama na kuthibitisha kuwa bado ana sifa za kushika nafasi
hiyo.
Alisema NEC inajua wazi kuwa haiwezi kumtangaza mtu moja kwa moja
pasipo baraka za chama kwa sababu siku hizi kumekuwa na wimbi la migogoro ndani
ya vyama vya siasa nchini na wengine kujivua uanachama au
kufukuzwa.
Wakati Dk Slaa akisema jukumu hilo ni la NEC, Naibu Katibu
wake, Zitto Kabwe alitaja jina la mmoja wa madiwani wa viti maalumu wa chama
hicho kuwa ndiye anayefuata katika orodha iliyopelekwa NEC.
Akizungumza
jana, Zito alisema kwa mujibu wa orodha yao ya viti maalumu anayefuata baada ya
wabunge walioteuliwa mwaka juzi ni diwani huyo ambaye jina lake tunalihifadhi
kwa sasa.
“Kwa mujibu wa orodha tuliyonayo ya wabunge wa viti maalumu
anayefuata baada ya Regia ni diwani kutoka (anataja wilaya na jina lake), ndiye
atakayechukua nafasi ya kiti hicho kilichoachwa na marehemu,” alisema
Zitto.
No comments:
Post a Comment