MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi amekerwa na mgomo wa madaktari na
kuwataka viongozi wa madhehebu ya dini kusaidia kabla maafa makubwa kutokea.
Dk. Nchimbi alisema hayo juzi wakati wa mahafali ya 16 ya wanafunzi wa
kidato cha sita katika
Shule ya Sekondari ya Jamhuri mjini Dodoma. Katika
mahafali hayo, wanafunzi 354 walitunukiwa vyeti, wakiwemo wavulana 266 na
wasichana 88.
Aliwataka viongozi wa madhehebu ya dini kwenda kwenye
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
kuzungumza na madaktari kwani wanaofanya mgomo
nao wana dini pia ni waumini wao.
“Muende Hospitali ya Mkoa wale
madaktari ni waumini wenu, waulizeni hatua waliyoichukua inaendana na mahubiri
wanayopata?” alihoji. Alisema hatua hiyo hailingani na maadili ya
kimungu
kwa kuwa wagonjwa wanaotakiwa kutibiwa hasa wajawazito pia wanahitaji sana
msaada wao.
“Hili si suala la kisiasa na linahitaji mikakati kulimaliza,
wakumbusheni haya wanayofanya duniani watakutana nayo siku ya hukumu,” alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa ametuma salamu kwa Mbunge wa Dodoma Mjini na kumtaka atembelee
shule hiyo kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge ili aone anaweza kujenga darasa
lipi kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu wa madarasa.
“Nakutuma
Katibu wa Mbunge, tungependa Mbunge aje atembelee shule hii kabla ya kuanza kwa
vikao vya Bunge ili aone ni darasa lipi anaweza kujenga,” alisema. Alisema
kumekuwa na taarifa zisizo sahihi kuwa taasisi za dini hazitoi fursa sawa kwa
wanawake lakini ukweli ni kuwa taasisi hizo zinatambua na kutoa fursa kwa
wanawake.
Dk. Nchimbi alisema kuwa taasisi za dini zimekuwa zikitoa
mchango mkubwa kwa Serikali na
Taifa na kuonyesha upendo mkubwa ambao
thamani yake haiwezi kupimika.
No comments:
Post a Comment