KIGOGO AMWAGA MAMILIONI, ATUMA MAKADA MIKOANI KUMNYOSHEA
NJIA
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikionya
wanachama wake kuacha ndoto za urais wa mwaka 2015, kauli hiyo sasa imeonekana
kupuuzwa na kugeuka kichocheo cha kuongeza kasi ya kujipanga kwa baadhi ya
makada wenye nia ya kusaka nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa taifa.Hivi karibuni
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alionya
kwamba chama hicho hakiko tayari kuendelea kuwakumbatia wanachama wake wanaunda
makundi ndani ya chama, kwa lengo la kusaka umaarufu wa kisiasa kuelekea
Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari
uliofanyika jijini Dar es Salaam, Nape alisisitiza kuwa endapo mwanachama yeyote
atabainika kuvuruga mshikamano ndani ya chama kutokana na kigezo hicho, CCM
haitasita kuchukua hatua kali dhidi yake.
Pamoja na CCM kutoa onyo hilo
kali, mbio za urais wa mwaka 2015 ndani ya chama hicho, zimeelezwa kuingia
katika sura mpya baada ya mmoja wa makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo,
kufanya kikao kizito jijini Arusha, kwa lengo la kuweka mikakati ya kujipanga na
kuimarisha kambi yake.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi
ya wana CCM mjini Arusha, zinaeleza kuwa, kigogo huyo alifanya kikao chake wiki
chache zilizopita katika moja ya majengo ya mfanyabiashara mmoja kutoka Kanda ya
Ziwa, yaliyopo nje kidogo ya jiji.
Kikao hicho kilichohudhuriwa na baadhi
ya viongozi wa CCM kutoka mikoa mbalimbali nchini, wakiwamo baadhi ya wenyeviti
wa mikoa wa chama hicho na baadhi ya viongozi wa Serikali, pamoja na mambo
mengine, kilifanya tathmini ya kina kujua maeneo ambayo mgombea huyo
hakubaliki.
Chanzo chetu kilidokeza kwamba tathmini hiyo ilionyesha kuwa
kada huyo hakubaliki sana katika mikoa ya Lindi , Mtwara pamoja na maeneo ya
mikoa ya Kanda ya Ziwa, ukiwemo Mkoa wa Mara.
Kutokana na hali hiyo,
ilikubaliwa kuwa fedha nyingi zitumike na watu mahiri wenye ushawishi, watumwe
katika maeneo haya ili kuwalainisha baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanaonekana
kuwa mbali na mgombea huyo, na jambo hilo lifanyike haraka kabla ya kuanza kwa
chaguzi mbalimbali ndani ya CCM mwaka huu.
Kauli ya Nape
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipoliuzwa kuhusiana na kikao hicho,
alisema hana taarifa zozote lakini alionya kuwa endapo itathibitika kuwa kuna
makada wa chama hicho wanafanya ‘rafu’ hizo, watachukuliwa hatua za kisheria za
chama kwani huu si muda wa kufanya kampeni za urais.
Aliwataka wanachama
wa CCM kuipa nafasi Serikali yao kutekeleza majukumu yake na ilani kwa ajili ya
maendeleo ya Watanzania.Awali, pia Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, aliwahi
kukaririwa akisema kuwa wanaotarajia kutumia fedha kupata urais kupitia chama
hicho wanajidaganya, ni bora watafute kazi nyingine za
kufanya.
Kikao cha mkakati
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao
hicho, zililidokeza Mwananchi Jumapili kuwa makada watakaotumwa kuzunguka
mikoani, baada kukamilisha kazi yao, watatakiwa kurejesha ripoti itakayofanyiwa
kazi, ili kundi hilo liweke mikakati zaidi ya kufanikisha lengo
lake.
Inaelezwa kuwa hofu kuu ya kundi hilo, ni kutoka kwa baadhi ya
makada wengine wa CCM, wanaotajwa kuonyesha nia ya kuwania nafasi ya urais,
kukubalika zaidi ndani ya chama katika mikoa hiyo, ambapo baadhi yao wanatoka
huko.
Chanzo chetu kilidokeza pia kuwa mbali ya kuweka mikakati hiyo kabambe
ya kuwania urais, pia wajumbe wa kikao hicho ‘kizito’, walifanyiwa sherehe kubwa
ambapo nyama na vinywaji mbalimbali vilimwagwa kwa wingi, ndani ya majengo ya
mfanyabiashara huyo, ambayo yamezungushiwa ukuta mrefu.
“Aisee! kikao
kilikuwa kizito mno mikakati mizito imewekwa , jamaa yuko serious (makini)
kuutaka urais, “alidokeza kada mmoja aliyekuwa ndani ya kikao hicho kwa sharti
la kutoandikwa jina gazetini.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa
tayari, makada waliotumwa kwenda mikoani ‘kumnyoshea njia’ mgombea huyo wa
urais, hivi sasa wanavinjari kwenye maeneo hayo, wakiwa na fedha za kutosha na
vitendea kazi vingine, yakiwemo magari ya uhakika.
Waliotumwa kufanya
kazi hiyo, ni wenyeviti wa baadhi ya mikoa ambao imeelezwa kuwa watatumia
nafasi zao kufanya ushawishi huo kwa urahisi.
Ingawa hadi sasa hakuna
kada ndani ya CCM ambaye ametangaza hadharani kutaka kuwania urais, inadaiwa
kwamba kuna kundi kubwa la watu ambao tayari wanapigana vikumbo chini chini
kutaka nafasi hiyo, kutokana na Rais wa sasa Jakaya Kikwete, kufikia ukomo wake
kikatiba mwaka 2015.
Hatua hiyo imedaiwa kuibua makundi yanayosabisha
nyufa zinazoweza kuleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho.
Tayari CCM
kimekiri kupitia Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama kuwa harakati za kuwania urais
ndani ya chama hicho, zinakivuruga.
Taarifa ya Kamati Kuu ya CCM
iliyosomwa ndani ya Kikao cha Halmashuari Kuu (NEC) ya CCM mjini Dodoma Novemba
mwaka jana ,pamoja na mambo mengine, ilikiri kuwa mbio za kuwania urais mwaka
2015 ndani ya chama hicho, ndicho kiini kikuu cha mgawanyiko.
Kamati Kuu
ilionya kuwa wanaotaka kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho, wanapaswa
kudhibitiwa na kwamba matumizi ya fedha katika kampeni
hayatakubalika.
Ushauri wa Kinana
Alhamisi wiki hii, Mjumbe wa Kamati
Kuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa na gazeti la Mwananchi akieleza kuwa
vigogo wa chama hicho walioanza kampeni za urais, sasa wanavuruga utendaji wa
Serikali ya Rais Kikwete.
Akiwa kwenye ziara ya kutembelea matawi ya CCM Mkoa
wa Dar es Salaam, Kinana alisema vigogo hao ni wabinafsi, wanaivuruga nchi na
hawana lolote wanalolifanya kwa maslahi ya chama hicho tawala.
Kinana
ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kampeni za Rais Jakaya Kikwete wakati akigombea
urais kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alionesha kukerwa na watu hao
na kueleza kuwa si sahihi kuanza kuzungumza masuala ya urais sasa wakati Rais
Kikwete bado ana miaka minne ya kutekeleza Ilani ya chama hicho.
“Sasa
hivi Rais Kikwete ana miaka mingine minne mbele kabla ya kumaliza uongozi wake
na CCM ina kero nyingi za kushughulikia ili kutekeleza ilani yake, halafu
wengine wanazungumzia urais sasa,” alikaririwa akisema Kinana.
Alisema
anasikitishwa na hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wanaoanza kupiga kampeni za
urais ni watu wazito ndani ya nchi na ni wajumbe wa vikao vikuu ndani ya
CCM.
Tishio lingine
Mbali ya chama hicho kukabiliwa na tishio la
mgawanyiko kutokana na urais wa 2015, pia kinakabiliwa na kazi ngumu ya
utekelezaji wa mkakati wake, kuwavua gamba baadhi ya makada wake wanaohusishwa
na kashfa za ufisadi.
Kikao kilichopita cha NEC ambacho kilitarajiwa
kuchukua maamuzi magumu ya kuwavua gamba wanachama hao, kilishindwa kufanya
hivyo, badala yake kikatoa muda kwa wanachama hao kujitathmini wenyewe na
kuchukua uamuzi kabla ya CCM kuwachukulia hatua.
No comments:
Post a Comment