Rais Jakaya Kikwete akimsikiliza katibu Mkuu wa CHADEMA Dk Willbrod Slaa
(kushoto) usiku wa kuamikia jana Ikulu jijini Dar es salaam, ikiwa ni sehemu ya
mazungumzo ya mchakato wa Katiba. Katikati ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman
Mbowe. Picha na Ikulu
NI KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA JUZI,
KAMATI KUU YAJIFUNGIA KUJADILI, NCCR- MAGAUZU WATOA TAKMO LAO
Fidelis Butahe MKUTANO kati ya Rais Jakaya Kikwete na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliofanyika juzi Ikulu, Dar es Salaam
ulichukua saa nane kutokana na uzito wa hoja zilizokuwa zimetolewa na pande zote
mbili.
Novemba mwaka jana, Chadema ilikutana na Rais Kikwete kwa mara ya
kwanza Ikulu na kumkabidhi kabrasha lililokuwa na mapendekezo mbalimbali kuhusu
mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambayo pamoja na mengine, kilitaka mchakato huo
urejeshwe upya bungeni na kumtaka mkuu huyo wa nchi asitie saini Muswada wa
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulipitishwa na Bunge. Hata hivyo, siku moja
baada ya mazungumzo hayo, Rais alitia saini muswada huo na kuwa
sheria.
Vyanzo vya habari kutoka Ikulu, vililiambia gazeti hili jana
kwamba Chadema ilipewa ratiba hiyo kuanzia saa 10:30 hadi saa 5:45 usiku ili
kutoa wigo mpana wa majadiliano hayo yenye nia ya kupata Katiba kwa njia za
amani na umoja.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, katika chumba cha mazungumzo
kulitawaliwa na majadiliano ya kina ambayo wakati mwingine, yaliambatana na
utani wa hapa na pale kwa mfano, Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbrod Slaa
alimwambia Rais: “Watu wanasema nakukwepa Rais.”
Ilielezwa kwamba katika mazungumzo hayo, wajumbe wa pande zote mbili
walijadili kwa uhuru mkubwa na mkuu huyo wa nchi namna ya kupata Katiba bora
bila mikwaruzano.
“Mazungumzo yalikuwa ni mazuri tu, pande zote mbili
zilizungumza na kutoa hoja zake, kulikuwa na utani wa hapa na pale. Yale ambayo
yalionekana kuwa magumu kidogo kila upande uliomba kuyachukua na kwenda
kuyafanyia kazi zaidi kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho.”
Novemba 28
mwaka jana, Rais Kikwete alisaini muswada huo na kukamilisha safari ya kutungwa
kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa
limeupitisha.
Tangu wakati huo Rais Kikwete amekuwa akitutana, kusikiliza
na kuchukua maoni na mawazo ya wadau mbalimbali kutoka vyama vya siasa, asasi za
kijamii na makundi mengine ya kijamii kuelekea mchakato wa kupata Katiba
Mpya.
Mchakato huo umekuwa ukipingwa na kwa hoja mbalimbali zikiwamo za
kuundwa kwa tume ya kuratibu mchakato huo, hadidu za rejea, mamlaka ya uundaji
wa tume na uteuzi wa wajumbe na wapi tume itapaswa
kuwajibika.
Kauli ya Ikulu Taarifa iliyotolewa jana
na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na kusainiwa na Mwandishi wa Habari Msaidizi
wa Rais, Premi Kibanga ilisema Rais Kikwete alisema licha ya nchi kuwa na Katiba
ambayo imelilea vizuri taifa, inahitajika Katiba mpya inayokwenda na
wakati.
Alisema baada ya kumalizika kwa kikao na viongozi wa NCCR-Mageuzi, Rais
Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chadema, ikiwa ni
mwendelezo wa mazungumzo yao yaliyoanza mwishoni mwa Novemba, 2011 kuhusu
Katiba Mpya.
“Katika mazungumzo haya na vyama vya siasa, Rais
amesisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kuwa hatimaye Watanzania wote
watakiri kuwa Katiba Mpya ni yao wote na hatimaye ifikapo mwaka 2015 nchi iweze
kufanya uchaguzi wake na Katiba Mpya,” alisema Kibanga.
Chadema
wajifungia Dar Kwa upande wa Chadema, jana Kamati Kuu (CC) chini ya
Mwenyekiti wake Freeman Mbowe ilikuwa katika Hoteli ya Protea Dar es Salaam
kujadili mkutano huo na Rais, Ikulu juzi.
Katika kikao hicho, Kamati
Maalumu ya Chadema kuhusu mchakato huo wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya
mwaka 2011, iliwasilisha taarifa yake.
Taarifa ya chama hicho,
iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika ilisema
uamuzi wa CC kuhusu mkutano na Rais Kikwete utatolewa baada ya kikao hicho
kumalizika.
Akizungumzia mkutano wa Ikulu, Mnyika alisema kamati hiyo
maalumu ya Chadema iliyokutana na Rais Kikwete ikiongozwa na Mbowe, ilitaarifiwa
hatua ambayo imefikiwa na Serikali katika kuanza kuiboresha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ya mwaka 2011, ili ikidhi mahitaji ya kuaminiana na muafaka wa kitaifa
kwa mawasiliano na ushauri wa wadau mbalimbali.
Kauli ya
NCCR-Mageuzi NCCR-Mageuzi kwa upande wake, kilitoa taarifa kwa
vyombo vya habari kikidai kwamba Rais Kikwete amekubali kuifanyia marekebisho
sheria hiyo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye aliongoza na
ujumbe wa watu sita kwenda Ikulu Dar es Salaam juzi, alisema jana kwamba baada
ya kuwasilisha ajenda zao mbili kuhusu katiba na umeme, waliambiwa sheria hiyo
itafanyiwa marekebisho katika kikao kijacho cha Bunge.
Mbatia aliwaambia
waandishi wa habari kwamba pamoja na sheria hiyo kurudishwa bungeni, pia
walimwomba Rais Kikwete aifanyie marekebisho Ibara ya 98 ya Katiba ya sasa kwa
kuwa inachangia kukwamisha mabadiliko ya Katiba.
“Lengo la kuanzishwa kwa
NCCR-Mageuzi ni Watanzania kuwa na Katiba yao na hata Rais wa Awamu ya Tatu
(Benjamin Mkapa), tuliwahi kumweleza kwamba Katiba ni ya kudumu na lazima iundwe
kwa maslahi ya wananchi na ndicho tulichomweleza Rais Kikwete,” alisema
Mbatia.
Alisema tangu wakati huo nchi imekuwa na katiba yenye mfumo wa
chama kimoja, licha ya kuwa ilipitishwa sheria ya kuwa na vyama
vingi.
Mbatia alisisitiza kwamba, katika msafara wa chama hicho Ikulu,
Mkuu wa Idara ya Katiba na Sheria wa chama hicho, Dk Sengondo Mvungi alitumia
zaidi ya saa moja kumfafanulia Rais Kikwete na timu yake jinsi mchakato wa
kuandika Katiba Mpya unavyotakiwa kuwa.
Alisema walimweleza Rais Kikwete
kwamba suala la Katiba ni la kisiasa, hivyo si vyema Tume itakayoundwa ikaachwa
chini ya uangalizi wa wanasheria pekee.
“Katika tume hii wanatakiwa
kutumiwa wataalamu mbalimbali hata kama watakuwa wanasiasa… kinachotakiwa ni
kuangalia uwezo wao,” alisema Mbatia.
Katika kikao hicho cha Rais na
NCCR-Mageuzi, viongozi wa Serikali waliokuwapo ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi na ujumbe wa chama hicho uliwajumuisha pia Makamu
Mwenyekiti wake, Zanzibar, Ambary Hamisi, Naibu Katibu Mkuu George Kahangwa,
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali, Mweka Hazina Taifa, Mariam Mwakingwe, na
Mbunge wa Kasulu Vijijini, Zaituni Buyogela.
|
No comments:
Post a Comment