RAIA wa Nigeria mwenye miaka 34 amekamatwa na polisi wa Uwanja wa Ndege Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere akiwa na dawa za kulevya tayari
kuelekea nchini Nairobi.
Kukamatwa kwa Mnigeria huyo kumekuja siku
chache baada ya polisi kukamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya zipatazo kilo
210 mkoani Lindi, ambazo zilikuwa tayari kusafirishwa kwenda jijini Dar es
Salaam zikivunja rekodi tangu kuanzishwa kwa Kitengo cha Dawa za
Kulevya.
Juzi, Polisi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius
Nyerere walimkamata Mnigeria huyo jambo ambalo lilithibitishwa na Kamanda wa
Polisi wa Viwanja vya Ndege nchini, Ulrich Matei akisema lilitokea saa 10:20
alfajiri.
Matei alisema kutokana na kuimarishwa kwa shughuli za upekuzi
uwanjani hapo, waliweza kumbaini raia huyo akiwa na pipi 14 za dawa za kulevya
ambazo zinaendelea kuchunguzwa kujua ni za aina gani.
Alifafanua kwamba,
mtuhumiwa huyo mwenye hati ya kusafiria namba A02425579 iliyotolewa Nigeria
mwaka 2010, alikuwa akijiandaa kuondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya
(KQ).
Kamanda Matei aliongeza, baada ya kupekuliwa raia huyo alikutwa na
kiasi hicho ambacho alikificha kwenye fulana na kuongeza kwamba alikuwa
akisafiri na ndege hiyo kwenda Kenya kisha Lagos, Nigeria.
"Hapa
uwanjani tunajitahidi kwa uwezo wetu wote kuhakikisha uwanja wetu hauwi njia ya
wahalifu. Hatuwezi kuruhusu watu wachafue taswira nzuri ya nchi yetu. Sasa
tulivyompekua, tulimkuta akiwa na kiasi hicho cha pipi akiwa amezifunga kwenye
fulana.
Alikuwa anasafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya yenye
namba KQ481 akielekea Nairobi kisha Lagos, Nigeria," alifafanua Kamanda Matei.
Hata hivyo, Matei alisema raia huyo bado alikuwa akishukiwa kuwa na
dawa nyingine alizomeza tumboni lakini hadi jana hakuwa ameweza kutoa nyingine
na alikabidhiwa kwenye kikosi cha Kudhibiti za Dawa za Kulevya kwa taratibu
zaidi za kisheria.
"Tulimshuku alikuwa amemeza dawa tumboni lakini hadi
jana asubuhi hakuwa ameweza kutoa. Tulichofanya sisi Polisi wa Uwanja wa ndege
ni kumkabidhi Kitengo cha Dawa za Kulevya ili waweze kuendelea na taratibu
nyingine ikiwa ni pamoja na kumpiga X-ray na vipimo vingine kubaini aina ya dawa
hizo alizokamatwa nazo kwani zinahitaji vipimo," alifafanua kamanda
Matei.
Alisema licha ya kumshikilia kwa siku nzima ya juzi raia huyo
ambaye alikamatwa Terminal Two, hakuweza kutoa dawa nyingine zaidi na kwamba
taratibu nyingine za kisheria zitaandaliwa.
No comments:
Post a Comment