KANISA la Kiinjili na Kilutheli Tanzania (KKKT), linalotarajia kuanzisha
Dayosisi mpya ya Shinyanga na Simiyu limefanikiwa kukusanya Sh milioni 116
taslimu ambapo kati ya hizo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na familia
yake walichangia Sh milioni 21.
Katika harambee hiyo, Mchungaji wa KKKT,
Philbert Celestine alimshukuru Lowassa na familia yake pamoja na wageni waalikwa
kwa kufanikisha mchango huo ambao ulivuka lengo.
Awali, harambee hiyo
ilikuwa na lengo la kupata Sh milioni 114 ili kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo
lakini walifanikiwa kuvuka lengo na kupata Sh milioni 204, kati ya hizo fedha
tasilimu zikiwa ni Sh milioni 116.
Akisoma risala kwa niaba ya KKKT
Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Mchungaji Celestine alisema kuwa kanisa
hilo jipya likimalizika na kuifikia malengo waliyojiwekea,
litasaidia katika
kukuza ufahamu wa kiroho baina ya waumini wa dayosisi hiyo mpya ambayo
inatarajia kufunguliwa mapema mwaka 2013.
Alisema lengo lao ni kuwafikia
na kupanua huduma ya neno la Mungu kwa kuwajenga waumini hao hasa ukizingatia
Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa
ngozi (albino).
Kwa upande wake, Lowassa akizungumza waumini hao,
alisema kuwa suala la ujenzi wa makanisa nchini ni zuri na ni vema kwa sasa
kutokuwategemea wafadhili kama ilivyokuwa awali na badala yake tubadilike kwa
kujenga sisi wenyewe.
“Zamani tulikuwa tumezoea kujenga makanisa kwa
kuwategemea wafadhili mbalimbali kutoka nje ya nchi hasa wazungu, lakini kwa
sasa tubadilike tujenge wenyewe kwani uwezo tunao wa kuchangishana,” alisema
Lowassa.
Lowassa alisisitiza kuwa yeye yupo tayari kurudi akiitwa katika
harakati zozote za kuchangia ujenzi wa nyumba za ibada. Askofu wa Dayosisi ya
Mashariki ya Ziwa Victoria, Andrea Gule akitoa shukrani zake katika harambee
hiyo, aliwataka wananchi na waumini kwa ujumla kuwa na moyo wa kuthubutu katika
kuchangia ujenzi hasa wa nyumba za ibada ili kuwakomboa
watu kiroho.
No comments:
Post a Comment