RIPOTI ya ugonjwa unaomsumbua Naibu
Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, imeendelea kuivuruga serikali, safari
hii Wizara ya Mambo ya Ndani ikisisitiza kuwa Wizara ya Afya ndiyo inayopaswa
kuzungumzia suala hilo.
Kauli hii mpya toka Wizara ya Mambo
ya Ndani imekuja ikiwa ni takriban wiki moja tangu gazeti hilt lilipomuuliza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, kuhusiana na
ripoti hiyo na kusema kuwa suala hilo haliwahusu.
Uamuzi wa Tanzania Daima Jumatano
kutaka kupata kauli toka Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo kimantiki
inashughulikia madai ya jinai ulikuja baada ya kile kinachodaiwa kuwa ripoti ya
ugonjwa wa waziri huyo kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali maarufu ya
Apollo nchini India ambayo hadi sasa imebaki kuwa siri, inadaiwa kueleza chanzo
cha ugonjwa wa Dk. Mwakyembe kuwa umetokana na sumu kali aliyowekewa hapa
nchini.
Gazeti hili jana lilimtafuta Waziri
wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, kutaka kupata kauli yake juu ya ripoti
hiyo na tuhuma zinazotajwa ambapo alisema mwenye uwezo wa kuzungumzia juu ya
ripoti hiyo ni Mkemia Mkuu wa Serikali toka Wizara ya Afya.
Alipoulizwa na gazeti hili
anazungumziaje juu ya kile kinachodaiwa Dk. Mwakyembe kuwekewa sumu hapa
nchini, Waziri Nahodha alijibu kwa sauti kali kidogo: “Aa..ah, sikiliza; wenye
uwezo huo nimekwambia ni Wizara ya Afya, mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani
kuzungumzia suala hilo ni mpaka niletewe taarifa kama mtu anatuhumiwa kwa
sababu wizara yangu inashughulika na kesi za jinai.
“Sasa sijaletewa taarifa, mimi
ripoti siijui, ripoti za afya za watu ziko Wizara ya Afya… hao si ndiyo
wanawapeleka watu India?…Sijaletewa ripoti sijaiona na sidhani kama nitalewa,”
alisema.
Alipoulizwa kwa nini anasema hadhani
kama ataletewa ripoti hiyo je hakuna taarifa zinazodai kuwa ugonjwa unaomsumbua
Dk. Mwakyembe unatokana na sumu? Bado aliendelea kusisitiza kuwa hajapokea
taarifa zozote za mtu kutuhumiwa kumuwekea sumu Dk. Mwakyembe na kusisitiza
kuwa kama gazeti hili linamfahamu mtuhumiwa huyo basi limtajie.
Hata hivyo ingawa taarifa rasmi ya
serikali haijatolewa, ripoti ya ugonjwa wa waziri huyo kutoka kwa madaktari
bingwa wa hospitali maarufu ya Apollo nchini India ambayo hadi sasa imebaki
kuwa siri inadaiwa kupelekwa serikalini kupitia Wizara ya Afya.
Taarifa za Dk. Mwakyembe kuwekewa
sumu, mara ya kwanza ziliibuliwa rasmi nchini na Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye ni rafiki mkubwa na mshirika wa karibu
wa Dk. Mwakyembe katika mapambano dhidi ya ufisadi nchini katika mahojiano na
kituo cha televisheni cha ITV katika kipindi chake cha dakika 45 kilichorushwa
mwaka jana.
Sitta alisikika akisema kuwa
wasiwasi huo wa Dk. Mwakyembe kuwekewa sumu unatokana na mabadiliko ya ngozi na
nywele alivyoondoka navyo nchini kwenda India.
Kwa Mujibu wa Sitta ambaye ni Mbunge
wa Urambo Mashariki (CCM), alisema alipokwenda kumwona Dk. Mwakyembe nyumbani
kwake, alipata mshtuko mkubwa kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza katika umri
alionao kushuhudia ngozi ya mtu ikitoa unga.
Sitta alikaririwa akisema, “Kuna
kitu kama mba kwenye nywele na kwenye ngozi ya Dk. Mwakyembe. Akishika hivi,
baadhi ya nywele zinadondoka. Mkono umevimba, sehemu mbalimbali. Mke wake
alichukua video. Alikuwa anatuonyesha kwenye laptop (kompyuta ndogo). Kwa kweli
inatisha.”
Hata hivyo, Sitta alihojiwa na
polisi kuhusiana na taarifa hiyo kwa madai kuwa ingeweza kuhatarisha amani,
lakini alipotakiwa kutoa ushahidi anadaiwa kutoa ushahidi wa habari za kwenye
mitandao ya kijamii.
Kabla ya Dk. Mwakyembe kwenda India
kutibiwa, kulikuwa na uvumi kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa kiongozi huyo
kulishwa sumu, ingawa yeye binafsi hajakanusha wala kuthibitisha habari hizo.
Katika mkutano wake wa kwanza na
waandishi wa habari tangu aliporejea nchini, Dk. Mwakyembe alisema ripoti ya
ugonjwa wake iko serikalini.
Hata hivyo, serikali hadi sasa
imekataa kuitoa hadharani ripoti hiyo ya madaktari bingwa wa Hospitali ya
Apollo, India, waliomtibu Dk. Mwakyembe.
Habari zaidi zinasema kuwa
mwanasiasa huyo amepania kuianika ripoti hiyo hadharani kama serikali
itaendelea kuifanya kuwa siri.
Mwakyembe alipelekwa India Oktoba 9
mwaka jana na kurejea nchini Desemba 11 mwaka jana hata hivyo licha ya kupata
matibabu nchini India na kuendelea na tiba hiyo hapa nchini, hali yake bado
siyo ya kuridhisha kwani amenyonyoka nywele, kope, nyuzi na hata vinyweleo
vyote mwilini.
No comments:
Post a Comment