NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, September 11, 2012

Shinikizo za Chadema Tanzania

Ramani ya Tanzania
Chama cha upinzani nchini Tanzania cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kimewataka waziri wa mambo ya ndani pamoja na mkuu wa jeshi la polisi kujiuzulu kufuatia mauaji ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi yaliyotokea wiki moja iliyopita huko mkoani Iringa.
Vilevile uongozi wa chama hicho umemtaka rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya kimahakama itakayochunguza kifo hicho kwa madai kwamba hawana imani na kamati iliyoundwa na waziri wa mambo ya ndani kwa maelezo kuwa haina mamlaka ya kisheria.
                                            Marehemu Daudi Mwangosi enzi za uhai wake

Huku mazingira yaliyopelekea kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi yakiwa bado yamegubikwa na utata, chama cha Demokrasia na maendeleo kimewataka waziri wa mambo ya ndani Emmanuel Nchimbi na mkuu wa jeshi la polisi Said Mwema kuachia ngazi mara moja kama njia ya kuwajibika.
Mwenyekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe, amesema kuwa Chadema haina imani na kamati iliyoundwa na waziri Nchimbi kwa madai kwamba imekosa mamlaka ya kisheria.
Hivyo amemtaka rais Jakaya Kikwete aunde tume ya kimahakama itakayochunguza kifo cha mwandishi huyo na kwamba, iwapo hayo hayatatekelezwa, chama hicho kitafanya maandamano makubwa.
Kwa upande mwengine, waandishi wa habari nchini wamedhamiria kufanya maandamano ya kimya kimya nchi nzima hapo kesho kulaani kuuawa kwa mwandishi mwenzao. Maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika katika mikoa yote kuanzia saa mbili asubuhi. Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, yamepangwa kuanza katika kituo cha runinga cha Chanel Ten na kumalizikia katika viwanja wa mnazi mmoja.
Katibu mkuu wa jukwaa la wahariri nchini Tanzania, Nevil Meena amesema kuwa tukio la kuuawa kwa mwandishi huyo wa habari marehemu Daudi Mwangosi tarehe mbili mwezi huu katika kijiji cha Nyololo huko mkoani Iringa, kumeibua hisia kali miongoni mwa waandishi wa habari pamoja na wanaharakati huku wengi wao wakihoji usalama wa waandishi wanapokuwa kazini hasa katika mazingira magumu.
Mtaniwia radhi kwa picha hii ya kutisha.Hivi ndivyo Mwangosi alivyouwawa Iringa

No comments:

Post a Comment