NJOMBE

NJOMBE

Wednesday, September 12, 2012

Rwanda yahusishwa upya na uasi DRC



Wanachi wakipinga vita Mashariki mwa DRC
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, linasema kuwa lina ushahidi mpya kuonyesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na waasi wa M23 kwa usaidizi wa wanajeshi wa Rwanda.
Shirika hilo linasema limefanya mahojiano na watu 190, walioshuhudua matukio hayo Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Utafiti wa shirika hilo unasema kuwa waasi wa M23 waliwasajili vijana wadogo na wanaume jeshini.
33 kati ya wale waliosajiliwa, wamesemekana kuuawa walipojaribu kutoroka. Baadhi walifungwa kamba na kupigwa risasi , hatua hiyo ikisemekana kuwa mfano wa adhabu itakayotolewa kwa watakaojaribu kutoroka.
Jamii ya kimataifa ilisitisha msaada kwa Rwanda baada ya madai ya jeshi la Rwanda kusaidia waasi hao ingawa baadaye msaada ulianza kutolea tena pale Uingereza iliposema kuwa imeweza kuzungumza na Rwanda kuhusu swala hilo.
Shirika hili linasema liliwahoji familia za waathiriwa wanyarwanda, maafisa wa utawala pamoja na wapiganaji wa zamani wa kundi la M23 kati ya mwezi Mei na Septemba.
Kwa mujibu wa afisaa mkuu wa utafiti,Anneke Van Woudenberg, waasi wa M23 wanafanya visa vya kuogofya vya ukiukwaji wa haki za binadamu, Mashariki mwa Congo.
Moja ya visa walivyodokezewa watafiti wa HRW, ni kile cha mwanamke mwenye umri wa miaka 32 aliyesema kuwa waasi wallivunja mlango wake na kumpiga mtoto wake mwenye umri wa miaka 15 hadi kufariki na kisha kumteka nyara mumewe. Kabla ya kuondoka waasi hao walimbaka kila mmoja kwa zamu, na kisha kumwagia mafuta taa kwenye miguu yake na kuiteketeza. Aliokolewa na jirani zake baada ya waasi hao kuondoka.
HRW imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwachukulia hatua waasi wa M23 huku akipendekeza maafisa wa Rwanda waliohusika na vita hivyo kufunguliwa mashtaka kwa kusaidia waasi hao kukiuka haki za binadamu pamoja na kutoa mafunzo, silaha na zana nzito za vita kwa waasi hao.
Hata hivyo serikali ya Rwanda imekuwa ikikana madai kuwa jeshi lake linahusika na uasi Mashariki mwa DRC.

No comments:

Post a Comment