NJOMBE

NJOMBE

Sunday, September 9, 2012

Wengi wauawa katika mapambano Sudan

Waasi wa Darfur wasema walivitimua vikosi vya serikali
Jeshi la Sudan na waasi wanasema wamekuwa katika mapambao tofauti mara mbili yaliyowaacha watu kadhaa kuuawa.
Jeshi linasema limewaua wapiganaji 32 walioshambulia kijiji magharibi mwa eneo la Darfur wakati waasi nao wakidai kuwa wamevitimua vikosi vya serikali kutoka eneo hilo.
Katika tukio tofauti Khartoum inasema kuwa waasi 45 wameuawa katika kijiji cha eneo la kusini la Kordofan, karibu na mpaka wa kusini wa Sudan.
Waasi wa Vuguvugu la Haki na Usawa (The Justice and Equality Movement-JEM) wamesema wamekiteka kijiji hicho huku wakiua askari mmoja.
Mwaka jana vikundi vya waasi katika majimbo mawili na pia katika jimbo la Blue Nile walianzisha muungano wenye lengo la kuiondoa serikali ya rais Omar al-Bashir.
Khartum inaishutumu Sudan Kusini kuwaunga mkono waasi hao.
Serikali mjini Juba inakanusha shutuma hizo ikiilaumu serikali ya Sudan kuyaunga mkono makundi ya waasi Sudan Kusini.
Mapigano ya hivi sasa yanakuja wakati Marekani ikiwa imetoa onyo kuhusu mgogoro unaoendelea wa mpaka kati ya Sudan na Sudan Kusini.
Onyo hilo lilitolewa na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice kufuatia mkutano wa Baraza la Usalama kujadii mgogoro huo.
Sudan Kusini imekubali pendekezo la suluhu ya mpaka lililotolewa na Umoja wa Afrika, lakini Sudan inakataa pendekezo hilo.
Tarehe ya mwisho ya Agosti 2 ya kufikia muafaka iliyokuwa imewekwa na Umoja wa Mataifa imeshindwa kuzaa matunda.
Hata hivyo pande zote mbili zinashinikizwa kuwa zimefikia makubaliano kabla ya tarehe mpya iliyowekwa ya Septemba 22.
Sudan na Sudan Kusini zimekuwa katika mgogoro kuhusu mpaka kati ya nchi hizo mbili na mapato ya uchimbaji mafuta.
Sudan Kusini ilipata uhuru kutoka Sudan mwaka jana, ikimaliza miaka mingi ya mapigano kati ya eneo la kaskazini linalokaliwa na Waislamu wengi na lile la kusini lenye Wakristo wengi na dini nyingine.

No comments:

Post a Comment