NJOMBE

NJOMBE

Sunday, September 9, 2012

Nigeria yaua wapiganaji wa Boko Haram

Ulinzi eneo la Maiduguri kaskazini mwa Nigeria
Jeshi la Nigeria linasema limewaua watu saba wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa kundi la wapiganaji wa Kiisalmu wenye msimamo mkali la Boko Haram katika mapambano kaskazini mwa nchi hiyo.
Msemaji wa jeshi hilo amesema watu wengine zaidi kumi na watatu wamekamatwa baada ya kushambulia kituo cha ukaguzi cha jeshi, katika mji wa Maiduguri.
Ghasia hizo zimetokea siku moja baada ya polisi wa Nigeria, kusema kuwa wataanza kulinda kutwa-kucha, milingoti ya simu za mkononi kufuatia milingoti kadhaa kama hiyo kushambuliwa mwezi uliopita, kaskazini mwa nchi.
Boko Haram ilisema ilifanya mashambulio hayo, kwa sababu milingoti hiyo inatumiwa kufuatilia mawasilino baina ya wafuasi wake.
Akitoa maelezo ya tukio hilo la Maiduguri, Luteni Kanali Sagir Musa amesema, ''Kundi la watu wenye silaha wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Boko Haram walishambulia kituo cha ukaguzi cha kijeshi sehemu ambayo wanajeshi walikuwa wameweka kizuizi na kufanya ukaguzi.
Ramani ya Nigeria ikionyesha eneo la Maiduguri
''Wanajeshi walijibu shambulio hilo kwa risasi. Watu saba wenye silaha waliuawa katika majibizano hayo ya ufyatulianaji risasi, na wengine kumi na watatu walikamatwa huku wengine wakikimbia. Hakuna majeruhi waliopatikana kwa upande wa wanajeshi.''
Boko Haram wanataka kuwekwa kwa utawala wa sheria ya Kiislamu nchini Nigeria.
Kundi hilo lilianzisha kampeni ya kijeshi mwaka 2009 kupigania kuanzishwa kwa utawala wa Kiislamu, likishambulia majengo ya serikali na makanisa na pia kuwaua wahubiri wa Kiislamu wenye msimamo wa kati.
Nchi hiyo imegawanyika kati ya eno la kaskazini lenye Waislamu wengi na lile la kusini linalokaliwa na Wakristo wengi na dini nyingine.

No comments:

Post a Comment