NJOMBE

NJOMBE

Saturday, September 1, 2012

Chuo cha Metropolitan chapokonywa leseni

Chuo kikuu cha London Metropolitan
Zaidi ya wanafunzi 2,000 kukihama chuo kikuu cha London Metropolitan
Zaidi ya wanafunzi 2,000 nchini Uingereza huenda wakarudishwa nchi zao za asili, baada ya leseni ya chuo kikuu cha London Metropolitan kudhamini na kutoa mafunzo kwa wanafunzi nje ya mataifa ya muungano wa Ulaya wa EU kufutiliwa mbali.
Idara ya serikali inayohusika na kuwazuia wageni wasio halali kuingia Uingereza, UK Border Agency (UKBA), imeelezea kwamba chuo kikuu cha London Metropolitan, kimeshindwa kufuatia suala la ikiwa wanafunzi kweli huwa wanafika darasani au la, na wengi wao hawana hata vibali vya kuwa nchini Uingereza.
Kutokana na hayo, chuo hicho kikuu hakitakuwa tena na mamlaka ya kuidhinisha visa kuwaruhusu wanafunzi kuingia Uingereza.
Chuo hicho kimekanusha madai ya UKBA, na kimeelezea kwamba kisheria kitachukua hatua.
Kamati maalum imeanzishwa ili kuwasaidia wanafunzi ambao wataathiriwa na hatua hiyo, ambayo huenda ikawalazimisha zaidi ya wanafunzi 2,000 kutoka mataifa mbalimbali, kufanya juhudi zaidi katika kutafuta wadhamini wapya, na vile vile vyuo vingine, la sivyo, warudishwe nyumbani.
Serikali imeelezea kwamba ingelipenda kukadiria idadi kamili ya wanafunzi ambao watajiunga na vyuo vingine, kabla ya kuwaamrisha watakaosalia, kuondoka nchini Uingereza chini ya muda wa siku 60.
Hata hivyo, wizara ya mashauri ya ndani ya Uingereza kwa sasa imeelezea kwamba haiwezi kuthibitisha ni lini itatoa tangazo la kuwataka baadhi ya wanafunzi hao kuondoka nchini.
UKBA imeelezea kwamba chuo kikuu cha London Metropolitan kimeshindwa "kuangazia mara kwa mara baadhi ya masharti muhimu" katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Waziri wa uhamiaji Damian Green alisema chuo hicho kimeshindwa kutimiza wajibu wake katika masuala matatu muhimu:
Zaidi ya robo ya wanafunzi 101 waliokaguliwa hawana vibali vya kuishi Uingereza.
Wanafunzi kati ya 20 hadi 50 ambao faili zao zilichunguzwa "hamna ushahidi thabiti" kwamba walikuwa na viwango vya kuridhisha kwa upande wa lugha ya Kiingereza.
Na wanafunzi 142 kati ya 250 (asilimia 57), haikuwezekana kuthibitisha kama walikuwa wakifika darasani au la, na kwa hiyo chuo kikuu hakina utaratibu thabiti wa kutambua kama kweli wanafunzi hao walikuwa wakiendelea vyema na masomo.

No comments:

Post a Comment