NJOMBE

NJOMBE

Sunday, September 2, 2012

Dk. Slaa: Sitta ni Kivumbi, Asema CHADEMA haiwezi kumpa hata uongozi wa kata

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta ni mtu hatari ambaye CHADEMA kimegundua kuwa anaweza kufanya lolote kupata madaraka.
Dk. Slaa alisema Sitta hatakiwi kuaminiwa kwa kuwa hata alipokuwa spika, huku akiwa mwana CCM, mara kadhaa alijaribu kuomba kujiunga na CHADEMA iwapo CCM ingemtosa.
“Huyu mtu haaminiki hata katika dhamira yake, kwa kuwa tulikutana zaidi ya mara 100 na hata tukawa tunaandikiana vimemo, yeye akiwa katika kiti cha spika. Kama anabisha leo akanushe juu ya uhaini wake dhidi ya CCM,” alisisitiza Dk. Slaa.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana mjini Iringa wakati akizungumza na waandishi wa habari, akijibu kauli iliyotolewa na Sitta aliyedai kwamba CHADEMA hakijastahili kupewa madaraka kwa kuwa hakina watu wenye uzoefu wa uongozi.
Sitta alidai mwenye uzoefu wa uongozi ndani ya CHADEMA ni Dk. Slaa pekee; akashutumu Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwamba uzoefu pekee alionao ni kuongoza kumbi za disko.
Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), na ambaye yumo katika fitina za kimakundi ya wanaoutaka urais ndani ya CCM, alisema hayo mjini Karagwe wiki hii, kama njia ya kijikweza mbele ya umma; na kuwashusha viongozi wa CHADEMA, ambacho chini ya uongozi wa Mbowe kimejengeka kuwa chama kikuu cha upinzani kinachotishia kuiondoa CCM madarakani.
Akijibu hoja hiyo, Dk. Slaa alidai kuwa mara kadhaa walizokutana, Sitta akiwa Spika wa Bunge alimweleza kuwa ana kundi la wabunge 55 waliokuwa tayari kuondoka katika CCM, na kwamba wangefanya hivyo siku tatu kabla ya Bunge la mwaka 2010 kumalizika.
Aliongeza kuwa, ukigeugeu wa Sitta, haukuishia baada ya uchaguzi, bali hata wakati wa mchakato wa kumpata spika ambapo baada ya kutoswa na CCM, alihangaika kuwapigia simu viongozi wa CHADEMA akiwaomba wampe nafasi ya kugombea nafasi hiyo kupitia chama chao.
“Alikuwa akinipigia simu saa sita usiku baada ya kutoswa na CCM na kwa bahati mbaya simu yangu ilikuwa ‘silence’, lakini saa 12 asubuhi nikapokea simu ya mke wake, Magreth Sitta akiniambia ‘Dk. baba anataka kuongea na wewe na anakutafuta kuanzia usiku’,” alisema.
Aliongeza kuwa, wakati alipopokea simu ya Sitta, jambo la kwanza aliomba amzuie Mabere Marando kugombea uspika ili agombee yeye na kwamba, angeitisha mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kutangaza kujiondoa CCM kwa kuwa ametoswa kwenye uspika.
Dk. Slaa alisema, katika hali ya kushangaza na inayoonesha kuwa kiongozi huyo ni mtu wa kuogopwa, wakati wakijiandaa kukutana na waandishi wa habari kwa nia ya kutangaza kujiondoa CCM, Sitta alimueleza kuwa amepigiwa simu kutoka kwa wakubwa akiahidiwa kupewa nafasi ya unaibu waziri ambayo hata hivyo, alidai hakubaliani nayo.
Alisema, wakati alipoambiwa hivyo na Sitta kuwa hakubaliani na nafasi ya unaibu waziri, akaanza kupata shaka ya kama anaweza kuwatumikia Watanzania kiuadilifu kwa kuwa alionesha dalili kuwa anachowaza ni nafasi ya juu zaidi badala ya kuwatumikia watu.
Aliongeza kuwa, mwaka 2010 Sitta akiwa na Dk. Harrison Mwakyembe pamoja na Fred Mpendazoe wakiwa ni waanzilishi wa Chama cha CCJ, walikutana na viongozi wa CHADEMA katika ofisi za spika mjini Dodoma na akawaeleza kuwa wanaanzisha chama hicho na ikishindikana watahamia CHADEMA.
Alibainisha kuwa, baada ya kukubaliana na kuiangalia katiba ya CCJ na kubaini kuwa ilikuwa inalingana na ya kwao, wakakubaliana Sitta awe mgombea urais kupitia CHADEMA.
Dk. Slaa alisema, hata hivyo Sitta akawageuka wenzake na akaendelea kubakia CCM.
Alizidi kumshambulia Sitta kuwa ni mtu asiye na uadilifu unaoweza kulingana hata na kiongozi wa ngazi ya kata wa CHADEMA kwa kuwa ndiye aliyekuwa kinara wa kuzuia hoja mbalimbali za ufisadi zilizotolewa na wabunge wa upinzani kwa sababu ya kuilinda Serikali ya CCM.
“Mnakumbuka hoja ya Buzwagi aliyoitoa Zitto kuwa waziri amesema uongo kwa kulidanganya Bunge, yeye akapindua kuwa ni hoja ya Zitto na wakamtoa nje ya Bunge kwa miezi minne, kisha wakamrudisha kinyemela baada ya mwezi mmoja na Sitta alishupalia kuzima hiyo hoja?” alihoji Dk. Slaa.
Alisema, Sitta ndiye spika aliyezuia hoja ya ufisadi wa BoT ya EPA licha ya kujua ukweli wa nyaraka zilizotolewa kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Akizungumzia kauli ya Sitta aliyedai kuwa Mbowe ni muongoza disko, hivyo hafai kuwa kiongozi, Dk. Slaa alisema Sitta kama mwanasheria na waziri aliyepewa fadhila ya kuongoza wizara, anazidi kuiaibisha serikali kwa kuwa mamlaka na leseni ya kuendeshea kumbi za starehe zinatolewa na Serikali ya CCM.
Alisema katika hali ya kawaida, Sitta amewatukana vijana na wapiga kura waliomchagua kwa kuona kitendo cha kuwepo kwa kumbi za disko ni uhalifu.
Dk. Slaa alisema CHADEMA ina utaratibu wa kupata viongozi na ndiyo maana alipoogopa kwa mara ya kwanza kujiunga na CHADEMA, zilifanyika taratibu nyingine za kuteua mgombea na chama kikazidi kufanikiwa.
Alisema Sitta hakumbuki hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere wakati alipopata uongozi hakuwa na wazoefu wa nchi bali aliendelea kuwatumia watendaji wa serikali ya kikoloni ambao walilazimika kufuata maagizo ya Serikali ya Tanganyika.
“Hakuna chuo cha uongozi na sisi hatuna ugomvi na watendaji wa serikali, bali tutawataka wawajibike kwa nafasi zao. Siasa na utendaji wa serikali tutaweka mbalimbali na atakayeshindwa kasi hiyo atakaa pembeni,” alisema Dk. Slaa.
Waraka mchafu wasambazwa
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, amewataka Waislamu nchini kutopumbazwa na ujumbe wa simu unaosambazwa na watu ukilenga kuwachonganisha na chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Iringa, Issa Mohamed alisema kuna kundi la watu kwa sababu wanazozijua wenyewe wameamua kusambaza ujumbe wenye lengo la kuichafua CHADEMA, huku wakijua huo ni uchochezi wa kidini.
Ujumbe huo ambao Tanzania Daima imeuona umeandikwa; “Wapendwa katika bwana tumejipanga vyema kuchukua nchi 2015, Haleluyaa. Operesheni vua gamba vaa gwanda itasaidia kuwatia mkononi Waislam. Uingereza na Ujerumani zimeahidi kuwapa vijana wetu mafunzo ya uongozi na ya kivita, tusiache maandamano kwani yanajenga chama zaidi, mawakala wetu waliomo ndani ya CCM na CUF wanafanya kazi vyema tuliyowatuma, vyombo vya habari vimeahidi kutubeba hadi kieleweke, watangazie waumini wetu kuwa ule mpango wa KICHUNGAJI unaendelea vyema kafiri kakosea namba sambaza ujumbe huu kwa Waislamu tujipange.”
Issa alisema kwa sababu ya tishio, Serikali ya CCM na wapambe wake wameogopeshwa na nguvu ya CHADEMA katika mikoa wanayopita, hivyo wameamua kubuni mbinu za kuwachonganisha na wananchi pasipo kujua hali hiyo inaliangamiza taifa.
Alivitaka vyombo vya usalama kuacha ushabiki wa kisiasa na badala yake vifuatilie hiyo meseji kwa kuwa ni sawa na uchochezi mwingine.
Kiongozi huyo aliwataka Waislamu kuzifanyia utafiti kila taarifa watazopewa ili wasije wakajuta baadae.
Wakati huo huo, Mkuu wa Operesheni Sangara katika ziara ya CHADEMA maarufu kama M4C inayoendelea, Benson Kigaila amesema kitendo cha serikali kuwaomba wasimame kupisha zoezi la sensa kimekuwa na manufaa kwao kwa kuwa wameweza kufanya kazi kubwa ambayo wasingeweza kama wangeendelea na ratiba yao.
Alisema wamefika katika kata 46 za majimbo ya Iringa mjini, Mufindi Kusini na Kaskazini na kutembelea zaidi ya vijiji 200 kwa ajili ya mikutano ya ndani na kukutana na wanachama.
“Hawa polisi na CCM ni makatibu uenezi wetu wametusaidia sana katika kutuomba tusimame kazi tuliyofanya, hakika watajuta kwanini walibuni mchezo wao huo,” alisema Kigaila.
Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment