NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, January 31, 2012

Mgomo wa madaktari wamkera RC Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi amekerwa na mgomo wa madaktari na kuwataka viongozi wa madhehebu ya dini kusaidia kabla maafa makubwa kutokea.

Dk. Nchimbi alisema hayo juzi wakati wa mahafali ya 16 ya wanafunzi wa kidato cha sita katika
Shule ya Sekondari ya Jamhuri mjini Dodoma. Katika mahafali hayo, wanafunzi 354 walitunukiwa vyeti, wakiwemo wavulana 266 na wasichana 88.

Aliwataka viongozi wa madhehebu ya dini kwenda kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
kuzungumza na madaktari kwani wanaofanya mgomo nao wana dini pia ni waumini wao.

“Muende Hospitali ya Mkoa wale madaktari ni waumini wenu, waulizeni hatua waliyoichukua inaendana na mahubiri wanayopata?” alihoji. Alisema hatua hiyo hailingani na maadili ya
kimungu kwa kuwa wagonjwa wanaotakiwa kutibiwa hasa wajawazito pia wanahitaji sana msaada wao.

“Hili si suala la kisiasa na linahitaji mikakati kulimaliza, wakumbusheni haya wanayofanya duniani watakutana nayo siku ya hukumu,” alisema. Mkuu huyo wa Mkoa ametuma salamu kwa Mbunge wa Dodoma Mjini na kumtaka atembelee shule hiyo kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge ili aone anaweza kujenga darasa lipi kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu wa madarasa.

“Nakutuma Katibu wa Mbunge, tungependa Mbunge aje atembelee shule hii kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge ili aone ni darasa lipi anaweza kujenga,” alisema. Alisema kumekuwa na taarifa zisizo sahihi kuwa taasisi za dini hazitoi fursa sawa kwa wanawake lakini ukweli ni kuwa taasisi hizo zinatambua na kutoa fursa kwa wanawake.

Dk. Nchimbi alisema kuwa taasisi za dini zimekuwa zikitoa mchango mkubwa kwa Serikali na
Taifa na kuonyesha upendo mkubwa ambao thamani yake haiwezi kupimika.

Madaktari ‘waidharau’ Serikali

JUMUIYA ya madaktari jana iliendelea ‘kuiendesha’ Serikali, tabia ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameiita dalili ya kuidharau Serikali, baada ya kukaidi kufika katika kikao chake cha majadiliano huku wakisubiriwa na mawaziri wengine sita pamoja na watendaji wengine wa juu serikalini.

Katika Ukumbi wa Karimjee, watendaji kadhaa wa Serikali na waandishi wa habari walikuwepo katika ukumbi huo kuwasubiri lakini hadi saa sita mchana hakukuwa na daktari hata mmoja aliyetokea.

Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia.

Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi, Waziri wa Mamabo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Afya, Dk, Lucy Nkya. Watendaji wakuu serikalini ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, wakuu wa Polisi na wakuu wa wilaya.

Ilipotimu saa sita na nusu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwasili na kuzungumza na waandishi wa habari kuelezea uamuzi ya Serikali baada ya kuwaita madaktari hao mara kwa mara kuzungumza nao bila mafanikio.

Walivyoanza dharau

Alisema Januari 20 mwaka huu jioni, ujumbe wa watu sita ulifika ofisini kwake na kutaka kuonana naye lakini kutokana na kuwa na ratiba ya kwenda Arusha katika maziko ya Mbunge wa Arumeru, Jeremiah Sumari, alimtaka Lyimo na Dk. Nkya kuzungumza nao na kumjulisha akiwa Arusha.

Alisema katika mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Mkopi, walifikia maelewano kurudi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuendelea na majadiliano ya madai yao ambapo walienda kesho yake na kufikia muafaka wa utaratibu wa kuyafanyia kazi.

“Hata hivyo, waliporejea kwa wenzao kutoa ripoti ya matokeo ya majadiliano na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, yalifanyika mapinduzi ya uongozi ikaundwa Kamati ya Mpito kushughulikia madai ya madaktari ikiongozwa na Dk. Stephen Ulimboka,” alisema Pinda.
Alisema alipotoka kwenye maziko alipokea maombi yao ya kuonana naye na kupangiwa siku iliyofuata yaani Novemba 24, mwaka huu, saa 11 jioni.

Pinda alisema madaktari hao hawakutokea huku namba za simu walizoacha kwa Katibu Mkuu zikiwa za waliopinduliwa na hawakuwa tayari kufika tena ofisini. Pinda alisema alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari Januari 25 mwaka huu, alitumia fursa hiyo kuwaomba waonane ili awasikilize na kutafuta ufumbuzi wa madai yao akiamini wangefanyia kazi ombi hilo baada ya kusikia katika vyombo vya habari.

“Pamoja na jitihada zote hizo, hakuna aliyekuwa tayari kufuata ushauri nilioutoa, kwa hiyo si kweli kwamba Serikali imetoa taarifa ya muda mfupi ya kutaka kukutana nao kama walivyodai na kunukuliwa na vyombo vya habari,” alisema Pinda.

Ushauri Tughe nao watupwa nje

Pinda alisema wakati wakiendelea na vikao vyao, alikutana na mawaziri kadhaa pamoja na viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ramadhani Kiwenge na kukubaliana kutuma ujumbe wa Serikali ili ikawasikilize.

Alisema alituma ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Dk. Mponda, Dk. Nkya na Ghasia kwenda kuonana nao kwenye ukumbi wa Hoteli ya Starlight Ijumaa iliyopita. Alisema katika mkutano huo yaliyotokea ni tabu kweli, kulikuwa na dalili za dharau huku wakipokewa kama siyo viongozi wao wakati waliwasilisha malalamiko yao kuomba kuonana naye.

Alisema kila mawaziri hao walipotaka kutoa maelezo ya malalamiko yao, waliandamwa na ghasia na waliporipoti kwake aliwataka kutokukata tamaa. “Lyimo aliwapigia simu juzi (Ijumaa iliyopita) asubuhi lakini hazikupokelewa ikabidi aende hadi katika Hoteli ya Starlight alipotafuta sana ili awaone lakini alibahatika kuzungumza na mwenyekiti wao tu.

“Walikataa ujumbe wangu niliompa Katibu Mkuu kwa madai hawataki kwa mdomo wanataka kwa barua, na aliponieleza nilimshauri asichoke akaandika barua na kuwapigia simu wakamtaka awapelekee karibu na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,” alisisitiza.

Alisema baada ya kupokea barua hiyo wakamwambia kuwa watamjibu na ilipofika juzi (Ijumaa iliyopita) saa tatu usiku walimpelekea barua ya kukiri kupata barua ya Waziri Mkuu na kutoa masharti matatu.

Pinda apewa masharti

Kwanza hawako tayari kukutana naye jana hadi leo ili kuwasubiri wenzao wa mikoani wahudhurie, pili Ofisi ya Waziri Mkuu iwajibu kwanza kwa maandishi madai yao kabla ya kukutana nao ili wapate nafasi ya kujadili hoja moja baada ya nyingine. Na tatu, walitaka Serikali itoe tamko wakati wa kuzungumza nao; kwamba haitatoa adhabu yoyote kwa daktari au mtumishi wa kada yeyote wa afya kutokana na mgomo huo.

Uwezekano wa kufikia muafaka

Pinda alisema kutokana na ukubwa wa mahitaji yao hawawezi kutekeleza mara moja, lakini kutokana na mzungumzo ikiwa wangekutana, wangefikia muafaka kwani uchumi wa nchi pia unaamua mambo mengi. Alisema kwa kutizama madai yao, ufumbuzi ungepatikana kwa mazungumzo na siyo kutoa amri ya kutaka ifanyike mara moja kama posho ya kulala kazini ambayo wanalipwa Sh 10,000 kweli ni ndogo wangeweza kuiongeza.

Alisema kwa dai la posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi, lingeweza kuangalia kwa makundi kwa wale wanaofanya kazi katika wodi za vichaa, katika mionzi na wengineo kwa kuwa inawezekana. Kuhusu uhaba wa nyumba, alisema uahaba huo upo kwa sekta nyingi hata polisi na wanajeshi, lakini kuna juhudi Serikali inafanya kwa kutambua hilo kwa kujenga nyumba 10 kwa kila wilaya katika wilaya 18 hivyo wangeweza kujadili kutoa posho bila kujali cheo.

Alisema kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu Serikali inaelewa na ipo tayari kutoa posho katika ameneo yasiyo na mvuto kwa watumishi wa kada mbalimbali.
“Kama kuhusu usafiri, utaratibu wa kukopeshana magari upo serikalini, kama tungekutana tungeona namna ya kuwapa kipaumbele kwa wanaoishi maeneo yanayolazimu usafiri kwa kuwa mfuko huo hautoshi,” alisema.

Kuhusu bima ya afya, Pinda alisema ni jambo la kuangalia na kama fedha ipo, siyo mbaya kutibiwa maeneo mazuri na kuongeza kuwa alidhani wangetaka kutibiwa bure na familia zao katika hospitali wanazofanyia kazi. Alisema katika suala la mshahara siyo rahisi kutekelezwa kwa kiwango hicho kwa mtumishi wa umma kwani ni lazima ufahamike kuwa utumishi wa umma pia unatoa huduma, hivyo ni vyema kutambua kuwa wako wa kada mbalimbali ingawa wao ni muhimu lakini kuna haja ya kuwa na uwiano.

Pia alisema kutaka uongozi wote wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ujiuzulu, siyo jambo la msingi kwani hawakutoa sababu ya msingi na kama kucheleweshwa kwa posho ni suala la serikali siyo wizara. Alisema kama upo upungufu mwingine wasioujua serikalini hilo lingejadilika lakini kuweka uongozi huo wote wa Wizara katika kundi moja kwa tuhuma zisizojulikana siyo sawa.

Pinda alisema huduma duni kwa wananchi ni moja ya changamoto kubwa serikalini ikiwa ni sehemu ya changamoto nyingi zilizopo katika sekta mbalimbali ambazo Serikali wanafanyia kazi hatua kwa hatua.

Uongozi wa mgomo mamluki

Alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari hao inayoongoza mgomo, Dk. Stephen Ulimboka siyo mtumishi wa Serikali na hajasajiliwa kama daktari kwa kuwa usajili wake ulisitishwa na Baraza la Madaktari mwaka 2005 baada ya kuongoza mgomo wa madaktari nchi nzima.

Kwa mujibu wa Pinda, Ulimboka alihitimu Shahada ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2004 na kupata usajili wa muda wa baraza kisha kupangiwa mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Alisema Novemba mwaka 2005, alishitakiwa katika Baraza kwa Ukiukwaji wa Maadili ya Taaluma ya Udaktari kwa kuitisha mgomo ambao ni makosa kimaadili na kukataa kufika mbele ya baraza kujibu tuhuma hivyo shauri lake halikumalizika.

Pinda alisema mwaka 2006, Rais alimsamehe na kurejeshewa usajili wa Baraza na kuruhusiwa kuendelea na mafunzo ya vitendo lakini hakuna taarifa kama alimaliza mafunzo hayo kwa kuwa hajawasilisha cheti cha kumaliza mazoezi na haifahamiki anafanya kazi wapi ingawaje inasemekana anafanya katika taasisi isiyo ya kiserikali (NGOs) inayojihusisha na masuala ya Ukimwi.

“Katika kumpa taarifa za msamaha wa Rais, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Baraza la Madaktari kwa nyakati tofauti walimtaka kutojihusisha na mgomo au suala lolote ambalo ni kinyume cha maadili ya taaluma ya udaktari,” alisema Pinda. Alisema Ulimboka katika barua yake ya Februari 2, 2007 ambayo ipo serikalini alikiri kwamba hatajihusisha wala kutoa ushawishi wowote kwa wengine kufanya vitendo kinyume na maadili ya udaktari.

Akizungumza na gazeti hili, Ulimboka alikiri kuitwa na Baraza la Madaktari mwaka 2005 na kweli alikuwa kiongozi wa mgomo huo wa madaktari. Alisema mwaka 2007 alimaliza mafunzo yake ya vitendo katika Hospitalia ya Mwananyamala na kupewa cheti chake katika Hospitali ya Muhimbili alipofukuzwa kabla ya mgomo kama utaratibu ulivyo.

Alikana kuandika barua Serikalini na kumtaka Waziri Mkuu kama anayo, aiweke hadharani huku akikiri kutokuwa mtumishi wa serikali na kudai siyo sababu ya kumzuia kutopigania maslahi ya madaktari.

30 wanusurika kuzama Ziwa Victoria

ZAIDI ya watu 30 wakiwepo watoto wadogo wanne wamenusurika kuzama katika Ziwa Victoria baada boti mbili kugongana eneo la Mwikoko karibu na jengo la maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Ajali hiyo ilitokea jana saa 11 alfajiri, ambapo boti ya uvuvi yenye namba za usajili RMU 5234 iligongana na boti ya abiria iliyojulikana kwa jina la mv Nyanganira inayomilikiwa na Ramadhan Nyanganira.

'Habarileo' lilifika eneo la ajali na kushuhudia boti hizo zikiwa zimeharibika huku kukiwa na madai ya watu kutoonekana baada ya baadhi yao kuokolewa. Baadhi ya mashuhuda na abiria walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa boti hizo na kutozingatia sheria za unahodha.

“Kabla ya ajali kutokea kama meta mia moja hivi, abiria walimuambia nahodha aangalie mbele boti iliyokuwa ikija, lakini alishindwa kumiliki vyema boti hiyo na alipokata kona tu boti ya uvuvi iligonga katikati,” alisema mmiliki wa boti hiyo, Nyanganira na kuongeza:

"Hatuwezi kusema kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha, ukweli utapatikana baada ya siku moja au mbili”. Abiria wa boti hilo aliyejitambulisha kwa jina la Eunice Maagi, mkazi wa Kiabakari aliyedai alikuwa akitoka kwenye msiba katika kijiji cha Kibuyi wilayani Rorya, alisema kuwa hadi alipookolewa na kupata fahamu vizuri, hakuna mtu yeyote aliyelalamika kama ndugu, jamaa au rafiki yake haonekani.

“Hakuna niliyemsikia analalamika kuwa amepotelewa na mtu sijui kwa kuwa bado
tumechanganyikiwa na pia kutojuana kutokana na kila mtu kuwa na safari yake, lakini sisi tulikuwa kama sita na wote tumeokolewa na tupo salama,” alisema Maagi.

Lowassa, familia wachangia KKKT Simiyu mil. 21/-

KANISA la Kiinjili na Kilutheli Tanzania (KKKT), linalotarajia kuanzisha Dayosisi mpya ya Shinyanga na Simiyu limefanikiwa kukusanya Sh milioni 116 taslimu ambapo kati ya hizo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na familia yake walichangia Sh milioni 21.

Katika harambee hiyo, Mchungaji wa KKKT, Philbert Celestine alimshukuru Lowassa na familia yake pamoja na wageni waalikwa kwa kufanikisha mchango huo ambao ulivuka lengo.

Awali, harambee hiyo ilikuwa na lengo la kupata Sh milioni 114 ili kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo lakini walifanikiwa kuvuka lengo na kupata Sh milioni 204, kati ya hizo fedha
tasilimu zikiwa ni Sh milioni 116.

Akisoma risala kwa niaba ya KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Mchungaji Celestine alisema kuwa kanisa hilo jipya likimalizika na kuifikia malengo waliyojiwekea,
litasaidia katika kukuza ufahamu wa kiroho baina ya waumini wa dayosisi hiyo mpya ambayo inatarajia kufunguliwa mapema mwaka 2013.

Alisema lengo lao ni kuwafikia na kupanua huduma ya neno la Mungu kwa kuwajenga waumini hao hasa ukizingatia Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa mauaji ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Kwa upande wake, Lowassa akizungumza waumini hao, alisema kuwa suala la ujenzi wa makanisa nchini ni zuri na ni vema kwa sasa kutokuwategemea wafadhili kama ilivyokuwa awali na badala yake tubadilike kwa kujenga sisi wenyewe.

“Zamani tulikuwa tumezoea kujenga makanisa kwa kuwategemea wafadhili mbalimbali kutoka nje ya nchi hasa wazungu, lakini kwa sasa tubadilike tujenge wenyewe kwani uwezo tunao wa kuchangishana,” alisema Lowassa.

Lowassa alisisitiza kuwa yeye yupo tayari kurudi akiitwa katika harakati zozote za kuchangia ujenzi wa nyumba za ibada. Askofu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Andrea Gule akitoa shukrani zake katika harambee hiyo, aliwataka wananchi na waumini kwa ujumla kuwa na moyo wa kuthubutu katika kuchangia ujenzi hasa wa nyumba za ibada ili kuwakomboa
watu kiroho.

Madaktari rudini kazini - Pinda aagiza


SERIKALI imewaagiza madaktari wote walio katika mgomo kurejea kazini leo asubuhi na asiyeripoti atakuwa amepoteza ajira serikalini.

Uamuzi huo wa Serikali umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, katika mkutano na waandishi wa habari katika viwanja vya Karimjee baada ya madaktari hao kususa kukutana naye kuzungumzia malalamiko yao.

Pinda pia amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na waganga wakuu katika hospitali zote nchini kukagua watumishi wao leo na asiyekuwepo kazini jina lake lipelekwe ashughulikiwe.

Alisema Serikali tayari imechukua tahadhari ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupeleka madaktari kutoka katika Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam, ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini.
Waziri Mkuu pia ameagiza vyombo vya dola kuzuia mikutano yoyote ya madaktari hao inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Wamegoma suluhu

Pinda alisema katika hatua iliyofikiwa, Serikali imetambua kwamba madaktari wanaongozwa na Kamati ya Mpito, hawataki suluhu kwa kuwa imefanya juhudi za kuwaita kwa kuwabembeleza ili kujadili na kushughulikia madai yao bila mafanikio. Alisema baada ya kuwabembeleza kwa muda mrefu ili kupata suluhu ya tatizo hilo bila mafanikio, wameona wasiendelee na mgogoro na kuonekana Serikali haina maana kwani watu wanaumia na madaktari hawataki mazungumzo.

Pinda amekiri kuwa atakabiliwa na changamoto, lakini akasema bora kushughulikia changamoto hiyo mpya kuliko kuendelea na iliyopo sasa. Alisema mbali na kuomba madaktari kutoka jeshini, Serikali pia imewaoamba madaktari wenye utu na ubinadamu kuendelea kutoa huduma wakati jitihada za kuwatafuta madaktari wengine katika taasisi binafsi zikiendelea.


Madai yao kushughulikiwa

Alisisitiza kuwa licha ya uamuzi huo, amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia kuendelea kushughulikia malalamiko ya madaktari hao na kwa yale yanayowezekana yaingizwe kwenye bajeti ijayo ili kuwasaidia watakaokuwepo kazini.

“Madaktari hawa wamefanya kinyume kwa mujibu wa kiapo na sheria za nchi zinazowaagiza wazi kutojihusisha na migomo, hususani katika sekta yao ambayo inahusu uhai wa binadamu kwa kuwa husababisha kupoteza maisha bila sababu,” alisema.

Mikoa 14, wilayani shwari

Waziri Mkuu alisema tangu mgomo uanze, Serikali imekuwa ikifuatilia kutoka katika mikoa yote na hadi kufikia juzi, katika mikoa 14 hospitali za mikoa na za wilaya hazikuwa na mgomo.
Mikoa hiyo ni Ruvuma, Lindi, Mtwara, Shinyanga, Arusha, Tabora, Kagera, Iringa, Mara, Pwani, Kigoma, Singida, Manyara na Rukwa.

Alisema katika mikoa saba, baadhi ya hospitali za mikoa zilikuwa katika mgomo huku hospitali za wilaya zote za mikoa hiyo, zikiendelea kutoa huduma kama kawaida. Mkoani Kilimanjaro Pinda alisema mgomo ulikuwepo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambao ulihusu madaktari waliopo katika mafunzo kwa vitendo.

Mbeya Pinda alisema mgomo ulikuwa kwa madaktari 65 walioko katika mafunzo kwa vitendo, madaktari kumi waliosajiliwa na madaktari bingwa kumi. Hospitali nyingine zilizogoma ni za Mkoa wa Mwanza ambako hata hivyo hakukuwa na mgomo wa wazi licha ya madaktari 46 wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kutoa tangazo la wazi la kushiriki mgomo, lakini dalili za mgomo zikionekana kwa waliopo katika mafunzo ya vitendo.

Alisema Morogoro waligoma madaktari katika Hospitali ya Mkoa wakati Tanga watumishi wote wa kada zote katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo walikuwa na mgomo wa chini chini na Dodoma katika Hospitali ya Mkoa na Dar es Salaam mgomo huo ulipoanzia.

Mshahara na mlolongo wa posho wanazodai

Pinda alisema katika barua ya madaktari hao ya Januari 27 mwaka huu kwake, walitoa madai nane wakitaka mshahara wa daktari anayeanza kazi kuwa Sh milioni 3.5 kwa mwezi.
Kwa sasa katika madai hayo walidai wanalipwa Sh 700,000 lakini Pinda alisema wanalipwa Sh 957,700 na ndio wanaoongoza kwa malipo mazuri katika sekta ya umma. Wanaofuata kwa mujibu wa Pinda ni wahandisi Sh 600,000 na wahasibu kati ya Sh 300,000 hadi Sh 400,000.

“Uamuzi wa kuwawekea mshahara mkubwa madaktari ni wa makusudi kwa kutambua umuhimu wao katika kubeba maisha ya watu, inawezekana haitoshi lakini nyongeza ya posho kwa asilimia mia na ishirini hakuna Serikali inayoweza kuongeza,” alisema.

Mbali na mshahara huo, madaktari hao kwa mujibu wa Pinda, wamependekeza kulipwa posho ya kulala kazini ya asilimia 10 ya mshahara wa mwezi. Kwa sasa wanalipwa Sh 10,000 kwa siku. Pia wametaka posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi asilimia 30 ya mshahara wa mwezi na posho ya nyumba asilimia 30 ya mshahara au wapewe nyumba.

Madaktari hao pia wamependekeza walipwe posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara na posho ya usafiri asilimia 10 ya mshahara au ikishindikana wakopeshwe magari. Baada ya mlolongo huo wa posho, madaktari hao ndio wakaweka pendekezo la kutaka madaktari waliokuwa katika mafunzo ya vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, warejeshwe mafunzoni hospitalini hapo.

Kipato cha Sh milioni 17

Pinda alisema kwa mujibu wa mapendekezo ya madaktari hao, akilipa mshahara wa Sh milioni 3.5 kwa mwezi na posho hizo, daktari anayeanza kazi atalipwa Sh milioni 7.7 kwa mwezi na Daktari Mshauri Mwandamizi atalipwa milioni 17.2 kwa mwezi.

Alisisitiza kuwa ili kutekeleza pendekezo hilo, Serikali italazimika kurekebisha viwango vya mishahara kwa watumishi wote wa kada ya afya na nyingine, ili kuweka uwiano kufuatana na muundo katika utumishi wa umma. “Kwa kuzingatia ukubwa wa gharama hizi, utekelezaji wa mapendekezo ya madaktari utakuwa hauwezekani kwa kuzingatia hali halisi ya bajeti ya Serikali,” alisema Pinda.

Alisisitiza kuwa madai yao ni sawa na nyongeza ya Sh bilioni 301.7 katika bajeti ya mshahara ya mwaka 2011/ 2012 ukijumlisha na nyongeza ya posho kwa watumishi wengine wa kada ya afya kwa miezi mitano iliyobaki, watapaswa kulipwa posho ya Sh bilioni 84.3.

Pinda alisema katika makundi hayo mawili tu; mishahara na posho Serikali itajikuta ikitoa Sh trilioni 2, ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya mishahara ya wafanyakazi wote serikalini ambayo kwa sasa ni Sh trilioni 3.45. Kwa maana hiyo, Pinda alisema madaktari wanataka wapewe theluthi mbili za mishahara ya wafanyakazi wote na waliobakia, wagawane theluthi moja iliyobakia jambo ambalo haliwezekani.

Monday, January 30, 2012

Zitto: Futeni posho tuboreshe maslahi ya watumi

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema serikali inapaswa kufuta kabisa mfumo wa posho za vikao katika stahili za viongozi na badala yake iboreshe maslahi ya watumishi wote kuepusha migomo kama inayoendelea sasa kwa madaktari.
Mbali na kutaka posho hizo ziondolewe, pia alisema kuna wabunge wanawapotosha wananchi kwa kuwaambia suala la posho ni suala lake binafsi kwa kile wanachoeleza kuwa ana vyanzo vingine vya mapato.
Zitto alitoa kauli hiyo jana katika Kanisa la Maisha ya Ushindi lililopo Ubungo External jijini Dar es Salaam, wakati akizindua albamu ya nyimbo za Injili ya msanii Miriam Ikombe.
“Tukizungumzia ugumu wa maisha wengine wanasema sisi wa upinzani tuna vyanzo vingine vya mapato, wanatutaka tusiseme ukweli juu ya maisha magumu yanayosababishwa na ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali ya nchi. Kwa hakika nchi imefika pabaya kwa kila anayesema ukweli kufikiriwa ana maslahi binafsi,” alisema Zitto.
Kuhusu mgomo wa madaktari, alitaka umalizwe kwa hekima na kueleza kuwa malipo duni kwa wafanyakazi wa umma ni matokeo ya uchumi kutozalisha mapato ya kutosha, hivyo kutaka uzalishaji uongezwe kwa kile alichosema bila uzalishaji hakuna kodi na mishahara itaendelea kuwa midogo.
“Hapa nataka viongozi wenzangu tuhamasishe watu kufanya kazi, tuonekane mashambani na viwandani na tuwe wakweli kwa wananchi, wabunge watumie muda wao kuzungumzia namna ya kukuza uchumi na kuleta ajira pia, kuwe na mkakati wa kweli wa kutokomeza ufisadi kwani nchi ni tajiri ila wananchi wake wanafanywa kuwa maskini kwa makusudi ya wachache,” alisema Zitto.
Alisema kwa jinsi gharama za maisha zinavyopanda kila kukicha huku wachache ndiyo wakifikiriwa kukabiliana na ongezeko hilo, ni wazi itakuwepo migomo isiyoisha katika jamii kwani hata kama madktari watatatuliwa matatizo yao leo, kuna uwezekano mkubwa sekta zingine zikaingia katika migomo.
“Tusishangae hata siku moja maaskari nao wakagoma kwa maana duka atakaloenda kupata mahitaji yake, mbunge anayelipwa laki mbili kwa siku ndilo hilohilo analotumia mfanyakazi anayelipwa chini ya laki moja na nusu kwa mwezi,“ alisema Zitto.

Madiwani watakiwa kukaribisha wawekezaji makini


MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, wametakiwa kuhamasisha wawekezaji ili kuwekeza kwenye miradi mbalimbali nchini kwani hali hiyo itawezesha upatikanaji wa ajira kwa vijana wilaya hiyo.
Wito huo ulitolewa jana na diwani wa kata ya Namtumbo mjini Alpihus Mchucha, katika kikao cha baraza la madiwani wakati akichangia hoja iliyosomwa na Kamati ya Uchumi na Mazingira kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo na kuwashirikisha watalamu wa idara mbalimbali.
Diwani Mchucha alisema kuwa ili kuweza kuyalinda mazingira vizuri na kupanua ajira kwa vijana ni vyema wawekezaji hao wakatambuliwa pia na Watanzania hasa katika kulinda mazingira na kupanua ajira ndani ya wilaya hiyo.
Tusipokuwa makini katika kutoa mikataba kwa wawekezaji tutajikuta tumewaacha wawekezaji wenye faida kuwaingiza wawekezaji wasio na faida kwetu jambo ambalo tutakuja kuanza kulaumiana pasipo sababu,” alisema diwani huyo.
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Namtumbo, Stephen Nana, alisema kuwa ni vyema wataalamu na madiwani kuzingatia yale yote yaliyojadiliwa kwa kuyafanyia kazi ili halmashauri iweze kuinuka kiuchumi na jamii kunufaika nayo.

Mwakyembe aibukia kanisani

•  Asema mafisadi wameshindwa kummaliza

HATIMAYE Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa mara ya kwanza ameonekana hadharani tangu atoke India kwa ajili ya matibabu.
Dk. Mwakyembe alionekana jana kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, katika ibada maalum ya kumshukuru Mungu kwa muujiza wa kupona ugonjwa uliokuwa unamsumbua.
Kiongozi huyo alisema kuwa nguvu za mafisadi zimeshindwa kummaliza.
Alisema kuwa hivi sasa anatarajia kuzunguka kwenye makanisa mbalimbali nchini kutangaza kushindwa kwa wabaya wake ambao walipanga kummaliza.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na madai kuwa Dk. Mwakyembe amelishwa sumu, lakini jana hakuweka bayana ni ugonjwa gani unaomsumbua na umesababishwa na nini
“Sikuwahi kuvaa viatu tangu nilazwe nchini India, lakini kwa mara ya kwanza leo nimevaa, shetani alipanga kunimaliza lakini ameshindwa.
Nimepanga kuzunguka kwenye makanisa kumzomea shetani (mafisadi) kwamba ameshindwa na kuwashukuru watu wa Mungu kwa maombi yao,” alisema.
Kikosi cha wapambanaji wa ufisadi
Katika ibada hiyo, Dk. Mwakyembe alisindikizwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; mbunge wa Kahama James Lembeli (CCM); mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM); na Aloyce Kimaro, aliyekuwa mbunge wa Vunjo.
Makada hao waliojipambanua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi walisema kuwa kamwe hawataogopa chochote katika mapambano dhidi ya ufisadi kwa kuwa neema inakuja siku za usoni.
Sitta alisema machozi ya Watanzania hayawezi kupotea bure dhidi ya mafisadi ambao wameamua kuzitumia rasilimali za taifa kujinufaisha.
“Neema inakuja na nchi itarudi kwenye mstari ambao Mwalimu Julius Nyerere alitamani taifa liwe, hakutaka liwe hivi leo ambapo baadhi ya watu wanatumia migongo ya wenzao kupata mafanikio.
Nchi leo imejaa magenge ya waovu ambao wamejipanga kuitafuna bila kujua Tanzania ni ya Mungu, mimi pamoja na kundi langu la kupambana na ufisadi hatuogopi chochote,” alisema Sitta.
Sitta alitumia muda mwingi kuzungumzia unyonywaji unaofanywa na waovu (mafisadi) ambao wamewaacha wananchi wakiishi maisha magumu bila msaada wowote.
Huku akishangiliwa na umati mkubwa wa waumini waliohudhuria kanisani hapo, Sitta alisema viongozi wengi wanatumia dhamana waliyopewa kwa ajili ya kuliibia taifa kitendo kisichokubalika mbele ya Mungu.
Akitumia kifungu cha Biblia (Habakuki 1:2-4) alisema kilio cha Watanzania juu ya maovu na kutotendewa haki kitafutwa hivi punde.
“Hata kwenye nchi yetu wananchi wanalia juu ya shida walizonazo, huku uovu na udhalimu ukiendelea; hakuna pa kukimbilia, haki hakuna kama ipo imelegea na inawanufaisha mafisadi.
Mikopo ya wanafunzi inacheleweshwa makusudi kwa lengo la wanafunzi hao kufukuzwa kwa kukosa ada, nchi inanyonywa, lakini Mungu anaona na iko siku ataingilia kati, hawezi kukubali watu wake wateseke,” alisema.
Alienda mbali zaidi na kusema nchi itapona na uongozi utabadilika.
Ugonjwa wa Mwakyembe
Waziri Sitta amesisitiza kwa mara nyingine kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Harrison Mwakyembe, alilishwa sumu.
“Nilishasema na narudia tena alilishwa sumu; mimi nimekuwa naye muda mrefu akiwa India na madaktari wa kule wanasema alilishwa sumu, kama wanabisha vyombo vya uchunguzi vitoe majibu haraka,” alifafanua.
Alisema miguu ya Mwakyembe ilikuwa kama ya tembo na ngozi yake ilikuwa inatoa unga.
Anne Kilango atema cheche
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, alisema ataendelea kupambana na kamwe hatachoka, kwani amevumilia mengi katika kuwawakilisha wanyonge.
“Naipenda nchi yangu na napenda haki, kiongozi bora ni yule anayetenda haki kwa wananchi wake, nitaendelea kusimamia na kusema kweli,” alisema.
Alisema amezaliwa kwa ajili hiyo na ataendelea kupigania haki ya wanyonge.
James Lembeli anena
Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), amesema licha ya Bunge kuwa ni mhimili wa nchi lakini ndiko kwenye ufisadi mkubwa.
“Wachungaji na viongozi wa dini liombeeni Bunge kwani watenda maovu wako huko, kwani wabunge wengi husimama kwa ajili ya kutetea nafsi zao na kamwe Askofu Josephat Gwajima usikubali mafisadi kuathiri kanisa lako,” alisema.
Kauli ya Aloyce Kimaro
Kimaro naye alisema yote yanawezekana kama Mungu alivyosema na siku zote ukweli unahitajika.
Kimaro aliongeza kuwa ukweli hauchagui mtoto au mkubwa na vigumu kwao kutendewa baya kwa vile Mungu mara nyingi hupenda mkweli.
“Mkiona wala rushwa semeni ukweli, hakuna watakalowafanya; Mungu atawalinda kutokana na kumpenda mtu wa namna hiyo,” alisema.
WAKATI huo huo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amechangisha zaidi ya sh milioni 204 katika harambee ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), lililoko mjini Shinyanga, hivyo kuvuka lengo halisi.
Lowassa ambaye alikuwa mgeni rasmi jana katika harambee hiyo iliyolenga kukusanya sh milioni 115, kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo hatua ya kuezeka, alikuwa kivutio kikubwa kwa waumini ambao wakati mwingi walikuwa wakimshangilia.
Akizungumza katika harambee hiyo, iliyochangisha sh milioni 136 zilipatikana taslimu na ahadi ya sh milioni 68, Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli (CCM), alitoa wito kwa Watanzania kujenga milango mipana ya ushirikiano wa kimaendeleo.
Alisema, Watanzania wanao wajibu mkubwa kuhakikisha kwamba wanadumisha maradufu ushirikiano, ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu kuchangia shughuli mbalimbali za madhehebu ya dini badala ya kutegemea msaada kutoka kwa wahisani.
“Zamani tulikuwa tukitegemea sana Wazungu watusaidie, lakini kwa sasa tunashukuru hali hiyo imeenda inatoweka,” alisema Lowassa ambaye alitumia muda usiozidi dakika nne kuhutubia kwenye harambee hiyo.

Serikali yageuka mbogo

•  Madaktari wasema hawataenda kazini, kesho kukutana

SERIKALI imetangaza kuwafuta kazi madaktari wote watakaoendelea na mgomo huku ikiviamrisha vyombo vya dola kuwakamata watakaodiriki kufanya mikutano kwenye maeneo mbalimbali.
Msimamo huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Karimjee na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya madaktari kushindwa kufika kwenye mkutano ulioandaliwa kuzungumzia madai na mgomo wa wataalamu hao.
Pinda aliwaamaru madaktari wanaoendelea na mgomo katika mikoa saba nchini kurejea kazini mara moja leo asubuhi huku akiweka wazi watakaokiuka agizo hilo watapoteza ajira zao.
Alisema serikali inatambua madaktari hao wanaongozwa na kamati ya mpito isiyotaka suluhu licha ya juhudi zilizofanywa za kuwaita kushughulikia madai husika.
“Serikali tayari imechukua tahadhari ya kukabiliana na hali hii kwa kuagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupeleka madaktari wake katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini. Kwa hiyo huduma zitaendelea kama kawaida,” alisema Pinda.
Katika mkutano huo Pinda aliongozana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya; Waziri wa Nchi Ofsi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia; Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha; na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika.
Akionekana kukerwa na kitendo hicho cha madaktari hao kushindwa kukutana naye, Pinda alisema kuanzia leo ameviagiza vyombo vya dola kuzuia mikutano yote ya madaktari hao, akisema ni kinyume cha sheria ingawa serikali ilikuwa ikiwavumilia tu.
“Mgomo wao si sahihi kwa sababu haukufuata taratibu za kuuitisha. Wao walipaswa kutangaza mgogoro na kisha kutoa notisi ya siku 60, jambo ambalo hawakufanya,” alisema Pinda na kukipongeza Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (Tughe) kwa kutambua hoja za madaktari hao lakini wakasema njia iliyotumika si sahihi.
Pinda ambaye aliwasili ukumbuni hapo saa 6:12 mchana badala ya saa 4:00 kama ratiba ilivyokuwa, alianza kwa kufafanua chimbuko la mgomo huo na hatua kadhaa zilizochukuliwa na serikali kuutatua.
Alisema tangu mwishoni mwa Desemba mwaka jana, kulikuwa na madai ya wataalamu mbalimbali waliokuwa kwenye mazoezi kwa vitendo (interns) kwamba wangeitisha mgomo kwa sababu ya kucheleweshewa posho zao; alisema juhudi zilifanyika na wakalipwa madai hayo yaliyokuwa yakifikia sh milioni 876.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya malipo kufanyika, mgogoro ulihama kutoka kwa interns na kuwahusisha wataalamu wa kada nyingine za afya wakiwemo madaktari na kwamba kwa kuwa interns hao nafasi zao zilikuwa zimezibwa wakati wakiwa wamegoma, serikali iliona ni vyema kuwasambaza kwenye hospitali nyinge jijini hapa.
“Uhamisho huo ulifanywa kwa nia njema ila wenzetu waliutafsiri kama adhabu ya kuwakomoa interns hao na kupitia Chama chao cha Madaktari (MAT), walileta madai kuwa tuwarejeshe Muhimbili wakitoa sababu nyingi ambazo kimsingi tuliona zina mantiki,” alisema Pinda.
Aliongeza kuwa wakati wakiwa kwenye majadiliano ya hoja hiyo na yeye kuonyesha nia ya kukutana nao, MAT walienguliwa na jukumu hilo kupewa Jumuiya ya Kamati ya Mpito iliyoongozwa na Dk. Stephen Ulimboka, ambayo ilitoa madai nane.
Katika madai yao walitaka posho ya kulala kazini ya sh 10,000 kwa siku, ilipwe kwa kiwango cha asilimia 10 ya mshahara wa mwezi, posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi iwe asilimia 30 ya mshahara wa mwezi; na posho ya nyumba walipwe asilimia 30 ya mshahara wa mwezi.
Madai mengine ni kupandishwa kwa posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu zifikie asilimia 40 ya mshahara, kupatiwa posho za usafiri kwa asilimia 10 ya mashajara iwapo itashindikana wapatiwe usafiri wa kwenda na kurudi kazini.
“Wanadai mshahara wa sh 700,000 ni mdogo sana kwa daktari anayeanza kazi, hivyo wanapendekeza alipwe sh 3,000,000 kwa mwezi. Wanataka kupatiwa bima ya afya pamoja na familia zao kwa kupewa kadi za kijani na wanataka interns warejeshwe Muhimbili bila masharti yoyote,” alisema Pinda.
Hata hivyo, akichambua madai hayo alisema serikali haiwezi kuyapatia ufumbuzi mara moja madai hayo ila taratibu za kuyapatia ufumbuzi zinaendelea huku akikanusha kuwa daktari anayeanza kazi analipwa sh 700,000 bali ni sh 957,7000.
Alisema madaktari hao wamependekeza wanaoajiriwa hivi sasa walipwe mshahara wa sh milioni 3.5 wakati watumishi wa kada nyingine kama wahandisi wanaanza na sh 600,000 na wahasibu wanaanza na mshahara wa sh 300,000; kwamba posho zote wanazodai zikijumuishwa zinafikia asilimia 120 ya mshahara wa daktari mmoja.
“Kwa mujibu wa mapendezo yao ina maana kiwango cha kuanzia mshahara wa mhudumu wa afya kitakuwa sh 670,316 na mshahara wa juu utakuwa sh mil. 8.1 kwa mwezi. Utekelezaji wa pendekezo hili utagharimu sh bil 83.5 kwa mwezi ambayo ni sawa na sh bil. 417.5 kwa kipindi kilichobaki cha miezi mitano,” alisema.
Pinda alifafanua kuwa kwa mujibu wa mapendekezo hayo mshahara na posho, daktari anayeanza kazi atapata sh mil. 7.7 na daktari mshauri mwandamizi atapata sh mil. 17.2 kwa mwezi.
“Endapo madai hayo yatatekelezwa kwa mwaka mmoja jumla ya mishahara yao itakuwa sh bil. 799.7 badala ya sh bil. 222. 2 hadi kufika Juni 2012.
Kiongozi wao si daktari
Katika hatua nyingine, Pinda alisema kuwa katika uchunguzi wao walibaini kuwa kiongozi wa mgomo, Dk. Ulimboka alihitimu shahada ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2004 na kupata usajili wa muda No. 2022 wa Baraza la Madaktari mwaka huu na kupangiwa internship Muhimbili.
Alisema kuwa Novemba 2005, aliongoza mgomo wa madaktari nchini na usajili wake ulisitishwa na kushtakiwa mbele ya baraza hilo kwa ukiukaji wa maadili ya taaluma ya madaktari kwa kutishia na kufanya mgomo.
Mwaka 2006 Rais alimsamehe na hivyo kurejeshewa usajili na baraza na kuruhusiwa kuendelea na internship.
“Katika kumpa taarifa za msamaha wa Rais, Wizara ya Afya na Baraza la Madaktari walimtaka Dk. Ulimboka kutojihusisha na migomo au suala lolote kinyume na maadili ya udaktari ambapo Februari 2, 2007 alikiri sharti hilo kwa maandishi.
Hadi sasa hakuna taarifa kama alimaliza internship kwa kuwa hajawasilisha cheti cha kumaliza mazoezi hayo na hatuna taarifa anafanya kazi wapi ila si mtumishi wa serikali na hajasajiliwa kama daktari, alisema Pinda.
Dk. Ulimboka anena
Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alisema hakuna sheria ya kumfukuza mfanyakazi asiyeenda kazini kwa siku moja na hivyo kuwataka madaktari waendelee kukaa nyumbani.
Alisema leo wanafanya taratibu za kisheria ili kesho wakutane kuzungumzia mgomo huo ambao sasa serikali inaonekana kutaka kutumia nguuvu kuwasambaratisha.
Alibainisha kuwa sababu ya wao kushindwa kwenda kukutana na Waziri Mkuu jana ni kuchelewa kupata barua ya wito wa kuitwa kwenye mkutano.
“Sisi tulipata barua saa 11 jioni na tukaandika barua kumjibu Pinda kuwa hawawezi kukutana leo kwa kuwa wenzao wengine wameshatawanyika, pia tulifanya hivyo kwa kuwa jana tulitarajia wenzetu kutoka mikoani wangewasili Dar es Saalam.”
Kuhusu kutohitimu mafunzo ya udaktari, alisema huo ni uongo kwa kuwa alimaliza mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Muhimbili na kutunukiwa cheti chake cha udaktari mwaka 2007.

Rais Kikwete katika mkutano wa Umoja wa Afrika Ethiopia

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na viongozi wenzie katika mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa Ethiopia jana Januari 29, 2012.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa Ethiopia jana Januari 29, 2012.
Viongozi wa Afrika wakiwa wamesimama wakati wimbo wa Umoja wa Afrika ukipigwa.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akijadiliana jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh Bernrd Membe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar (Fedha na Uchumi), Dr Mwinyihaji Makame Mwadini katika mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa Ethiopia jana Januari 29, 2012.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na Rais Paul Kagame wa Rwanda kabla ya kuanza rasmi kwa mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa Ethiopia jana Januari 29, 2012.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipanda mti kama kumbukumbu ya mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa Ethiopia jana Januari 29, 2012.

PICHA ZOTE NA IKULU

Sunday, January 29, 2012

Urais CCM 2015 balaa

KIGOGO AMWAGA MAMILIONI, ATUMA MAKADA MIKOANI KUMNYOSHEA NJIA
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikionya wanachama wake kuacha ndoto za urais wa mwaka 2015, kauli hiyo sasa imeonekana kupuuzwa na kugeuka kichocheo cha kuongeza kasi ya kujipanga kwa baadhi ya makada wenye nia ya kusaka nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa taifa.Hivi karibuni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alionya kwamba chama hicho hakiko tayari kuendelea kuwakumbatia wanachama wake wanaunda makundi ndani ya chama, kwa lengo la kusaka umaarufu wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Nape alisisitiza kuwa endapo mwanachama yeyote atabainika kuvuruga mshikamano ndani ya chama kutokana na kigezo hicho, CCM haitasita kuchukua hatua kali dhidi yake.

Pamoja na CCM kutoa onyo hilo kali, mbio za urais wa mwaka 2015 ndani ya chama hicho, zimeelezwa kuingia katika sura mpya baada ya mmoja wa makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo, kufanya kikao kizito jijini Arusha, kwa lengo la kuweka mikakati ya kujipanga na kuimarisha kambi yake.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya wana CCM mjini Arusha, zinaeleza kuwa, kigogo huyo alifanya kikao chake wiki chache zilizopita katika moja ya majengo ya mfanyabiashara mmoja kutoka Kanda ya Ziwa, yaliyopo nje kidogo ya jiji.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na baadhi ya viongozi wa CCM kutoka mikoa mbalimbali nchini, wakiwamo baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa chama hicho na baadhi ya viongozi wa Serikali, pamoja na mambo mengine, kilifanya tathmini ya kina kujua maeneo ambayo mgombea huyo hakubaliki.

Chanzo chetu kilidokeza kwamba tathmini hiyo ilionyesha kuwa kada huyo hakubaliki sana katika mikoa ya Lindi , Mtwara pamoja na maeneo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, ukiwemo Mkoa wa Mara.

Kutokana na hali hiyo, ilikubaliwa kuwa fedha nyingi zitumike na watu mahiri wenye ushawishi, watumwe katika maeneo haya ili kuwalainisha baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanaonekana kuwa mbali na mgombea huyo, na jambo hilo lifanyike haraka kabla ya kuanza kwa chaguzi mbalimbali ndani ya CCM mwaka huu.

Kauli ya Nape
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipoliuzwa kuhusiana na kikao hicho, alisema hana taarifa zozote lakini alionya kuwa endapo itathibitika kuwa kuna makada wa chama hicho wanafanya ‘rafu’ hizo, watachukuliwa hatua za kisheria za chama kwani huu si muda wa kufanya kampeni za urais.

Aliwataka wanachama wa CCM kuipa nafasi  Serikali yao kutekeleza majukumu yake na ilani kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.Awali, pia Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, aliwahi kukaririwa akisema kuwa wanaotarajia kutumia fedha kupata urais kupitia chama hicho wanajidaganya, ni bora watafute kazi nyingine za kufanya.


 Kikao cha mkakati
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho, zililidokeza Mwananchi Jumapili  kuwa makada watakaotumwa kuzunguka mikoani, baada kukamilisha kazi yao, watatakiwa  kurejesha ripoti itakayofanyiwa kazi, ili kundi hilo liweke mikakati zaidi ya kufanikisha lengo lake.

Inaelezwa kuwa hofu kuu ya kundi hilo, ni kutoka kwa baadhi ya makada wengine wa CCM, wanaotajwa kuonyesha nia ya kuwania nafasi ya urais, kukubalika zaidi ndani ya chama katika mikoa hiyo, ambapo baadhi yao  wanatoka huko.
Chanzo chetu kilidokeza pia kuwa mbali ya kuweka mikakati hiyo kabambe ya kuwania urais, pia wajumbe wa kikao hicho ‘kizito’, walifanyiwa sherehe kubwa ambapo nyama na vinywaji mbalimbali vilimwagwa kwa wingi, ndani ya majengo ya mfanyabiashara huyo, ambayo yamezungushiwa ukuta mrefu.

“Aisee! kikao kilikuwa kizito mno mikakati mizito imewekwa , jamaa yuko serious (makini) kuutaka urais, “alidokeza kada mmoja aliyekuwa ndani ya kikao hicho kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa tayari, makada waliotumwa kwenda mikoani ‘kumnyoshea njia’ mgombea huyo wa urais, hivi sasa wanavinjari kwenye maeneo hayo, wakiwa na fedha za kutosha na vitendea kazi vingine, yakiwemo magari ya uhakika.

Waliotumwa kufanya kazi hiyo, ni wenyeviti  wa baadhi ya mikoa ambao imeelezwa kuwa watatumia nafasi zao kufanya ushawishi huo kwa urahisi.

Ingawa hadi sasa hakuna kada ndani ya CCM ambaye ametangaza hadharani  kutaka kuwania urais, inadaiwa kwamba kuna kundi kubwa la watu ambao tayari wanapigana vikumbo chini chini kutaka nafasi hiyo, kutokana na Rais wa sasa Jakaya Kikwete, kufikia ukomo wake kikatiba mwaka 2015.

Hatua hiyo imedaiwa kuibua makundi yanayosabisha nyufa zinazoweza kuleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho.
Tayari CCM kimekiri kupitia Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama kuwa harakati za kuwania urais ndani ya chama hicho, zinakivuruga.

Taarifa ya Kamati Kuu ya CCM iliyosomwa ndani ya Kikao cha Halmashuari Kuu (NEC) ya CCM mjini Dodoma Novemba mwaka jana ,pamoja na mambo mengine, ilikiri kuwa mbio za kuwania urais mwaka 2015 ndani ya chama hicho, ndicho kiini kikuu cha mgawanyiko.

Kamati Kuu ilionya kuwa wanaotaka kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho, wanapaswa kudhibitiwa na kwamba matumizi ya fedha katika kampeni hayatakubalika.

Ushauri wa Kinana
Alhamisi wiki hii, Mjumbe wa Kamati Kuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa na gazeti la Mwananchi akieleza kuwa vigogo wa chama hicho walioanza kampeni za urais, sasa wanavuruga  utendaji wa Serikali ya Rais Kikwete.
Akiwa kwenye ziara ya kutembelea matawi ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kinana alisema vigogo hao ni wabinafsi, wanaivuruga nchi na hawana lolote wanalolifanya kwa maslahi ya chama hicho tawala.

Kinana ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kampeni za Rais Jakaya Kikwete wakati akigombea urais kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alionesha kukerwa na watu hao na kueleza kuwa si sahihi kuanza kuzungumza masuala ya urais sasa wakati Rais Kikwete bado ana miaka minne ya kutekeleza Ilani ya chama hicho.

“Sasa hivi Rais Kikwete ana miaka mingine minne mbele kabla ya kumaliza uongozi wake na CCM ina kero nyingi za kushughulikia ili kutekeleza ilani yake, halafu wengine wanazungumzia urais sasa,” alikaririwa akisema Kinana.
Alisema anasikitishwa na hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wanaoanza kupiga kampeni za urais ni watu wazito ndani ya nchi na ni wajumbe wa vikao vikuu ndani ya CCM.

Tishio lingine
Mbali ya chama hicho kukabiliwa na tishio la mgawanyiko kutokana na urais wa 2015, pia kinakabiliwa na kazi ngumu ya utekelezaji wa mkakati wake, kuwavua gamba baadhi ya makada wake wanaohusishwa na kashfa za ufisadi.

Kikao kilichopita cha NEC ambacho kilitarajiwa kuchukua maamuzi magumu ya kuwavua gamba wanachama hao, kilishindwa kufanya hivyo,  badala yake kikatoa muda kwa wanachama  hao kujitathmini wenyewe na kuchukua uamuzi kabla ya CCM kuwachukulia hatua.

Madaktari wawagomea mawaziri mkutanoni

SAKATA la madaktari nchini linazidi kuchukua sura mpya baada ya wataalamu hao kukataa hoja za ujumbe wa Serikali ulioongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi, Hawa Ghasia huku wakigoma kusikiliza kauli yoyote kutoka kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Hadji Mponda

Wakati mawaziri hao wakikumbwa ana tafrani hiyo tayari wauguzi katika Hospitali  ya Taifa Muhimbili (MNH) na ile ya Mkoa wa Dodoma wametishia kusitisha utoaji huduma ifikapo Jumatatu kama masuala yao hayajapatiwa ufumbuzi.

Vigogo wa Serikali waliofika kukutana na madaktari hao jana ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya,  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
Tukio hilo lilitokea jana kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Star Light, Jijini Dar es Salaam ambako madaktari hao walikusanyika na baadaye kupewa taarifa kuwa kuna ujumbe wa Serikali utafika kwa majadiliano.  Madaktari hao waliwatimua ujumbe huo baada ya kuusikiliza juu ya wito wao wa kuwataka wasitishe mgomo ili wafungue ukurasa wa majadiliano, wakajibiwa kuwa kwa sasa ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo na siyo ahadi. 

Ujumbe huo wa Serikali uliwasili ukumbini hapo majira ya mchana na kukaribishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka ambaye baada ya kuwawekea viti pembeni mwa jukwaa kuu, aliwatambulisha kwa washiriki.   “Ugeni tuliokuwa tunasubiri umefika, si rahisi sisi wote kuwafahamu ni vema wangejitambulisha wao kwa majina kisha tuendelee na utaratibu tuliojiwekea,” alisema Dk Ulimboka.

Mara baada ya kauli hiyo, wageni hao walianza kujitambulisha. Wa kwanza alikuwa Waziri  Ghasia aliyewasalimia madaktari hao na kujitambulisha kisha kueleza kuwa aliongoza ujumbe huo kuwasilisha taarifa ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.  Dalili mbaya kwa ujumbe huo, zilianza kujitokeza walipoitika kwa nguvu salamu ya Waziri Ghasia huku wakiwanyamazia Waziri wa Afya na maofisa waandamizi wa wizara hiyo.

Baada ya tukio hilo kumalizika, Dk Ulimboka alitoa taratibu za mkutano kuwa ni kusoma taarifa maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kupelekwa kwa Waziri Mkuu.  “Sisi hapa tutawakabidhi taarifa iliyoandaliwa na madaktari ambayo ni maalumu kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baada ya kuwasomea, tutawakabidhi kisha tusubiri majibu ya taarifa yetu tukiwa hapahapa,” alisema Dk Ulimboka.

Dk Ulimboka alisoma taarifa hiyo mbele ya wageni hao ambayo ilitaja madai yao kadhaa ikiwemo kumtaka Waziri Ghasia  kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwaondoa katika wizara hiyo, Waziri Mponda na naibu wake Dk Nkya, Katibu Nyoni na Mganga Mkuu, Dk Mtasiwa.

Mara baada ya kusoma taarifa hiyo alikabidhi barua hiyo  kwa Waziri Ghasia huku akisisitiza kuwa wataendelea na mgomo hadi watakapopatiwa majibu ya hoja zao.

 “Tunaomba taarifa hiyo imfikie haraka Waziri Mkuu,  ijadiliwe kwa haraka na kutoa majibu yatakayotupatia ufumbuzi ili nasi  turudi kazini tukaokoe maisha ya Watanzania,” alisema Dk Ulimboka ambaye kwa kauli yake iliashiria kufunga mjadala.

Baada ya kauli hiyo, Waziri  Ghasia alisimama na kueleza kuwa wao walifika wakiwa na ujumbe toka kwa Waziri Mkuu hivyo ni vema wangekubaliwa wauwasilishe ambapo alimtaja Waziri wa Afya Dk Mponda kuwa angeusoma.
Dk Ulimboka alijibu hoja hiyo akisema  “Madaktari hatuna tatizo na ujumbe toka kwa waziri Mkuu Mizengo Pinda ila ujumbe kutolewa na Waziri wa Afya Dk Hadji Mponda hatukubali kwasababu hatuna imani naye labda kama kweli ni taarifa, ungesoma wewe,” alisema Dk Ulimboka na kukaa chini.

Waziri Ghasia alikubaliana na hoja hiyo na katika kuwasilisha taarifa hiyo, alisema alisononeshwa kusoma majibu yanayohusu madai ya madaktari hao kwa niaba ya waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Afya wakati yeye (Dk Mponda) akiwepo.

Ghasia alisema wizara imetafakari kwa kina suala la madaktari waliokuwa kwenye mafunzo katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili na kuwarudisha kwenye kituo hicho cha kazi huku ikiahadi kuwalipa stahili zao.
“Wazira imetafakari kwa kina na imeamua kuwarejesha madaktari wote waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili na wanatakiwa kuripoti katika vituo hivyo vya kazi kuanzia Jumatatu,” alisema Ghasia.

Kuhusu madai mengine, alisema Serikali itaendelea na majadiliano ya pamoja  huku akiwaomba warejee kazini.
“Sisi tuwaombe tu kwamba madai yenu yote Serikali inayafanyia kazi. Suala la nyumba tayari tumeshapata fedha kutoka Global Fund kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za madaktari ili waweze kukaa karibu na vituo vyao vya kazi,” alisema Ghasia.  Akijibu ombi la kuwataka warejee kazini, Dk Ulimboka alisema hilo litategemea majibu ya taarifa walioiwasilisha kwa Waziri Mkuu, ambapo alisisitiza kuwa wao wataendelea na mikutano katika ukumbi huo.

“Sisi tutaendelea na mikutano kujadili taarifa yenu na pia tungeshauri taarifa hii mtuletee kwa maandishi, lakini pia tunasubiri majibu ya taarifa yetu tuliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambayo tumeitoa kwa maandishi,” alisema Dk Ulimboka.  Dk Uliomboa aliwataka wawakilishi hao wa Serikali kutambua kuwa  ujumbe haukuwa wa kushawishiana kurudi kazini bali ni wa kupeana taarifa.

Kauli hiyo iliashiria kwamba hoja ya ujumbe huo haina uzito wa kuwashawishi kuacha mgomo huku wakikataa hoja zao sasa kujadiliwa na wizara badala yake walisisitiza Waziri Mkuu kushughulikia suala hilo.    Walimtaka Waziri Mkuu, kutoa majibu ya madai yao kwa wakati ili asiwafanye kufikia hatua ya kusitisha huduma katika vitengo vya dhararu.

  “Mgomo huu unaendelea nchi nzima hadi majibu ya madai yetu tuliyowasilisha kwa  Waziri Mkuu yamepatiwa majibu.
Tunashauri kazi hiyo ifanywe haraka vinginevyo tusije tukashawishika kusitisha huduma kwenye vitengo vya dharura,” alisema Ulimboka.

 Tishio la mgomo zaidi
Wakati huo huo, Chama cha Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kimesema kuwa wauguzi wataendelea kutoa huduma kwa kusuasua hadi Jumatatu  na kama suala hilo litakuwa halijapatiwa ufumbuzi,  watasitisha huduma na kufunga hospitali.

“Sisi tutaendelea kutoa huduma katika mazingira ya shida  hivi mpaka Jumatatu tu,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Paul Magesa.

Habari kutoka katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma zilieleza pia kuwa, kwa sasa hakuna wagonjwa wapya wanaopokelewa  na kuwa waliopo wodini wakitoka, hospitali hiyo nayo itasitisha kutoa huduma.   MWISHO

Kizaazaa cha Mchina cha leta mushikeli bongo



Na Mwandishi wetu
Dawa za Kichina za kuongeza makalio zimeleta kizaazaa cha aina yake kufuatia baadhi ya wanawake waliozitumia kwa lengo la ‘kuwachanganya’ wanaume kukiona cha mtemakuni.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, baadhi ya wanawake hao wakiwemo mastaa wa Bongo sasa wanahaha kutafuta njia za kupunguza miili yao baada ya kubaini uamuzi waliochukua awali haukuwa sahihi.
Imebainika kuwa, kufuatia matumizi ya dawa hizo wapo ambao sasa hawatamaniki kutokana na kuwa na maumbile ‘kichekesho’ hivyo kukosa ule mvuto waliotarajia.
Akizungumza kwa masikitiko, mwanamke mmoja aliyeonekana kuathirika na dawa hizo aitwaye Zaina wa Kinondoni, Dar alisema, awali alidhani kuwa na makalio makubwa kungesaidia kumdatisha mumewe lakini kumbe ndiyo alikuwa anatafuta matatizo.
“Nilikuwa na umbo langu zuri tu, wenyewe wanaita namba nane lakini shoga yangu akanishawishi nitumie dawa hizo akidai eti nitakuwa na kalio litakalomdatisha mume wangu, kumbe ndo’ kaniingiza mkenge.
“Ona nilivyo, kwa kweli najuta kutumia dawa hizi, hapa nilipo nimeambiwa kuna dawa inaitwa Mlonge inayotibu magonjwa mbalimbali, ndio naisaka ili niondokane na hali hii,” alisema mama huyo.
Naye Husna wa Magomeni aliliambia Risasi Jumamosi kuwa, yeye alikuwa akitamani kuwa na kalio kubwa na akashauriwa na marafiki zake atumie dawa hizo za Kichina lakini kwa anachokiona kwa dada yake, hataki kabisa kuzisikia.
“Dada yangu hatamaniki kwa dawa hizo. Alikuwa na umbo zuri lakini baada ya kuzitumia, amekuwa kituko na kila alipopita amekuwa akipata usumbufu kutoka kwa wanaume,” alisema Husna na kuongeza:
“Mbaya zaidi kumbe mume wake alikuwa hapendi mwanamke mwenye wowowo, sasa hivi hakuna maelewano ndani ya ndoa na mume wake amekuwa akimsaliti kwa kwenda kutafuta dogodogo nje, mimi sitaki kuingia huko.”
Tabia ya baadhi ya wanawake kutumia dawa za kuongeza makalio kama wanavyoonekana wanawake walio ukurasa wa mbele imekuwa ikiwaletea matatizo ikiwa ni pamoja na wengine kushindwa kuwajibika vilivyo wawapo faragha na wapenzi wao na kuzomewa wanapokatiza mitaani.
Gazeti hili linawashauri wanawake kukubaliana na maumbile waliyopewa na Mungu kwani kutafuta muonekano mpya kwa kutumia dawa hizo na nyinginezo ni kujitafutia madhara yanayoweza kuathiri maisha yao.

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AMALIZIA ZIARA YA MKOA WA TANGA, WILAYANI LUSHOTO





 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa mkulima wa Nyanya, Judith Munis, wa Kikundi cha Upendo Jegestal, kuhusu kilimo cha nyanya, wakati alipotembelea wakulima wa Kituo cha Habari na Mafunzo (Shamba Darasa) cha Jegestal-Lushoto, juzi Januari 27, 2012, akiwa katika ziara yake ya mkoa wa Tanga.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiangalia chupa ya Juisi iliyotengenezwa na wajasiliamali, Salome Mtawa (kulia) wa kikundi cha Usambara Lishe Trust,  wakati alipotembelea wakulima wa Kituo cha Habari na Mafunzo (Shamba Darasa) cha Jegestal-Lushoto, juzi Januari 27, 2012, akiwa katika ziara yake ya mkoa wa Tanga.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akikagua jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto baada ya kuweka jiwe la Msingi katika jengo hilo lililopo Chakechake Lushoto juzi Januari 27, 2012, wakati akiwa katika ziara yake ya mkoa wa Tanga. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Sophia Mjema.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwasalimia na kuwaaga wasanii waliokuwa wakitoa burudani, wakati akiondoka Chakechake baada ya kuweka jiwe la Msingi katika Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, juzi Januari 27, 2012, wakati akiwa katika ziara yake ya mkoa wa Tanga.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa wakulima wa mbogamboga, Juma Kambaga, kuhusu uzalishwaji wa mbogamboga hizo wakati alipotembelea wakulima wa Kituo cha Habari na Mafunzo (Shamba Darasa) cha Jegestal-Lushoto, juzi Januari 27, 2012, akiwa katika ziara yake ya mkoa wa Tanga. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Galawa.


Saturday, January 28, 2012

Asitisha bunge aungana na madactari Mnyika



 
Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), Mhe. John Mnyika.
Mgomo wa madaktari unaoendelea hivi sasa umedhihirisha kwamba tuna serikali dhaifu yenye ombwe la uongozi. Haiwezekani wananchi wakawa wanakufa kwa kukosa matibabu stahiki na wengine wakipata madhara kutokana na kuchelewa kupata matibabu sababu ya mgomo wa madaktari halafu viongozi wenye dhamana hawachukui hatua sahihi.
Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye mwenye dhamana kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 33 ndiye kiongozi wa shughuli za serikali na ibara ya 35 shughuli zote za utendaji wa serikali zinatekelezwa na watumishi wa serikali kwa niaba ya Rais; ameondoka kwenda nje ya nchi mgomo ulipoanza na hakuna kauli yoyote mpaka sasa toka kwa Makamu wa Rais wala kwa Ikulu.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda badala ya kwenda kwenye eneo la mgomo na kuzungumza na madaktari naye ameishia kuzungumza na vyombo vya habari. Waziri wa Afya Dk. Haji Mponda na Naibu Waziri Dk. Lucy Nkya nao jana wamezungumza na waandishi wa habari badala ya kwenda kukutana na madaktari na kuzungumza nao kuhusu madai yao ya msingi.

Kwa upande wetu CHADEMA tulitoa kauli tarehe 25 Januari 2012 ya kutaka serikali ichukue hatua na tuliona tuipe serikali nafasi ifanye kazi yake hata hivyo serikali haionyeshi kuupa uzito unaostahili mgogoro huu wenye kuathiri hali za wagonjwa na maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Tuliacha kwenda katika eneo la mgomo kukutana na madaktari katika siku za awali kuepusha suala hili kutafsiriwa kuwa ni la kisiasa. Hata hivyo, kuchelewa kwa serikali kukutana na madaktari kunahitaji hatua za pamoja. Dhamira yangu kama mwananchi, mbunge katika mkoa wa Dar es Salaam na kiongozi wa chama cha siasa naumizwa na hali inayoendelea. Ni vigumu kuweza kuendelea na majukumu ya kibunge na ya kichama katika masuala mengine wakati serikali iko legelege katika suala ambalo linahusu uhai wa wananchi wenzangu uko mashakani.

Hivyo nawajibika siku ya leo kuelekeza nguvu katika kuungana mkono na madaktari katika madai yao ili kuishinikiza serikali kuweza kutuma ujumbe mkubwa kukutana na madaktari leo au kesho. Na iwapo serikali haitakutana nao katika muda huo, itabidi uongozi wa kambi ya upinzani bungeni ukiwa ni serikali kivuli na uongozi mkuu wa CHADEMA ukiwa ni chama mbadala kuweza kukutana nao.

Natambua kwamba uzembe na ufisadi katika serikali kwenye sekta ya afya unaligharimu taifa na maisha ya wananchi. Hivyo, CHADEMA inaitaka serikali kukamilisha kwa haraka majadiliano na madaktari na kutimiza madai yao ili kuepusha madhara zaidi kwa umma.

Nawapa pole wananchi ambao wameathirika na migomo inayoendelea na kuzingatia kwamba mgomo huo umesababishwa na udhaifu katika serikali.

Natoa mwito kwa umma wa watanzania kuwaunga mkono madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya katika hospitali na zahanati za umma kama sehemu ya kuboresha huduma katika maeneo husika.

Madai ya madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya nchini yasiposhughulikiwa kwa wakati na kwa ukamilifu watumishi husika wanaweza wasiwe kwenye mgomo wa wazi kama ilivyo kwa baadhi ya hospitali na zahanati nchini lakini wataendelea na migomo baridi kwa kutoa huduma mbovu au kuacha kazi kwenye maeneo ya umma na wengine kwenda kufanya kazi nje ya nchi wakati kukiwa na uhaba wa watumishi nchini.

Aidha, pamoja na migomo inayoendelea, naendelea kutoa rai kwa madaktari na watumishi wengine wa umma kuhakikisha maisha ya wagonjwa walio katika hali ya hatari yanaokolewa.

Nimezungumza na viongozi wetu wakuu kuhusu suala hili na natoa mwito kwa wadau wote kuunganisha nguvu katika kuisimamia serikali kushughulikia madai ya madaktari na wafanyakazi wengine wa sekta ya afya kwa haraka ili kuepusha madhara zaidi kwa umma.

Wananchi wenzangu wa Jimbo la Ubungo na umma kwa ujumla uzingatie kwamba tangu Mwalimu Nyerere aondoke madarakani mwaka 1985, Serikali ya CCM imeongeza wingi wa majengo mbalimbali kwenye sekta ya afya hata hivyo imeshindwa kusimamia utoaji bora wa huduma za afya katika zahanati, hospitali na vituo vya afya. Kutokana na mfumo mbaya wa usimamizi wa sekta ya afya, misingi imara ya kuimarisha sekta ya afya iliyowekwa baada ya uhuru imevunjwa na kubomolewa ikiwemo katika masuala yanayohusu kujali maslahi ya watumishi wa umma katika sekta hii muhimu.

Hali hii imefanya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa na nakisi ya watumishi asilimia 48% na takwimu zinaonesha kuwa 18% ya wafamasia, 15% ya madaktari, 13% ya madaktari wasaidizi waliacha vituo vyao vya kazi na kwenda kutafuta kazi kwenye mashirika ambayo yanalipa mishahara mikubwa na mizuri. Nakisi hii itaongezeka zaidi iwapo madai ya msingi ya madaktari na watumishi wengine hayatashughulikiwa na serikali itaendelea kuchelewa kushughulikia migogoro na migomo mingine inayoendelea.

Ni imani yangu kwamba serikali ikiwa na dhamira inaweza kuongeza mishahara kwa watumishi wa sekta ya afya ili kuweza kuwavutia wataalamu kubakia nchini badala ya kwenda kugoma au kwenda kutafuta kazi nje ya nchi kutokana na malipo mazuri huko. Hii ni pamoja kuwezesha malipo ya mazingira magumu kutolewa kwa watumishi wa afya wanaofanya kazi katika maeneo na kada maalum.

Kwa sababu hii, leo sitashiriki kikao cha Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kinachoendelea ili kupata wasaa wa kufuatilia kwa karibu suala hili na kuwasiliana na viongozi wenzangu kwa ajili ya hatua zaidi za pamoja.


Majambazi wapanga mawe barabarani kupola

 
Niliondoka Singida Mjini saa kumi na moja alfajiri kuelekea Dodoma. Kilomita 40 kutoka Manyoni nilikutana na hali hiyo pichani kunako saa kumi na mbili na nusu. Eneo la tukio niliwakuta askari watano wamevalia kiraia wakiwa na silaha za moto. Wameniambia tukio limetokea usiku wa kuamkia leo majira ya kuanzia saa sita usiku na linawahusisha maja majambazi wasiopungua wanane.

Kuna walioporwa fedha, simu na mali zao . Mahali hapa kuna pori kubwa upande wa kushoto. Inaaminika majambazi hayo yenye silaha yangali  yamejiicha porini.
Hakuna aliyekamatwa. Nilishuhudia polisi hao wakifuatilia nyayo huku wakinionyesha mahali majambazi hayo yalilala  chini kujificha wakisubiri giza na kuanza kupanga mawe yao. Kwa kusoma mazingira ya eneo kwangu mimi napata tafsiri kuwa majambazi hayo yalifanya maandzi ya mpango wao  kwa siku kadhaa.

Maana, mawe hayo mazito yanaonekana kuwa yalikuwa yakisogezwa usiku karibu na tukio na kufikia idadi waliyohitaji. Intelijensia ya kipolisi ingefanya kazi  yake sawa sawa na kwa kushirikiana na wenyeji ingewezeza kubaini mapema movement  ya mawe yale. Na katika dunia ya sasa , mbwa wa polisi waliopewa mafunzo wangefanya kwa haraka na kwa ufanisi zoezi la kufuatilia majambazi porini badala ya polisi kufuatilia nyayo kwa macho. 
 

Mwakyembe aweka wazi yanayomsibu

•  Achoshwa na maswali ya afya yake

 


   AFYA ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, ni tete baada ya kuugua ugonjwa uliomsababisha kuvimba mwili wote.Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na yeye mwenyewe zinaeleza kuwa, alianza kuwashwa ngozi miezi mitatu iliyopita kabla ya hali kubadilika siku za karibuni na hatimaye kuvimba sehemu kubwa ya mwili wake.

HATIMAYE Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameamua kuzungumzia ugonjwa unaomsumbua kwa muda mrefu sasa.
Akizungumza  jana kwa njia ya simu, Dk. Mwakyembe alisema wiki ijayo anatarajia kuzungumzia ugonjwa huo ambao baadhi ya watu wamekuwa wakiuhusisha na kulishwa sumu.
Miongoni mwa watu wanaodai kuwa Dk. Mwakyembe kalishwa sumu ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye mara kwa mara amekuwa akiwatuhumu watu anaowaita mafisadi kushiriki katika uovu huo.
Sitta amenukuliwa akisema pamoja na kutoa madai hayo jeshi la polisi halijayatilia uzito zaidi ya kumhoji yeye na Dk. Mwakyembe.
Katika mazungumzo yake jana na gazeti hili, Dk. Mwakyembe ambaye alirejea nchini mwishoni mwaka jana akitokea India kwa matibabu, alisema kwa siku mbili hizi hawezi kuzungumzia hali yake na kilichomsibu.
“Kwa sasa waulize madaktari kuhusu hali ya ugonjwa wangu, mimi nitafute wiki ijayo tuzungumze,” alisema Mwakyembe bila kubainisha ni siku gani hasa.
Juzi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipozungumza na waandishi wa habari alisema kuwa serikali haiko tayari kuzungumzia ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe, kwani ni kinyume cha maadili ya utabibu.
Pinda alisema hata kama anafahamu ugonjwa unaomsumbua hawezi kuuzungumzia na badala yake mwenye wajibu wa kufanya hivyo ni Dk. Mwakyembe mwenyewe.
Wakati Pinda akitoa kauli hiyo, serikali ilishawahi kutoa taarifa ya magonjwa yaliyowasumbua baadhi ya viongozi waliopata kutibiwa nje ya nchi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete.
Kwa muda mrefu Dk. Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa ambao hadi sasa haujawekwa wazi jambo linalowafanya baadhi ya wananchi wapate wasiwasi kuhusu usalama wa viongozi wa serikali.
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa madaktari waliomtibu katika Hospitali ya Apollo nchini India waliandika ripoti inayohusu ugonjwa wake ambayo inasemekana imekabidhiwa serikalini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowahi kuandikwa na gazeti hili kutoka kwa baadhi ya watu walio karibu na kiongozi huyo ni kuwa hali yake si nzuri na hatoweza kurejea katika shughuli zake za kawaida katika kipindi kifupi kijacho.
Watu hao walidokeza kuwa Naibu Waziri huyo amenyonyoka nywele, kope na vinyweleo huku ngozi ikiwa imeharibika.
Kabla ya Dk. Mwakyembe kuanza kuugua na hatimaye kupelekwa India alitoa taarifa kwa jeshi la polisi juu ya njama za baadhi ya watu kutaka kumuua.
Baada ya madai hayo Dk. Mwakyembe aliitwa polisi kutoa maelezo juu ya tuhuma hizo lakini mpaka sasa jeshi hilo halijaeleza hatua ilizozichukua dhidi ya watu waliotajwa kuhusika na njama hizo

                                                  

Pinda alikoroga posho za wabunge

WANANCHI, wanasiasa na wanaharakati wamemjia juu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu kauli yake ya kuhalalisha nyongeza ya posho za wabunge.
Wakizungumza na mwanahabari wetu, jana jijini Dar es Salaam walisema kiongozi huyo ameonyesha namna viongozi walivyoweka mbele maslahi binafsi hasa linapofika suala la fedha.
Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari juzi, Pinda alitetea posho za wabunge akisema kiasi wanachokipata ni kidogo na wengi wao mwisho wa mwezi hawabaki na kitu, kwani fedha zote za mishahara hukatwa kulipia madeni waliyoingia kwa ajili ya kusaidia majimbo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema Pinda atakuwa Waziri Mkuu wa kwanza kuwapotosha Watanzania kuhusu posho.
Alisema posho wanayopewa wabunge ni kwa ajili ya matumizi yao na si kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
“Nimekuwa mbunge kwa miaka 15 sijawahi kutoa fedha mfukoni mwangu kwa ajili ya kumhudumia Mtanzania mmojammoja kama nitatoa ni kwa hiyari yangu.
“Si kweli kwamba mbunge anaishiwa fedha zake zote kwa ajili ya kumhudumia Mtanzania, kwani Watanzania wanao mfuko wao wa maendeleo ambao wabunge hukaa na wananchi kujadili fedha hizo zitumikaje,” alisema Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa Slaa, Pinda alipaswa kuzungumza juu ya ugumu wa maisha ya Watanzania yalivyo sasa na namna ya kuwasaidia na si kuzungumzia wabunge peke yao kwa kuwa wao hawana shinda kama ilivyo kwa Mtanzania wa kawaida.
Akitolea mfano, alisema Pinda alipaswa kuangalia makundi yanayolalamika kuhusu malipo yao kama ilivyo kwa madaktari hivi sasa, kuliko kuchukua jukumu la kuwapotosha Watanzania.
“Kila siku ninasema serikali ya CCM imeshindwa kutafuta njia sahihi ya kupunguza ugumu wa maisha kwa Watanzania badala yake inatumia ujanja ujanja kuonyesha kwamba inashughulikia matatizo yao wakati si kweli,” alisema.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbarara Maharagande, alisema suala la nyongeza za posho za wabunge si la kuzungumza kwa wakati huu ambapo maisha ya Watanzania yamegubikwa na mfumko wa kutisha wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.
Alisema CUF wanahitaji mfumo wa kisiasa ambao utazaa mfumo mzuri wa kiuchumi utakaowatoa Watanzania kwenye maisha magumu.
Alisema posho ya sh 200,000 kwa siku inayotolewa kwa wabunge 328 ni sawa na sh mil. 65.6 ambazo serikali hutoa kwa siku.
Maharagande alisema fedha hizo ni nyingi na kama zingetumika ipasavyo zingeweza kufanya jambo kubwa la maendeleo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Kijinsia (TGNP) Usu Marya alishangaa serikali na wabunge kushindwa kutambua wajibu wao.
“Sisi kama wanaharakati tunaona kuna tatizo la msingi la dhana nzima ya uwajibikaji, serikali inashindwa kutambua majukumu yake na Bunge pia,” alisema.
Alisema mbunge hapaswi kutoa fedha zake mfukoni kwa ajili ya kusaidia jimbo inayopaswa kufanya hivyo ni serikali na wabunge kazi yao ni kusimamia wajibu huo wa serikali.
“Si kazi ya wabunge kutoa fedha mfukoni kusaidia watu, serikali inapewa dhamana ya kusaidia watu kwa kutoa huduma kwa wananchi kutokana na kodi inazozikusanya…sisi wanaharakati tunaipinga; inakwenda kinyume kabisa, inakuwa kama wabunge wanaihonga serikali.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe aliyebobea katika masuala ya uchumi, Prosper Ngowi, amesema Pinda anatakiwa kuelewa kuwa maisha magumu si kwa wabunge peke yake bali ni kwa Watanzania wote.
Alisema alichotakiwa kuzungumza Pinda katika hotuba yake ni kueleza namna serikali itakavyoweza kuwapunguzia ugumu wa maisha Watanzania.
Aliongeza maisha yaliyopanda si katika mkoa wa Dodoma kama wanavyodai wabunge bali ni nchi nzima na hasa watu wenye vipato vya chini.
Mkazi wa mkoa wa Kagera, Yohana Kazimoto, ambaye alipiga simu chumba cha habari cha Tanzania Daima, alisema viongozi wengi wamesahau kutetea maslahi ya wananchi badala yake wanaangalia yanayowahusu.
Naye mkazi wa Yombo Vituka jijini Dar es salaam, Ester Barimi, alisema kama viongozi wa serikali wameamua kujilimbikizia posho, wafanye hivyo pia katika sekta nyingine zikiwemo za afya, elimu na kilimo

Makamba ataka mikataba ya wachimba Uranium

KAMATI ya Bunge ya Nishati na Madini, imeitaka Wizara ya Nishati na Madini, kuwasilisha mikataba ya kampuni za Mantra na Urinex, zinazojihusisha na uchimbaji wa madini ya Uraniam, ili kuliwezesha Bunge kujiridhisha juu uhalali wao  katika kufanya shughuli hizo.

Hayo yalisemwa  na Mwenyekiti wa kamati hiyo, January Makamba, ambaye alisema hatua hiyo inatokana na umuhimu wa madini yenyewe katika dunia ya sasa.

Alisema kukaguliwa kwa mikabata hiyo, kutasaidia kubaini uhalali na uwezo wa kampuni hizo katika kufanya shughuli hizo.


“Kuna kampuni mbili za uchimbaji wa madini ya Uranium hapa nchini, lakini hadi sasa mikabata yake hatujaiona, kwa hiyo  tumeitaka wizara kuwasilisha mikataba hiyo kwenye kikao kijacho cha Bunge ili tuweze kuikagua,”alisema Makamba.

Alisema Kampuni ya Urinex  inachimba madini hayo katika maeneo ya Manyoni, mkoani Singida na Bahi huko Dodoma wakati Kampuni ya Mantra,  inachimba Uranium  katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Alisema Serikali kupitia kamati hiyo inapaswa kuhakikisha kuwa madini yanawanufaisha wananchi kuiwezesha nchi kujiingizia mapato.

Alisema madini hayo  yanahitajika sana duniani katika shughuli mbalimbali  na kwamba kwa msingi huo kama lazima ijue mikabata yote inayohusu uchimbaji wa Uranium.

Alisema kutowasilishwa kwa mikataba ya kampuni hizo, kumeifanya kama yake, kushindwa kujadili suala lolote kuhusu kampuni hizo.

Friday, January 27, 2012

Kinana: Wanaotaka urais 2015 wamvuruga Kikwete


ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Kampeni za Rais Jakaya Kikwete wakati akigombea urais kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Abdulrahman Kinana, amesema vigogo wa chama hicho walioanza kampeni za urais sasa wanavuruga utendaji wa serikali.Akizungumza jana katika ziara yake ya kutembelea matawi ya CCM mkoa wa Dar es Salaam,  Kinana alisema vigogo hao ni wabinafsi, wanaivuruga nchi na hawana lolote wanalolifanya kwa maslahi ya chama hicho tawala.
“Sasa hivi Rais Kikwete ana miaka mingine minne mbele kabla ya kumaliza uongozi wake na CCM ina kero nyingi za kushughulikia ili kutekeleza ilani yake, halafu wengine wanazungumzia urais sasa," alisema Kinana
Kinana alizitaja kero hizo kuwa ni elimu, afya, maji, barabara, mazingira, maisha magumu yanayosababishwa na mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani shilingi.

Kauli hiyo ya Kinana ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, imekuja katika kipindi ambacho baadhi vigogo wa CCM wamekuwa wakipigana vikumbo kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi, huku wakitumia majukwaa mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, makanisa na misikiti kujipigia kampeni.

Akizungumzia harakati za vigogo hao kugombea Urais ndani ya CCM Kinana alisema; “Wote wanaozungumza kwenye vyombo vya habari, hawasemi kwa manufaa  ya wananchi wala maslahi ya wanachama bali  kwa maslahi yao binafsi.”
Alifafanua kwamba, masuala ya kuutaka urais siyo ya kuzungumzia sasa kwani bado Rais Kikwete ana miaka minne ya kuwa madarakani huku akikabiliwa na kazi kubwa ya kutatua matatizo ya wananchi katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na hali mbaya kiuchumi.

 “Je, huu kweli ni wakati wa kuyazungumzia hayo? (masuala ya kuwania urais)," alihoji Kinana.
Kinana alitahadharisha kuwa mazingira wanayoyajenga vigogo hao yatawafanya wanachama na wananchi kwa ujumla, wawachukie utakapowadia wakati wa uchaguzi mwingine.

Alisema anasikitishwa na hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wanaoanza kupiga kampeni za urais ni watu wazito ndani ya nchi na ni wajumbe wa vikao vikuu ndani ya CCM, lakini wanaona kusema kupitia vyombo vya habari watasikika nchi nzima.

“Hao mnaowasikia wakisema kwenye vyombo vya habari ni wajumbe wa vikao tena vikubwa na hakuna anayewazuia. Wanaona wakisema kwenye vikao, wananchi hawatasikia,” alifafanua.

Kinana alisema hayo akijibu swali aliloulizwa na mmoja wa wanachama wa CCM tawi la Buguruni, aliyetaka kujua kwa nini vigogo wa chama hawaonyeshi mshikamano kwa kutotumia vikao vya chama kujali masuala mazito kama hayo, badala yake wanakwenda kwenye vyombo vya habari?

“Viongozi wa juu muwe na mshikamano, nendeni kwenye vikao, mna vikao vya kusemea, acheni kusema kwenye vyombo vya habari,” alionya Kinana

Kinana aliwahakikishia wana CCM mkoa wa Dar es Salaam kwamba, suala hilo atalifikisha kwenye chama ili lifanyiwe kazi kulingana na taratibu zake.
Katiba mpya
Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba, Kinana alisema Rais Kikwete amekuwa akifanya kazi yake vizuri ikiwemo kuwashirikisha wadau mbalimbali kuhusu jambo hilo na amekuwa akikutana nao Ikulu ili  kujenga amani na utulivu nchini.

Aliwataja wadau hao kuwa ni pamoja viongozi wa vyama vya upinzani.
Alisema Rais ni kiongozi wa nchi na anatumia nafasi hiyo kupata maoni kutoka kwa watu mbalimbali ili kuwa na katiba mpya iliyo bora.

Kwa mujibu wa Kinana, Rais Kikwete amekutana na viongozi wa vyama vya upinzani na tayari amepata maoni ya CCM, kupitia Kamati yake Kuu (CC).Hivyo, alisema Rais anakutana na makundi yote ya watu bila upendeleo ili kujenga mshikamano katika kuandika katiba mpya.

Alifafanua kwamba, kinachofanyika sasa ni kuunda mchakato wa namna maoni ya katiba hiyo yatakavyochukuliwa kutoka kwa wadau mbalimbali.

Hata hivyo, alisema kwa sasa Rais anasubiri wabunge wafanyie marekebisho baadhi ya vipengele vya Sheria ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.Kinana alisema baada ya marekebisho hayo, Rais ataunda tume ya kukusanya maoni itakayojumuisha watu wa kada zote bila kujali itikadi za vyama vyao vya siasa.

Akerwa na 'uheshimiwa'
Katika hatua nyingine Kinana alisema  amekuwa akikerwa na tabia ambayo katika siku za karibuni imeshika kasi, kwa viongozi ndani ya chama kuitwa “waheshimiwa.”

Alisema hata kwenye mikutano yake na wanachama jijini Dar es Salaam amekuwa akiitwa “mheshimiwa” ambalo hakubaliani nalo na kushauri neno kuwa sahihi linalopaswa kutumika ni “ndugu.”

Rushwa ndani ya CCM
Kinana alisema kuwapo kwa vitendo vya rushwa ndani ya chama ni tatizo linachangia kwa kiasi kikubwa kupata viongozi wasiofaa ndani ya chama, hivyo kusisitiza kuwa safari hii, wameamua kulivalia njuga.
Alisema wanaotaka uongozi kwa rushwa hawafai kwa sababu hawana malengo mazuri ya chama bali binafsi.
Kinana alionya kwamba, kuna baadhi ya wanachama ambao huwashawishi wagombea ili wawape fedha kwa ajili ya kuwapigia kampeni na kuhakikisha kuwa wanashinda.
Alisema mwanachama anayetaka fedha ili amchague kiongozi hana malengo mazuri na chama hicho, hivyo naye anapaswa kuchukuliwa hatua kwa vile kufanya hivyo ni kukisaliti chama.

CCM kufuta unafiki
Katika hatua nyingine, CCM mkoa wa Dar es Salaam umesema katika uchaguzi ndani ya chama na jumuia zake unaotarajia kufanyika mwezi ujao, wamepania kuondoa aina zote za unafiki.

Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salam, Said Mihewa alisema katika kuchuja wagombea, watahakikisha haki inatendeka na kipaumbele kitatolewa kwa wanachama kufanya uamuzi.

Alisema iwapo vikao vya chini, tawi na kata vitamwelezea mwanachama yeyote kwamba hafai kuwa kiongozi, watawaita na kuwakutanisha ana kwa ana na wanayemtuhumu ili wafafanue jinsi asivyofaa.
“Tutawaita na kuwakutanisha na mnayesema hafai, mseme mbele yake kuwa hafai! Na yeye ajieleze kwa nini anasema anafaa?” alisema Mihewa.

Mchakato wa uchaguzi wa ndani wa CCM unatarajiwa kuanza mwezi ujao na kumalizika Oktoba mwaka huu.

Madaktari wagoma kumfuata Pinda ofisini

WAKATI mgomo wa madaktari ukizidi kusambaa nchini, wanataaluma hao wamesema hawako tayari kumfuata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ofisini kwake, badala yake yeye awafuate wanakofanyia mikutano yao.

Juzi, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Pinda aliwaangukia madaktari hao kuwa yupo tayari kukutana nao wakati wowote na kuwataka waende ofisini kwake kuonana naye ili wazungumze kuhusu madai yao.

Mgomo huo wa madaktari ambao ulianzia katika hospitali za Muhimbili na Ocean Road, hadi jana ulikuwa umesambaa katika hospitali nyingine nchini ambazo ni pamoja na Bugando ya Mwanza, KCMC Moshi, Bunda mkoani Mara na Meta mkoani Mbeya na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

'Pinda njoo wewe'

Akijibu ombi hilo la Pinda, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoongoza mgomo huo, Dk Stephen Ulimboka alisema hatua ilipofikia madaktari hawatakuwa tayari kumtafuta Waziri Mkuu.
“Kwa sasa mtu yeyote anayetutaka atufuata hapa, hatuwezi kumtafuta tena Waziri Mkuu sababu tulishafanya juhudi hizo bila ya mafanikio,” alisema Ulimboka ambaye pamoja na wenzake wanafanya mikutano yao ukumbi wa Starlight.

Wizara yahaha

Madaktari wakimtaka Pinda awafuate, wizara  yenye dhamana na afya jana ilitoa tamko kuhusu mgomo huo ikisema madaktari watapewa nyumba za kuishi karibu na vituo vya kutolea huduma.
Tamko hilo lilitolewa Jijini Dar es Salaam  na Waziri wa Afya na Usatawi wa Jamii Dk Hadji Mponda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mponda akijibu dai moja baada ya jingine la madaktari hao, alisema serikali kupitia wizara hiyo  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na wizara ya Fedha, inaendelea na kazi ya kurekebisha  waraka utakaoruhusu madaktari kupewa nyumba bila kujali madaraja yao na mishahara.
Akifafanua kuhusu  rufaa za wagonjwa hususani vigogo kusafirishwa nje ya nchi kwa matibabu, alisema wizara hugharamia watanzania wote bila kuangalia ni wa aina gani ili mradi watimize vigezo vya kwenda kutibiwa nje.

Muhimbili hali mbaya

Katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana wagonjwa waliambiwa warudi nyumbani hadi watakapopata taarifa za kumalizika kwa mgomo kupitia vyombo vya habari.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wagonjwa hao walisema walipewa taarifa na baadhi ya wafanya kazi katika vitengo tofauti, vinavyotoa huduma za kliniki hospitalini hapo.
Vitengo vilivyodaiwa kuwatangazia habari hiyo wagonjwa hao ni Taasisi ya Mifupa (MOI), kitengo cha kuhudumia watoto wenye matatizo ya upungufu wa damu na kitengo cha Kliniki ya matatizo ya moyo.
Mmoja wa wagonjwa hao, Rukia Hamisi alisema alipofika MOI alitokea mmoja wa wafanya kazi katika taasisi hiyo na kuwatangazia kuwa wagonjwa wote waondoke eneo hilo hadi watakapotangaziwa kuwa mgomo umekwisha.
“Mimi nimekuja tangu asubuhi, lakini ilipofika saa tatu asubuhi alikuja mfanyakazi mmoja na kututangazia kuwa tuondoke katika eneo hilo hadi tutakapo tangaziwa kuwa mgomo umekwisha kupitia vyombo vya habari,” alisema Hamisi.
Mmoja wa wafanya kazi wa MOI ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alikiri kutoa taarifa hizo na   kusisitiza kuwa hali hiyo imetokana na madaktari wanaotakiwa kuwahudumia wagonjwa hawakuwapo kazini.
Muhonewa Mfaume ambaye alikwenda hosptalini kwa ajili ya kutaka barua yake aliyopewa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iweze kusainiwa na daktari ili aweze kwenda kutibiwa nje ya nchi, alisema alipofika katika kitengo hicho aliambiwa na mmoja wa wafanyakazi wa idara ya  mapokezi kwamba, arudi nyumbani
Afisa Habari Mwandamizi wa Hosptali ya Taifa Muhimbili Aminiel Aligaesha alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alijibu kwa kifupi kuwa hana taarifa na pia akasisitiza kuwa, huduma zinazoendelea vizuri.
KCMC nako mambo yaharibika

Mgomo huo umezidi kutikisa nchi na kuvuruga huduma za utabibu baada ya madaktari katika hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi nao kujiunga rasmi kwenye mgomo.

Hata hivyo, madaktari hao wamekubaliana kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura tu wakiwamo wa ajali, wanaohitaji kujifungua na walioko wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu(ICU).

Katika tamko lao hilo, madaktari hao waliokutana katika ukumbi wa maktaba walisema katika kipindi chote cha mgomo hawatapokea wagonjwa wa nje na kwamba kliniki zote hazitafanya kazi.

Ingawa hospitali hiyo inamilikiwa na Shirika la Msamaria mwema (GSF) lakini wapo madaktari ambao mikataba yao ya ajira ipo chini ya shirika hilo na wapo ambao ajira zao ziko moja kwa moja serikalini.

Bugando

Jana madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando waliungana na wenzao katika mgomo unaoendelea kusambaa nchi nzima hivi sasa.

Madaktari hao walianza mgomo kwa kukataa kuwapokea wagonjwa wapya isipokuwa wagonjwa wa dharura tu.

Wakizungumza wakati wa mkutano wao uliofanyika katika hosteli ya madaktari wanafunzi, walisema kurudi kwao kazini kutategemea maelekezo kutoka kwa uongozi wa kamati maalum waliyoiunda kuratibu mgomo huo.

Juhudi za uongozi wa hospitali hiyo chini ya Mkurugenzi wake, Dk Charles Majinge kuzuia mgomo huo ziligonga mwamba baada ya madaktari hao kumweleza kuwa mgomo huo haujaitishwa dhidi ya hospitali hiyo wala uongozi wake na kwamba, madai yao yako nje ya uwezo wa utawala wa Bugando.

Dk Majinge alikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mgomo wa madaktari katika hospitali yake.

Bunda

Huduma ya tiba kwenye baadhi ya vituo vya afya wilayani Bunda, jana zilidorora kufuatia baadhi ya madaktari na wahudumu kuitisha mgomo.

Mwananchi imebaini kuwa ingawa wahudumu na madaktari hao wamefika kazini kwa wakati lakini walikataa kuwahudumia wagonjwa.

“Mimi nimefika hapa saa 3:00 asubuhi lakini sijahudumiwa. Wanaingia (wahudumu) wanakaa ndani kisha wanatoka bila kuwaita wagonjwa," alisema mmoja hospitalini hapo saa 8:00 mchana jana.

Kaimu mganga mkuu wa wilaya hiyo Dk Fransic Mayengera alikana uwepo wa mgomo hospitalini hapo na huku aiita hatua hiyo kuwa ni kutokana na uzembe wa watumishi wa hospitali na kwamba uongozi wake umeanza kuwashughulikia."

Wajawazito wateseka Mbeya

Mgomo wa madaktari katika Hospitali ya Meta mkoani jana uliwaathiri zaidi kina mama wajawazito huku wengine wao wakiambiwa kuwa waende katika hospitali nyingine kwa vile hospitalini hapo hakuna huduma.

Kila mgonjwa aliyefika hospitalini hapo jana alielezwa kuwa hakukuwa na huduma hivyo, akatafute hospitali nyingine huku baadhi ya wauguzi wakijibizana na wagonjwa.

Baadhi ya Waandishi wa habari waliofika katika kituo hicho cha Meta walishuhudia mama mjamzito, Sarah Christopher akiambiwa aende kwenye hospitali nyingine huku hali yake ikionyesha ni mbaya.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo ya Meta Dk Leter Msafiri alisema  kutokana na mgomo unaoendelea, kuna baadhi ya huduma zimesitishwa ila wanatoa huduma za dharura ambazo ni pamoja na upasuaji unaofanywa na madaktari bingwa.

Dk Msafiri alisema huduma zilizositishwa ni kliniki na  huduma ambazo wagonjwa wanaonekana kuwa hali zao siyo mbaya.


Kilaini
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilani alisema inasikitisha kuona wagonjwa wakiteseka hospitalini kutokana na mgomo huo.
"Kwa namna yoyote ile, wagonjwa wanapaswa kuhudumiwa kwa sababu suala la matibabu linahusisha ni uhai," alisisitiza na kuongeza:
"Inaleta shida kidogo kujua kwa nini Serikali haitatui madai ya madaktari ambayo ni ya msingi, au haina fedha?  Kama Serikali haina fedha iseme ili wahusika na Watanzania wote wajue.’’
Baregu LHRC
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimemtaka  Pinda, kwenda kuonana na madaktari hao badala ya kusubiri wamfuate ofisini.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba alisema haiwezekani Waziri Mkuu aendelee kukaa ofisini wakati anajua kuwa madaktari wanagoma na wagonjwa wanataabika.
“Hakuna haja ya Pinda kusema madaktari wakiwa tayari waende kuonana naye kwa sababu huu ni ubabaishaji. Wao (madaktari) wako tayari na ndio maana wakagoma hadi pale madai yao yatakaposikilizwa sasa yeye (Pinda) akiendelea kuwasubiri ofisini maana yake nini kama sio kuleta vifo?"                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                             
Imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Onesmo Alfred Daniel Mwingira, Ibrahim Yamola, Christopher Maregesi, Bunda, Ray Naluyaga, Godfrey Kahango, Mbeya, Daniel Mjema na Rehema Matowo,Moshi