NJOMBE

NJOMBE

Wednesday, August 22, 2012

''Kaa kando'' Todd Akins aambiwa

Mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Republican , Mitt Romney, amemtaka mwanasiasa mwenzake wa chama hicho kujiondoa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa kiti cha Useneta baada ya kutoa matamshi yaliyozua utata kuhusu ubakaji.
Mwanasiasa wa bunge la Congress, Todd Akin
Todd Akin, ambaye ni mwanasiasa wa bunge la Congress alizua manung'uniko kwa kudai kuwa mwili wa mwanamke una uwezo wa kuzuia mimba katika baadhi ya matukio ya ubakaji.
Matamshi ya Todd Kin anayegombea kiti cha seneta nchini Marekani yalitolewa wakati wa mahojiano. Alikuwa akitetea msimamo wake dhidi ya utoaji mimba.
Alipoulizwa kuhusu kutoa mimba iwapo mwanamke atabakwa, Todd Kin alieleza kuwa katika ubakaji halali au kile alichokitaja kuwa 'legitimate rape' kuna uwezekano kwamba kibiolioia, mwili wa mwanamke utamzuia kupata mimba anapobakwa.
Matamshi yake yamezua hisia kali.
Mpinzani wake Mitt Romney amesema, ''Matamshi yake kuhusu ubakaji yanaudhi sana na siwezi nikatetea msimao wake au nikamtetea yeye''
Baadhi ya wenzake Todd Akin kutoka chama cha Republican wamemtaka kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha useneta.
Hiki ni kipindi kigumu kwa wana Republican ambao walikuwa wamejiandaa kuendeleza kampeni yao kwa kumshambulia rais Obama kwa jinsi uchumi ulivyozorota wakati wa uongozi wake. Badala yake sasa wamejikuta wakirushiana maneno kuhusu sera za kijamii.
Chama cha Democrats kimechukua fursa hiyo kushambulia Republicans kwa kuwataja kama watu ambao hawazingatii maslahi na hisia za wanawake.
Todd Akin ameomba msamaha kufuatia matamshi yake.
"Nilitumia maneno yasiofaa na ninaomba msamaha. Nina watoto wawili wa kike na nataka haki kutendeka, nina roho ya huruma kwa waathiriwa wa ubakaji na nawaombea. Ukweli ni kuwa, mtu anaweza akapata mimba kutokana na ubakaji. Ukweli ni kwamba, kuna waathiriwa wengi wa ubakaji. Makosa yangu ni kutumia maneno yasiofaa. Naomba msamaha wako. ''
Hata hivyo halitakuwa jambo la kushangaza iwapo atalazimika kujiondoa kwenye mbio za kuwania kiti cha useneta kwa sababu ya matamshi hayo.

No comments:

Post a Comment