NJOMBE

NJOMBE

Saturday, August 18, 2012

Rada ya Chenge yailiza serikali


•  Matengenezo yake kugharimu sh milioni 40, itatengemaa wiki mbili zijazo
GHARAMA za kifaa kilichoharibika kwenye rada kutoka Kampuni ya BAE System ya Uingereza na kuibua utata mkubwa nchini, kitagharimu sh milioni 40.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), Fadhili Manongi, alisema kuwa wahandisi wamebaini kuwa kifaa hicho, Power Supply Unit kiliharibika wiki tatu zilizopita.
 Rada hiyo iliyonunuliwa kwa ushauri wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, iligharimu sh bilioni 40 na kuibua mjadala mzito ndani na nje ya nchi kwamba imenunuliwa kwa bei kubwa kuliko bei halisi.
Manongi alisema kutokana na tatizo hilo, wahandisi na wataalamu wa rada hiyo wamelazimika kuzima mtambo wake, huku wakifanya mawasiliano na Kampuni ya BAE Systems ili kupata kifaa kingine.
“Ubovu wa kifaa hicho ulibainika wiki tatu zilizopita na tukalazimika kuzima mtambo la sivyo kama tusingebaini hilo mtambo ungeweza kuharibika kabisa. Jumatatu ya wiki ijayo tutakipeleka kifaa hicho nchini Afrika Kusini kuona kama wanaweza kukitengeneza na wasipoweza tutaagiza BAE System kutupatia kifaa kingine,” alisema Manongi.
Hata hivyo, alisema ni kawaida kwa mtambo huo kuzimwa kwani kuna wakati wahandisi hulazimika kuzima ili kuweka mafuta mazito ya grisi.
Manongi, alisema kifaa hicho hakiwezi kupatikana mara moja kwani lazima utoe taarifa kwa kampuni husika ili iweze kukitengeneza.
Alisema pamoja na kuharibika kifaa hicho, bado huduma za usafiri wa anga zimeendelea kufanya vizuri, huku kukiwa hakuna malalamiko kutoka kwa wateja wa ndani na nje ya nchi.
Kuhusu usalama wa anga, Manongi, alisema wamekuwa wakifuatilia kwa karibu suala hilo na hakuna tatizo lolote lililojitokeza tangu kuharibika kwa kifaa hicho.
“Hii sio mara ya kwanza kuharibika na kubadilisha vipuri katika mtambo huo kwani tumekuwa tukifanya hivyo mara nyingi tu…ikumbukwe kuwa huu ni mwaka wa 12 tangu tuwe na rada hiyo,” alisema.
Alisema kuwa huduma za anga zimekuwa zikiendeshwa sio na rada peke yake, bali kuna vitu mbalimbali vinavyosaidia na kuvitaja kuwa ni Non Directional Beacon (Non), Very High Omni Direction Range (VOR) na Distance Measuring Equipment (DME).
Ununuzi wa rada hiyo uliogharimu sh bilioni 40, umekuwa ukipigiwa kelele na watu wa kada mbalimbali wakidai kulikuwa na rushwa.
Hata hivyo hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete alisema hakuna rushwa katika ununuzi wa rada hiyo na baadaye kuungwa mkono na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye aliwahi kuahidi kwamba angewataja watuhumiwa hao.
Membe aliyewasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake bungeni hivi karibuni, alishindwa kutekeleza ahadi yake licha ya kutakiwa kufanya hivyo na baadhi ya wabunge, wakiongozwa na Waziri Kivuli wa wizara hiyo, Ezekia Wenje (CHADEMA) ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana.
Kabla Membe hajasoma hotuba yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alitoa taarifa rasmi ya serikali bungeni kuhusu suala hilo na alisema hakuna mtuhumiwa wa rada anayeweza kupelekwa mahakamani na kutamka kwamba mjadala kuhusu suala hilo umefungwa.
Kashfa hiyo ya rada, imekuwa ikimhusisha Chenge ambaye pia aliwahi kukutwa na kiasi cha sh 1.2 bilioni, kisiwani Jersey, Marekani ambazo Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, ilikuwa ikichunguza kama zilikuwa na uhusiano na biashara hiyo.
Chanzo cha Habari Mtanzania Daima

No comments:

Post a Comment