NJOMBE

NJOMBE

Thursday, August 23, 2012

Dk. Ulimboka azimwa azidiwa kete

•  Vigogo serikalini wamzidi nguvu, abaki njia panda
 DHAMIRA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka ya kutaka kuwafichua polisi na watu wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio la kumteka, kumpiga, kumtesa na kumtupa katika Msitu wa Mabwepande, imezimwa na vigogo wa serikali, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Uchunguzi ambao gazeti hili limekuwa likiufanya tangu Dk. Ulimboka awasili nchini, umebaini kuwa kinara huyo wa mgomo wa madaktari uliotikisa nchini, amekuwa na vikao na vigogo wa idara za ulinzi na usalama na kumshawishi awe mtulivu katika kipindi hiki ambapo serikali inafanya uchunguzi wa kina kubaini waliohusika kumteka nyara.
Watu wa karibu na daktari huyo, walilieleza gazeti hili kuwa, katika kipindi kifupi amekutana na vigogo kadhaa wa serikali wakimtaka asiseme chochote kwa hofu ya kuvuruga uchunguzi.
Wakati vigogo wa serikali wakifanikiwa kumzima Dk. Ulimboka, upande wa pili wa wanaharakati, ndugu na madaktari wenzake, wamekuwa wakimbana kumtaka awe jasiri kueleza umma ukweli, na hata kuwataja kwa majina waliohusika kumteka.
Hata hivyo, Joshua Mulundi aliyetajwa kuwa raia wa Kenya amefikishwa mahakama akituhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Habari kutoka ndani ya uongozi wa Chama cha Madaktari (MAT), zilidai kuwa, hali ya ushawishi kutoka kwa vigogo wa serikali na mbinyo anaoupata kutoka kwa wanaharakati na madaktari wenzake, umemweka njia panda Dk. Ulimboka kiasi cha kushindwa kuamua kama atoke hadharani kueleza ukweli au atulie ili kulinda maisha yake.
Mara baada ya kurejea nchini akiwa na afya njema, Dk. Ulimboka amekuwa akikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari, kwamba anajiandaa kueleza ukweli wa tukio nzima na hata kuwataja waliohusika na unyama aliofanyiwa.
“Kwa jinsi hali ilivyo, Dk. Ulimboka atabaki na siri moyoni maana amekutana na watu wazito, wamezungumza nae na kumshawishi anyamaze, ndiyo maana hadi sasa hayuko tayari kuueleza umma kile alichopania kusema. Lakini pia wanaharakati na hata wanasiasa kila siku wanajaribu kumshawishi atoke hadharani kusema ukweli kabla tukio hilo halijaanza kusahaulika masikioni mwa watu,” alisema daktari mmoja ambaye ni mtu wa karibu na Dk. Ulimboka.
Katika kuthibitisha kwamba Dk. Ulimboka hayuko tayari kusema chochote, juzi gazeti hili lilikutana nae katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Ubungo ambapo alisema kuwa kitendo cha kinyama alichofanyiwa, anamwachia Mungu.
Dk. Ulimboka ambaye aliongozana na familia yake kanisani hapo kwa nia ya kutoa sadaka na kumshukuru Mungu, alipobanwa hakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kusema muda ukifika ataweka ukweli hadharani na kukanusha tuhuma za kunyamazishwa na vigogo.
Duru za kiintelijensia zililieleza gazeti hili kuwa, katika hali ya kawaida Dk. Ulimboka hawezi kusema chochote kama ilivyotokea kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe aliporejea kutoka kwenye matibabu.
Dk. Mwakyembe ambaye aliugua ugonjwa ambao hata mwenyewe aliamini ulitokana na sumu, uliosababisha aoze kucha, kutoka unga mwilini na miguu kupasuka, alipata kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba atakuja kueleza ukweli jinsi alivyopewa sumu iliyomsababishia ugonjwa huo.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe tangu aliporejea hadi kuteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi, hajawahi kueleza chochote kama alivyoahidi na kumweka mahali pabaya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta ambaye ndiye aliyeshikia bango kwamba Dk. Mwakyembe alipewa sumu.
Dk. Ulimboka ambaye alipelekwa Afrika Kusini akiwa hawezi kutembea wala kula mwenyewe baada ya Juni 27 mwaka huu kutekwa na watu wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, amekuwa akiwakwepa wanahabari na anaishi kwa kujificha.
Kiongozi huyo wa madaktari amerejea nchini huku serikali na madaktari wakiwa hawajafikia mwafaka kuhusu madai yao.
Madai ya madaktari hao ni hali bora ya mazingira ya utoaji afya nchini, ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu, posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa kazini.
Safari ya Dk. Ulimboka kwenda kwenye matibabu nchini Afrika Kusini ilitawaliwa na usiri mkubwa alipoondoka nchini Juni 31 mwaka huu, akisindikizwa na Dk. Pascal Lugajo, kaka yake, Dk. Hobakile Ulimboka na mke wake, Dk. Judith Mzovela.
Kutekwa
Dk. Ulimboka alitekwa na kufanyiwa vitendo vya ukatili wakati akiratibu mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea na aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono na miguu akiwa katika hali mbaya.
Kutokana na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu waliituhumu serikali kuhusika na tukio hilo, huku yenyewe ikikana na kuliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka waliohusika.
Wakati Dk. Ulimboka alipokuwa akiendelea na matibabu Afrika Kusini, Rais Jakaya Kikwete alisema serikali haihusiki na kilichomtokea daktari huyo kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu katika majadiliano baina ya serikali na madaktari.
Rais Kikwete alisema hayo katika hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
“Dk. Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya serikali na madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na serikali,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alichofanyiwa Dk. Ulimboka kimemsikitisha na kumhuzunisha kwa kuwa ni kitendo cha kinyama na kinyume kabisa na mila na desturi za Tanzania.
Kauli ya Rais Kikwete kuhusu mgomo wa madaktari inafanana na ile iliyokuwa imetolewa awali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema wanatambua kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka kuhusu kilichomtokea Dk. Ulimboka, lakini ameshangazwa na hisia hizo akisema haoni sababu ya serikali kufanya hivyo.
Chanzo Mtanzania daima

No comments:

Post a Comment