NJOMBE

NJOMBE

Thursday, August 23, 2012

Watu 48 wauawa Kenya

Ramani ya Kenya
Ramani ya Kenya
Polisi nchini Kenya, wanasema kuwa watu 48, waliuawa siku ya Jumanne usiku wa kuamkia , Jumatano, kufuatia mapigano makali kati ya jamii za Pokomo na Orma katika eneo la Mto Tana Kusini Mashariki mwa Kenya.
Mauaji hayo yilitokea wakati watu wenye silaha kutoka jamii ya Pokomo waliposhambulia kijiji kimoja katika eneo la Reketa huku wakiteketeza makaazi ya watu.
Naibu kamanda wa polisi mjini Mombasa, Joseph Kitur, amethibitisha kuwa watu 48 waliuawa, 31 kati yao ni wanawake, watoto 11 na wanaume sita.
Ng'ombe wapatao 60 vile vile walikatakatwa na wavamizi hao.
Kitur amesema shambulio hilo ni la kushangaza kwa kuwa watu 34 waliuawa kwa kukatakatwa mapanga, wengine 14 nao waliteketea hadi kufa katika nyumba zao.
Amesema uchunguzi wa awali umebainisha kuwa shambulio hilo lilifanywa na watu kutoka jamii ya Pokomo.
Tangu mwezi uliopita, jamii hizo mbili zimekuwa zikipigana kuhusu umiliki wa ardhi inayotumiwa kama eneo la malisho ya mifugo, lakini shambulio hilo la Jumatano ndilo baya zaidi kuwahi kutokea katika historia yao.
Ripoti zinasema polisi wanawasaka wale waliofanya mashambulio hayo.
Kuna taarifa kuwa watu kadhaa wamekamatwa na polisi lakini mkuu huyo wa polisi hakuthibitisha ripoti hizo.
Idara ya polisi imesema uhasama kati ya jamii hizo mbili umekuwa ukitokota kwa muda, lakini hapakuwa na ishara ya fununu yoyote kuwa shambulio hilo la Jumatano lingetokea.
Mwaka wa 2001, takriban watu 130, waliuawa kwenye mapigano katika maeneo ya mipakani kati ya jamii hizo mbili.
Mbunge wa Eneo hilo, Danson Mungatana, amesema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi mashambulio mengine yaliyofanywa na jamii ya Orma ambapo mamia ya mifugo iliibwa.

No comments:

Post a Comment