NJOMBE

NJOMBE

Thursday, August 30, 2012

Ngoma nzito Polisi


•  Wadaiwa kumfanyia mtoto unyama wa kutisha Manyara

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa kutokana na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola, Rais Jakaya Kikwete, anapaswa kuingilia kati kuunda tume huru ili kuwezesha uchunguzi wa kina.
Hata hivyo, wakati CHADEMA ikitaka tume huru ya kuchunguza matukio hayo likiwemo lile la kuuawa kwa kijana Ally Hassan Singano maarufu kama Zona katika maadamano yao juzi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, limejivua lawama za mauaji hayo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema wanapinga kauli za serikali, Jeshi la Polisi na CCM zenye kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na mauaji yanayoelezwa kufanywa na askari mkoani Morogoro.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alisema kuwa kauli zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani juzi, Dk. Emmanuel Nchimbi zina mwelekeo wa kulilinda Jeshi la Polisi, ambalo askari na maofisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji badala ya kuwezesha ukweli kuthibitika na hatua kuchukuliwa kwa wahusika.
“Ikumbukwe kuwa Agosti 27 mwaka huu, polisi mkoani Morogoro walifyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya machozi wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa ajili ya kuelekea kwenye mkutano halali, na kusababisha kifo cha raia mmoja asiye na hatia na kujeruhi wengine wawili,” alisema.
Alisema kwa mauaji hayo na mengine katika maeneo mbalimbali nchini, Serikali ya CCM kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya msingi wa raia wote.
Mnyika alibainisha kuwa, hawakubaliani na hatua zilizochukuliwa na serikali mpaka sasa kuhusu tukio husika pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waziri Nchimbi juzi, ambayo alidai kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli kutoka polisi.
“CHADEMA haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za askari kufyatua risasi na mabomu ya machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na jeshi hilo wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Kwamba wakati serikali na polisi wakisema kuwa marehemu alikutwa umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani na eneo lake na ofisa mmoja akaonesha ishara, na ndipo mabomu ya machozi na risasi za moto zikafyatuliwa na mojawapo kumpata na kudondoka.
Mnyika alidai kuwa mashahidi wote waliohojiwa wanaeleza kwamba bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo pekee yanayotofautiana ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za moto na wengine wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi.
Aliongeza kuwa sababu zilizotolewa na serikali kuwa polisi walizuia maandamano ya CHADEMA mkoani Morogoro kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si za kweli kwa vile sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu wa barabara na kuwa yalipangwa siku ya kazi.
Kwa mujibu wa Mnyika, ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la Polisi ya Agosti 23, 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL.II/202 na kwamba polisi mkoani Morogoro ndio waliacha kuheshimu utawala wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo ya pande zote.
“Kwa kuzingatia utofauti mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na serikali na Jeshi la Polisi kuhusu matukio husika na ukweli halisi ulivyotokea, CHADEMA kinasisitiza kuwa uchunguzi huru ufanyike kwa mujibu wa sheria ya uchunguzi wa vifo sura ya 24 ya sheria za Tanzania,” alisisitiza.
Wajitetea Moro
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema kuwa matokeo ya uchunguzi wa tukio hilo, yalionesha kwamba jeraha lililokuwa kichwani kwa marehemu lilitokana na kugongwa na kitu kizito kilichorushwa na si risasi.
Alisema kuwa uchunguzi huo ulifanywa na madaktari wawili wa mkoani humo pamoja na Dk. Ahmed Makata kutoka jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na mwanasheria wa CHADEMA, Aman Mwaipaya na baadhi ya askari.
Kamanda Shilogile alisema kuwa baada ya matokeo hayo ya daktari, polisi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kubaini kitu hicho kilichorushwa na kusababisha kifo cha kijana huyo.
Alisema kuwa baadaye Jeshi la Polisi litachukua hatua za kisheria kwa askari ama mtu mwingine atakayebainika kuwa alirusha kitu hicho, ikiwa ni pamoja na kumkamata kiongozi wa CHADEMA aliyechochea maandamano hayo yaliyozua vurugu.
Kamanda Shilogile alisema kuwa ili kubaini hayo yote, serikali imeunda tume ya kuchunguza na kwamba inayoundwa na askari polisi na watu wengine ambao watasaidia kukamilisha uchunguzi huo.
Aliongeza kuwa tume hiyo ambayo tayari imeshafika mkoani Morogoro itatafuta maelezo na ushahidi kutoka kwa watu mbalimbali walioshuhudia tukio hilo, wakiwemo wanahabari na hivyo kuwaomba wote watakaohitajika kutoa ushirikiano.
Kuhusu majeruhi Hashimu Seif aliyejeruhiwa mguu katika vurugu hizo, Shilogile alisema kuwa uchunguzi umebaini kuwa alijeruhiwa na bomu lililomuangukia mguuni na kwamba anaendelea vizuri ikiwa bado yuko hospitali ya mkoa kwa matibabu zaidi.
Wadaiwa kumtesa mtoto
Katika hatua nyingine jeshi hilo Mkoa wa Manyara, limeingia katika kashfa nzito likidaiwa kumpiga na kumuumiza vibaya mtoto wa kiume, Kadogoo Kalanga (16), ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Selina kwenye chumba cha uangaliazi maalumu (ICU) akiwa hajitambui.
Mtoto huyo ambaye taarifa za polisi juu ya kilichompata zinatofautiana, yuko mahututi akiwa amevimba sehemu za siri na nyuma ya kichwa (kichogoni).
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Akili Mpwapwa alisema kuwa mtoto huyo alipatwa na hali hiyo baada ya kufikishwa kwenye kituo cha polisi cha Orkasumeti wilayani Simanjiro kwa tuhuma za wizi wa mbuzi wawili na kupandisha mori, na hivyo kujipigapiga chini hali iliyomsababishia kupoteza fahamu.
Hata hivyo, maelezo yake yanapingana na polisi waliompeleka mtoto huyo kwenye kituo cha afya Orkasumeti, ambao waliwaeleza madaktari kuwa alipata ajali ya pikipiki.
Daktari aliyempokea mtoto huyo kituoni hapo, aliyejitambilisha kwa jina moja la Ester, alimweleza mwandishi wa habari juzi kwa njia ya simu kuwa, mtoto huyo alifikishwa hapo Jumatatu wiki hii na askari ambao walimweleza kuwa alipata ajali ya pikipiki.
Alisema kuwa walimpa huduma ya kwanza, lakini kutokana na hali aliyokuwa nayo ya kutojitambua, walishindwa kubaini anaumwa wapi, hivyo siku iliyofuata akashaurina na madaktari wenzake wakaamua kumpa rufaa kwenda hospitali yenye vifaa kwa ajili ya vipimo zaidi.
Kamanda Mpwapwa alipoelezwa kuwa taarifa yake inatofautiana na ile ya askari wake kwenye kituo cha afya, aliendelea kusisitiza kuwa taarifa anazotoa ni zile alizopewa na Mkuu wa Polisi (OCD) wa Wilaya ya Simanjiro, na kwamba kama inatofautiana na nyingine hilo halimuhusu.
“Maelezo ninayokupa mimi ni yale niliyopewa na OCD wangu, kama kuna “contradiction” (mkanganyiko) kati ya taarifa niliyopewa na ambayo imetolewa mahali pengine hilo si tatizo langu,” alisema.
Naye mama wa mtoto huyo, Paulina Kalanga, aliwaeleza waandishi wakati akisubiri mtoto wake apatiwe matibabu kwenye hospitali ya Selian kuwa, alipata taarifa kwamba Kadogoo yuko kituo cha afya saa tano asubuhi ya Jumatatu na alipofuatilia alimkuta akiwa hajitambui.
Alisema madaktari walimweleza kuwa mtoto huyo alipelekwa hapo na askari polisi watatu na alipomkagua akishirikiana na ndugu zake, walibaini kuwa ameumizwa vibaya sehemu za siri ambazo  zimechubuka na kuvimba, huku kaptula aliyokuwa ameivaa ikiwa imelowa mkojo na kuchanika eneo la katikati.
Paulina aliongeza kuwa, tangu wakati huo hadi jana asubuhi mtoto huyo hajaongea zaidi ya kuzungusha kichwa sana wakati fulani, hali inayomlazimu amsaidie kukishikilia kuepuka asijiumize.
Alisema kuwa mtoto huyo anaonekana kuumia kila anapoguswa maeneo ya nyuma ya kichwa, kwenye mbavu na kwamba anahisi mfumo wake wa haja ndogo huenda umepata tatizo kwani tangu Jumatatu hapati choo kidogo licha ya kuwekewa chupa kadhaa za maji ya kumwongeza nguvu mwilini.
Kadogoo alilazimika kuhamishiwa katika Hospitali ya Agha Khan ya mjini Arusha kwa kutumia gari la wagonjwa la Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro lenye namba za usajili SM 5004 ili kufanyiwa kipimo cha kichwa, CIT SCAN.
Mama mzazi wa mtoto huyo pamoja na ndugu wengine waliokusanyika hospitalini hapo, walieleza masikitiko yao juu ya kitendo hicho cha kinyama wakidai mpaka sasa polisi imeshindwa kuwapa namba ya taarifa iliyofunguliwa kwao (RB) kuhusu kosa linalomkabili Kadodoo.
Chanzo Mtanzania daima

No comments:

Post a Comment