NJOMBE

NJOMBE

Friday, August 17, 2012

Uingereza yatishia ubalozi wa Ecuador

Wakati Julian Assange, alipotorokea ubalozi wa Ecuador miezi miwili iliyopita, Serikali ya Uingereza ilisema kuwa alikuwa amekwepa mikono ya maafisa wa usalama wa taifa hilo.
Maafisa wa Uingereza walieleza kwamba bado wangalimtia mbaroni Assange kama angaliondoka kwenye ubalozi huo, kwa madai kuwa alikataa kutii masharti ya kuachiliwa kwa dhamana na mahakama. Ilidhaniwa kuwa bora tu aendelee kuwa katika ubalozi wa Ecuador alikuwa salama.
Hata hivyo Uingereza imebadili kauli yake na kusema kuwa inaweza kuingia katika ubalozi wa Ecuador mjini London na kumtia mbaroni Assange chini ya Sheria maalumu inayohusiana na maswala ya kibalozi ya mwaka 1987.
Waziri wa mashauri ya Kigeni wa Ecuador ameshutumu kauli hiyo ya Uingereza na kusema kwamba ni vitisho ambavyo "ni kinyume cha demokrasia, na tabia ya watu wasiostaarabika wala kuheshimu sheria. Waziri Ricardo Patino alisema kuwa Uingereza ikiingia katika ubalozi wake, kitendo hicho kitatambuliwa kama uchokozi.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya kigeni wa Uingereza amefafanua kuwa Uingereza ingali ina matumaini kwamba maafikiano yatapatikana kidiplomasia. Lakini maafisa wa Uingereza wangali wanasisitiza kuwa ni wajibu wao kumkamata na kumhamisha Assange hadi Sweden ambako anakabiliwa na madai ya ubakaji kutoka kwa wanawake kadhaa.

No comments:

Post a Comment