NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, July 10, 2012

Dk. Migiro augwaya uraisNAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliyemaliza muda wake, Dk. Asha-Rose Migiro, amegoma kuweka bayana kama ana mpango wa kuwania wadhifa wa urais kama ambavyo amekuwa akibashiriwa na badala yake alisema kwamba ataendelea na kazi yake ya ualimu.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kurejea nchini jana akitokea Marekani, Dk. Migiro alisema kuwa kwa sasa anapumzika kwa muda kabla ya kurudi tena kwenye ulingo wa siasa.
Mwanasiasa huyo, amekuwa akitajwa sana siku za hivi karibuni kama mmoja wa watu wanaoweza kusimamishwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015 kurithi mikoba ya Rais Jakaya Kikwete.
Bila kukubali wala kukataa, Dk. Migiro aliyeitangaza nchi kwenye ramani ya dunia, alisema, “Kwa taarifa yenu nchi hii tayari ina Rais na mimi baada ya kumaliza kipindi changu cha miaka mitano UN nina hamu ya kurejea nchini…nimerejea kama mama wa familia, kama dada na kama mwalimu.
“Nitakuwa nje ya siasa kwa muda; unajua baada ya kumaliza utumishi wako UN ziko taratibu unazotakiwa kufuata; pia siku mbili kabla ya kumaliza muda wangu Katibu Mkuu Ban Ki-Moon, aliniteua kuwa mjumbe wa Kamati ya Ukimwi, hivyo sijajua majukumu yangu yatakuwaje,” alisema Dk. Migiro.
Dk. Migiro ambaye kabla ya kushika wadhifa huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, aliwasili kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 9:28 alasiri na kulakiwa na viongozi mbalimbali wa CCM na baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Nafurahi kumaliza miaka mitano kwa mafanikio; nitarudi Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) kutoa taarifa kwamba nimerejea nchini… kwa sababu wakati naondoka nilichukua likizo bila malipo ambayo imekwisha mwaka jana… nilikuwa mwalimu kwenye Kitivo cha Sheria,” alisema Dk. Migiro.
Kabla ya kurejea Tanzania naibu katibu mkuu huyo, aliandika waraka maalum na kuutuma kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ukiwa na kichwa kisemacho ‘Hakika, kila chenye mwanzo hakikosi mwisho na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa jingine.’
Kuhusu mchakato wa kupata Katiba mpya, Dk. Migiro alipongeza na kusema miongoni mwa mambo aliyoyasimamia alipokua UN ni utawala wa sheria na haki za binadamu huku akisisitiza kwamba upatikanaji wa Katiba mpya ni jambo muhimu.
Chanzo cha habari Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment