NJOMBE

NJOMBE

clock

Sunday, July 15, 2012

CHADEMA yalitikisa Bunge

WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) sasa wamedhihirisha wazi kuwa kero kwa uongozi wa Bunge.
Hali hiyo imedhihirika waziwazi juzi baada ya kiti cha Spika kuchukua uamuzi mzito dhidi ya wabunge wawili machachari wa CHADEMA, Tundu Lissu na John Mnyika.
Juzi kiti cha Spika kilichukua uamuzi mzito dhidi ya hotuba kali ya kambi ya upinzani ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria iliyowasilishwa bungeni mjini hapa na mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani, ambaye pia ni Mbunge wa  Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lisu na kusababisha kiongozi huyo kupelekwa kwenye  Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.
Hatua hiyo ilifikiwa  baada ya mnadhimu huyo kukataa kufuta maneno aliyoyaandika na kuyasoma katika hotuba yake ambayo yalikuwa yakieleza kuwa baadhi ya majaji wanaoteuliwa hawana uwezo, hivyo wanashindwa kufanya kazi zao ipasavyo.
Imedaiwa kuwa maneno hayo ni ya kashfa kwa majaji na serikali kwa ujumla.
Awali baada ya kumalizika kwa hoja za wabunge waliokuwa wakichangia mjadala wa bajeti ya Sheria na Katiba iliyojadiliwa kwa siku moja na kupitishwa jana. Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Muhagama, alimpa nafasi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ili kuzungumza kuhusiana na kauli zilizotolewa na kiongozi huyo wa kambi ya upinzani.
Mwanasheria huyo alieleza kuwa ana wajibu wa kuwaelekeza mawakili popote walipo na hasa walioko bungeni kufuata na kusimamia misingi ya taaluma hiyo bila kuathiri wadhifa wao wa ubunge.
“Kwa kweli nimefedheheka sana na maneno yaliyotolewa bungeni leo na jambo la kwanza ni maoni ya msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kuhusiana na bajeti ya Katiba na Sheria,” alisema Werema.
Aidha, Werema alitumia nafasi hiyo kumtaka mnadhimu huyo wa kambi ya upinzani kufuta maneno yake hayo ambayo alisema kuwa hayana ukweli wowote kwani majaji wote wanaoteuliwa wana uwezo mkubwa na wanateuliwa kwa kufuata misingi na taratibu husika ambazo zimewekwa za kuwapata majaji.
“Kauli hiyo ni ya ajabu sana na sikutegemea mtu kama Lisu unaweza kuzungumza kauli kama hiyo  na kuwataja watu ambao hawana uwezo wa kuingia humu ndani ya Bunge kujitetea huku ukijua dhahiri kuwa kanuni zetu zinakataza kuwataja watu wa aina hiyo.
“Mwenyekiti namtaka mbunge afute kauli yake hiyo na vinginevyo kama akikataa basi inabidi apelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi,” alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Baada ya Mwanasheria Mkuu kutoa muongozo huu kwa mwenyekiti wa Bunge, shughuli za kupitisha bajeti ya Katiba na Sheria ziliendelea na zilipomalizika mwenyekiti alimtaka afute maneno yake kama alivyoagizwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baada ya kukataa kufuta mwenyekiti huyo alisema jambo hilo analipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili liweze kuchukuliwa hatua.
“Naiagiza kamati hiyo ipitie mwenendo wa shughuli zote kwa siku ya juzi, pamoja na “Hansard’’ na mtiririko wote wa miongozo iliyotolewa na kulishauri Bunge nini lifanye katika hatima ya jambo hilo, kwa kufanya hivyo tutajenga heshima ya Bunge katika kufanya maamuzi na kushughulikia mambo mengine,” alisema Mhagama.
Mbali na hilo, mwenyekiti huyo alisema kwenye ukurasa wa tisa wa hotuba ya kambi ya upinzani Lissu alitamka kuwa kuna baadhi ya majaji ambao waliteuliwa na rais hawana uwezo na hawakufanyiwa usaili.
Mwenyekiti huyo alisema kauli hiyo inaingilia mambo ya mhimili mwingine ambao ni Mahakama, hivyo ni kinyume cha kanuni za Bunge.
Alisema pia kwa kuondoa maneno hayo kutalinda heshima ya  uteuzi wa majaji uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni pamoja na kuwatendea haki majaji hao kwa kutoendelea kuvunja kanuni namba 64 kwa kujadili mwenendo wa majaji hao ndani ya Bunge.
Baada ya Mhagama kutoa nafasi hiyo Lissu alianza kwa kukilaumu kiti kwa kukiuka kanuni na kudai kuwa wanaotaka kutoa maneno hayo katika hotuba yake hawakuzingatia kanuni.
“Mwenyekiti kwa heshima kubwa sana nimeshangazwa sana na utaratibu ambao unataka kutumika hapa, kwani haupo katika kanuni za Bunge na haupo mahali popote,” alisema.
Lisu alisema kama  kuna jambo ambalo mtu hakulipenda ama kama amesema kitu ambacho si cha kweli alipaswa kuomba utaratibu kwa mujibu wa kanuni 68 (1) ili akae na anielekeze kama nilichosema kipo kinyume na utaratibu na si vinginevyo.
Mnadhimu huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa kama alisema uongo utaratibu wa kanuni upo kwenye kanuni ya 63, ambayo inazungumzia kutosema uongo bungeni na hatua za kuchukuliwa dhidi ya mtu huyo na si kutakiwa afute bila kufuata kanuni kama ilivyo hivi sasa.
“Sasa natakiwa nifute tu bila kufuata kanuni, hapa tutagombana sana na kwa kitendo hicho cha kuniambia nifute bila kiti chako kufuata kanuni ni kuniambia mnataka kukanyaga kanuni za Bunge hili, hivyo mimi sitakuwa tayari,’’ alisema Lissu.
 Kwa upande wa Mnyika, Naibu Spika Job Ndugai alilazimika kuagiza mbunge huyo afikishwe katika kamati hiyo kwa madai ya kutoa tuhuma za uongo dhidi ya Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba akidai kuwa anakabiliwa na tuhuma za EPA.
Agizo hilo hata hivyo lilipingwa vikali na Mnyika pamoja na kambi ya upinzani, likihoji maamuzi ya kiti hicho juu ya suala hilo.
Mara kadhaa wabunge wa CHADEMA na wale wa NCCR Mageuzi, wameshambuliwa vikali na wabunge wa CCM, huku ikidhihirika kutetewa kwa nguvu kubwa na kiti cha Spika.
Mathalani, wabunge wa CCM wamekuwa wakishambulia wale wa upinzani kwa maneno ya kudhalilisha, lakini kiti cha spika kimekuwa mara kadhaa kikifumbia macho, kinyume cha hali inapokuwa hivyo kwa wabunge wa upinzani.
Itakumbukwa kwamba wakati Mnyika akichukuliwa hatua hiyo, hadi sasa mwongozo wa spika kuhusiana na kauli ya waziri mkuu kulidanganya Bunge, na lile sakata la Zitto dhidi ya Mkulo havijachukuliwa hatua yoyote kwa mwaka sasa.
Chanzo Mtanzania Daima

No comments:

Post a Comment