NJOMBE

NJOMBE

Sunday, July 15, 2012

Mkurugenzi Mtendaji, vigogo TANESCO wasimamishwa kazi


BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mhandisi William Mhando na wafanyakazi wengine watatu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka unaoikabili menejimenti hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Victor Mwambalaswa, ambaye ni Mbunge wa Lupa (CCM), ilisema kuwa Julai 13 bodi ilikutana katika kikao cha dharura na kujadili masuala mbalimbali ikiwamo tuhuma hizo.
Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Jenerali Robert Mboma (Mstaafu), ilisema kuwa kutokana na tuhuma hizo kuwa nzito, ni vema ukafanyika uchunguzi huru ambao unaanza mara moja kwa kumtumia mchunguzi huru.
Iliwataja wengine waliosimamishwa ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Manunuzi, Harun Mattambo.
Ilisema kuwa pamoja na hatua hizo, bodi itahakikisha shughuli za kiutendaji na uendeshaji wa shirika hilo zinaendelea kama kawaida.
Hata hivyo, kusimamishwa kwa vigogo hao kumezua tafrani, huku kukiwa na habari kwamba hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni kuficha siri nzito ya kukwama kwa shirika hilo.
Habari zimedai kuwa kumsimamisha kazi Mhando kunatokana na kile kinachosemwa ‘jeuri’ yake ya kukataa maagizo ya wakubwa ambao wamekuwa wakitaka kuliendesha shirika hilo kisiasa zaidi badala ya kukubaliana na uhalisia.
Wakati Mhando akidaiwa kuhujumu shirika, habari zinasema kuwa yeye mwenyewe ameelekeza lawama kwa serikali na watendaji wake wakuu kwa kulinyima shirika hilo pesa ilizoahidi kwa ajili ya miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme, na kulizuia shirika hilo kuuza umeme kwa faida, kwa sababu za kisiasa.
Inasemekana hatua dhidi ya Mhando inatokana na woga wa waziri na katibu mkuu juu ya mjadala mkali unaotarajiwa kuibuka bungeni wakati wa kujadili bajeti ya wizara yao. Mhando anatolewa kafara kisiasa, lakini taarifa zinasema naye amejibu barua ya katibu mkuu kueleza jinsi asivyohujumu shirika hilo.

No comments:

Post a Comment