NJOMBE

NJOMBE

Sunday, July 22, 2012

Utoro wa wabunge wakwamisha bajeti

UTORO wa wabunge uliokemewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, wiki iliyopita jana ulikwamisha kupitishwa kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Wiki iliyopita Makinda alisema utoro kwa wabunge hivi sasa umekithiri na akaonya kuwa kama wataendelea na tabia hiyo ipo siku watakwamisha upitishaji wa bajeti ya wizara husika.
Utabiri huo wa Spika Makinda, jana ulitimia baada ya wabunge hasa wa kambi ya upinzani kuibua hoja ya kukwamisha upitishwaji wa bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka 2012/2013 kutokana na uchache wa wabunge.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), ndiye aliyekuwa wa kwanza kutoa hoja kwa kutumia kanuni ya 112 ambapo alitaka bajeti hiyo isipitishwe kwa kuwa wabunge waliopo hawajafikia nusu ya wabunge wote.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni inataka Bajeti ipitishwe ikiwa idadi ya wabunge waliohudhuria itafikia nusu ya wabunge wote.
“Hapa tulipo mimi nimeshahesabu mara mbili wabunge wote hatuzidi 110, na tunajua idadi ya wabunge wote ni 352 na nusu yake ni wabunge 175, ili tutende haki nakuomba uhesabu idadi ya wabunge waliopo kabla ya kupitisha bajeti hii ili tuwatendee haki Watanzania,” alisema.
Baada ya hapo alisimama Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) akitumia kanuni ya 77 (1) na (2) kuwa wabunge waliopo hawafikii nusu ya wabunge wote.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni ya 77 (1). Akidi kwa kila kikao cha Bunge wakati wa kufanya maamuzi itakuwa ni nusu ya wabunge wote, kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 94 ya Katiba, isipokuwa kwamba idadi hiyo haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa kubadilisha masharti yoyote ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.
“Mbunge yeyote aliyehudhuria anaweza kumjulisha Spika kwamba, wabunge waliopo ni pungufu ya akidi inayohitajika kwa ajili ya shughuli inayoendelea.
“Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Naibu Spika, nasisitiza kuwa hatufiki nusu humu ndani,” alisema.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi) naye alisisitiza kanuni hiyo hiyo kipengele cha tatu. “Endapo Spika ataridhika kwamba kweli idadi ya wabunge walio ndani ya Ukumbi wa Bunge ni pungufu ya akidi inayohitajika basi atasimamisha shughuli za Bunge kwa muda atakaoutaja na atamwagiza katibu kupiga kengele.”
Naibu Spika Job Ndugai, alisema idadi hiyo inatakiwa wakati wa kupiga kura ya mwisho ya kuipitisha bajeti hiyo si wakati wa hatua za awali za kamati ya matumizi.
Kauli hiyo ilimfanya Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu, asimame na kutaka kiti cha Spika kisiliburuze Bunge kwa kukiuka kanuni na kuliomba Bunge liahirishe shughuli hiyo.
Hata hivyo Ndugai hakukubaliana na kauli ya Lissu. Ndugai huku akisema kuahirisha shughuli za Bunge ni gharama kubwa, alichukua muda kuamua jambo hilo.
Ndugai aliamuru Kamati ya matumizi iendelee huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alitoka nje kuwahamasisha wabunge warejee ukumbini. Mbali na juhudi za Waziri Lukuvi pia kengele ilikuwa ikipigwa nje ya ukumbi wa Bunge kuwahamasisha warejee ukumbini.
Juhudi zakwama
Pamoja na jitihada za viongozi mbalimbali wa serikali na Bunge kuhakikisha idadi ya wabunge inafika nusu, jambo hilo lilishindikana na ndipo Ndugai alipoamua kuahirisha shughuli za Bunge.
“Ni Vizuri wananchi waelewe kuwa tuna huu msiba wa kitaifa unaoendelea Zanzibar kuna wabunge wenzetu wako kule Zanzibar hasa kutoka Zanzibar kwa ruhusa ya Spika…, kuna mawaziri na manaibu wapo kule na wengine wako kule kwa shughuli maalumu.
“Kuna wabunge kadhaa ambao mimi mwenyewe nimewaruhusu wapo kwenye msiba wa mazishi ya mama wa mbunge mwenzetu, Mike Lekule Laizer (CCM).”
Wakati Ndugai akiendelea kutoa ufafanuzi huo, wabunge wa upinzani walikuwa wakitoa kauli na kugonga meza kuonesha kupinga utetezi huo.
Vitendo hivyo vilimfanya Ndugai kuwataka wamsikilize badala ya kupiga kelele ambazo haziwasaidii, kwakuwa kiti cha Spika hakiwezi kumkandamiza mtu.
“Nawaombeni ndugu zangu tunaposikilizana kama watu wazima…tupeane nafasi, mnalolitaka litakuwa …..mkisema nyinyi nawapa nafasi….mimi nikisema mnaanza kupiga kelele.
“Inanisikitisha sana tunapovunjiana heshima, tunakuwa kama watoto wadogo, mimi sidhani kama inatujengea heshima mahali popote katika nchi yetu, tunafanya jambo la msingi la taifa,” alisema.
Alisema kwa busara alizonazo ameamua kuahirisha kikao hicho, hatua ya kamati ya Bunge zima hadi Jumatatu (kesho).
Baada ya kauli hiyo wabunge wengi hasa wa upinzani walikuwa wakipiga meza kwa kushangilia ‘ushindi’ walioupata.
NCCR-Mageuzi wakomalia
Mara baada ya Bunge kumalizika wabunge wa NCCR-Mageuzi walikutana na waandishi wa habari na kuweka bayana kuwa hivi sasa wanafanya uchunguzi kujua ni vikao gani vilifanyika bila idadi ya wabunge kutimia, baada ya hapo wapeleke hoja kutaka maamuzi yaliyofikiwa yatenguliwe.
Mbunge wa Kasulu Kusini, David Kafulila, alisema maamuzi mengi yamekuwa yakifanywa bila akidi kutimia, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya taifa.
“Tutaomba Spika atupe orodha ya wabunge waliohudhuria katika kikao hiki cha Bajeti na tukibaini tutaomba maamuzi yaliyoafikiwa yatenguliwe,” alisema.
Chanzo cha habari Mtanzania Daima.

No comments:

Post a Comment