|
Mh.Mary Nagu |
HARAKATI za urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeingia
katika hatua mpya baada ya kuvuja kwa taarifa za kuwapo mkakati wa
kuwapa nafasi wanasiasa wanawake na kuwatosa wanaume kwa kile
kinachodaiwa kuvunja makundi yenye uhasama.
Habari za ndani ya makundi makuu ya wataka urais ndani ya CCM,
zimethibitisha kuwapo taharuki kubwa miongoni mwao baada ya taarifa za
wanawake kupewa nafasi kubwa kuzidi kushika kasi siku zinavyozidi
kwenda.
”Kuna mpango wa kuwatosa wanaume kwa nia ya kuwapa fursa wanawake
ndani ya CCM ili baadae atakayepatikana, akishinda akasaidie kulinda
maslahi ya wale wasio na uadui wa kudumu, lakini wana maslahi ya kudumu
(permanent interests)," alieleza mtoa habari wetu.
|
Mh.Anna Tibaijuka |
Habari zinaeleza kwamba, nguvu kubwa iliyotumika katika maeneo
mbalimbali nchini katika chaguzi za ndani ya CCM ni moja ya mikakati ya
maandalizi ya mpango huo wa kuwasimika wanawake.
Wataka urais wanaolengwa kuzimwa ni pamoja na Waziri Mkuu aliyejiuzulu
kwa kashfa, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wanawake wanaotajwa kufanikisha mpango huu ni Dk. Mary Nagu, Prof.
Anna Tibaijuka na Dk. Asha Migiro ambao wote watasukumwa na makundi
yenye fedha nyingi ili angalao wawili kati yao waingie hatua ya mwisho.
”Ambao wanatajwa kutaka kuingizwa hatua za mwisho ni Migiro na
Tibaijuka ili wapate nafasi ya kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu
wa CCM ambao kwa kiasi kikubwa wameandaliwa kwenye chaguzi za CCM
zinazoendelea kwa mikakati maalum na kwa nguvu kubwa ya fedha,” kilisema
chanzo chetu.
|
Mh.Asha Rose Migiro |
Uchaguzi unaoendelea ndani ya CCM kwenye nafasi mbalimbali, una
umuhimu wa peke yake mwaka huu kutokana na ukweli kwamba ndio uchaguzi
wa mwisho ambao utaonesha sura halisi ya kuwapata wagombea wa nafasi za
udiwani, ubunge na urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2015.
Tayari makundi yameshajipanga kwa kuanza kufitiniana, kuwekeana
mizengwe na mengi yanayofanana na hayo ili mradi tu watu wao wapite
kwenye chaguzi hizi za ndani ya chama ili iwe rahisi kupata mtu wa
kulinda maslahi yao au kujihakikishia ulaji pindi mtu wao atakapopita.
Kutokana na nguvu ya CHADEMA na kile kinachoonekana kwa wana CCM wenye
ushawishi mkubwa kuogopana kwa sababu mbalimbali, kuna mkakati wa kuwa
na 'plan B' ya kusimamisha wanawake, mkakati kama uliotumika kumzima
aliyekuwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta.
Sitta alijikuta akitolewa nje ya ulingo baada ya majina ya wanawake
pekee kupitishwa na Kamati Kuu ya CCM kuwania nafasi hiyo ya uspika.
Wakati akitetea kiti cha uspika, Sitta ambaye sasa ni Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alikuwa mstari wa mbele katika kupinga
ufisadi baada ya kutajwa ya kuwa aliendesha kampeni ya kumng'oa
aliyekuwa waziri mkuu kwa wakati huo, Lowassa, kwa kulazimishwa na Bunge
kujuzulu kutokana na kashfa ya kampuni tata ya kufufua umeme ya
Richmond.
”Hapa Sitta alikuwa hana jinsi ila kusalimu amri, na yakafanyika yaliyokusudiwa na wabaya wake wanaounga mkono ufisadi.
“Hii plan B inaweza kutumika kabisa kwenye uchaguzi ujao 2015 kutokana
na mikakati yenye hila inayohusisha fedha nyingi inayoendelea ndani ya
CCM,” kilisema chanzo chetu.
Kwa kadri muda unavyokwenda, kumekuwa na ongezeko la malalamiko kwenye
chaguzi za CCM katika ngazi mbalimbali kutokana na nguvu kubwa ya fedha
kutumika kama njia ya kujipanga kwenye kupitisha jina la mgombea kwenye
nafasi ya urais.
Mfumo ulioko sasa hivi wa kuwatumia wajumbe wa halmashauri kuu za
wilaya/mikoa kuchagua wawakilishi wa kwenda kwenye Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) na Mkutano Mkuu wa Taifa umeonesha kuwa na dosari kubwa sana
kutokana na rushwa kubwa ya fedha inayotumika kuwapata wawakilishi
hawa.
Watu wenye malengo ya kugombea urais na wapambe wao wamekuwa wanatoa
fedha nyingi kwa watu wanaowataka kwenye mikoa na wilaya ili pindi
watakapochaguliwa wakawapigie kura ya kuwapitisha kwenye NEC na mkutano
mkuu wa taifa.
"Kwa kweli rushwa za namna hii ni hatari sana na zinaweza kutupatia
viongozi wa ajabu na wapenda rushwa kutokana na mbegu waliyoiotesha
tokea kwenye msingi. Demokrasia nzuri ni ile ya kupanua wigo ili pawe na
matokeo mazuri na yenye maslahi mapana zaidi," alisema mstaafu mmoja wa
CCM.
Baadhi ya wastaafu na wana CCM wanaochukia rushwa wanapendekeza kuwapo
kwa baraza rasmi la mwisho la kupitisha jina la mgombea wa urais hata
kama amepitishwa na vikao vya NEC na mkutano mkuu.
"Pengine baraza hili liwe na marais wastaafu, makatibu wakuu wastaafu,
watu wenye weledi mbalimbali kwenye jamii, na pia mawaziri wakuu
wastaafu ambao hawagombei kwenye nafasi hiyo ili mradi tu apatikane mtu
makini kwenye nafasi nyeti kama hii ya urais," alisema mstaafu mmoja
aliyenukuliwa.
Chanzo cha Habari na Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment