WAZIRI wa
Ujenzi, Dk John Magufuli, ameanzisha operesheni maalumu ya kukamata
magari ya umma yanayotumia namba za kiraia, baada ya kubaini kuwa
yanatumika kufisidi fedha za Serikali.Waziri huyo pia ameahidi
kuwachukulia hatua kali waliouziwa magari ya Serikali na bado wanatumia
namba zile zinazoonyesha kuwa yanamilikiwa na Serikali.
Alitoa
onyo hilo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari huku akiahidi kuendesha operesheni kali ya kuhakikisha wote
waliokiuka taratibu wanawatiwa mbaroni.
"Operesheni hii
itahusisha magari yote ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala wa
Serikali, Mashirika ya Umma na taasisi nyingine za umma," alisema
Magufuli.
Alisema hivi karibuni Serikali ilibaini kuwapo kwa
magari ya umma yaliyosajiliwa kwa namba za kiraia na yanatumia namba
hizo kwa manufaa binafsi na hivyo kuisababishia Serikali hasara.
Dk Magufuli alisema kwa kuzingatia hali hiyo, atahakikisha kuwa utaratibu wa usajili wa magari ya umma unafuatwa.
“Serikali
itafanya operesheni maluum ya kurejesha usajili wa magari yote ya umma
kwenye utaratibu,” alisisitiza waziri huyo maarufu katika kusimamia
sheria zinazohusu wizara yake.
Alisema Serikali inatoa muda wa
hadi kufikia Novemba 15 mwaka huu magari ya umma yenye namba za kiraia,
yarejeshwe kwenye namba stahiki za magari hayo.
"Baada ya hapo,
tutatumia vyombo vya ulinzi na usalama katika kukamata magari,
pikipiki, bajaj na mitambo ya umma na tunawaomba wananchi watusaidie kwa
kutoa taarifa,"alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli alisema Serikali
iliweka utaratibu unaozuia matumizi ya namba za kiraia kwenye magari,
pikipiki, bajaj na mitambo yake na kwamba hata hivyo utaratibu huo sasa
umekiukwa.
Alisema Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973,
inaipa mamlaka, Wizara ya Ujenzi kusajili na kutunza kumbukumbu za
magari yote ya Serikali ambayo yatapewa namba zitakazotanguliwa na JW,
PT,ST, MT,CW na DFP. Alisema magari, pikipiki, bajaj na mitambo ya
umma itakayokamatwa, itapelekwa katika maeneo ya vituo vya polisi ama
karakana za Tamesa mikoani na maeneo ya idara za ujenzi wilayani.
Alisema
wanaohusika kusimamia na kufanikisha zoezi hilo ni makatibu wakuu wa
wizara zote, makatibu tawala wa mikoa yote, wakurugenzi watendaji wa
halmashauri zote, watendaji wakuu wote wa taasisi na idara za serikali
na watanzania wote. |
No comments:
Post a Comment