HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kueleza mshangao wake kuhusu
vitendo vya rushwa kupenya katika chaguzi zinazohusisha wanawake ndani
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepokewa kwa hisia tofauti na makada wa
chama hicho na wadadisi wa masuala ya siasa, Tanzania Daima Jumatano
limebaini.
Kikubwa kinachoonekana kuwashtua wafuatiliaji wa siasa ndani ya CCM ni
hatua ya Rais Kikwete kutoa kauli ya mshangao pasipo kuonekana
akichukua hatua zozote za kukabiliana na vitendo vya rushwa ambavyo yeye
mwenyewe anakiri kwamba vinahatarisha uhai wa chama hicho.
Mmoja wa makada wa muda mrefu serikalini na ofisa wa juu mstaafu wa
moja ya taasisi nyeti za dola, amelieleza Tanzania Daima Jumatano
kwamba, kauli ya Kikwete imeonyesha namna kiongozi huyo
anavyojitanabahisha kwa namna tofauti na ilivyopata kufanywa na
watangulizi wake watatu.
Ofisa huyo ambaye kama walivyo wengine wanne waliozungumza na
waandishi wa gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa kwa majina yao,
alisema Rais Kikwete ambaye ndiye mwenyekiti wa taifa wa CCM alipaswa
kutoa kauli ya kukemea, karipio na yenye mamlaka dhidi ya wagombea
wanaotoa rushwa katika chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa ofisa mwingine mstaafu, kitendo cha rais kutoa kauli
zinazobadilika badilika kuhusu rushwa huku akiwa na mamlaka ya
kuwachukulia hatua watuhumiwa wa vitendo hivyo hususan ndani ya serikali
na katika vikao vya chama anavyoviongoza, ni dalili za woga wa kuchukua
maamuzi sahihi.
“Rais wangu ni mtu wa kushangaza na mwoga. Amepata kusema anawafahamu
wala rushwa kwa majina. Ni huyu huyu aliyewahi kutamka kuwa siku za wala
rushwa zinahesabiwa na leo anasema eti anashangaa kusikia hata wanawake
wanajihusisha na rushwa katika uchaguzi,” alisema kada mwingine
mwandamizi ndani ya CCM.
Duru za siasa kutoka ndani na nje ya chama hicho tawala, zinasema kuwa
kwa hali ilivyo sasa, CCM inaweza kufa kama isipofanya mabadiliko
makubwa yatakayosaidia kudhibiti hali hiyo.
Tangu kuanza kwa uchaguzi huo wa chama hicho ngazi ya shina hadi
taifa, kumekuwa na malalamiko kila kona ya kukithiri kwa vitendo vya
rushwa, huku watuhumiwa hao wakipitishwa na vikao vya juu na kuibuka na
ushindi.
Tayari baadhi ya vigogo walioanguka katika uchaguzi wa ndani ya CCM
katika ngazi tofauti, wamekuwa wakizungumza chini kwa chini kwamba
kuongezeka kwa kasi ya vitendo vya rushwa ndani ya chama imetokana na
udhaifu wa Rais Kikwete kushindwa kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo.
Akihutubia Mkutano Mkuu wa Nane wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) wa CCM
juzi, Rais Kikwete aliishia kuonya juu ya vitendo vya rushwa vinavyozidi
kushamiri ndani ya chama hicho, akisema kuwa visipochukuliwa hatua
mapema, kuna hatari ya kukifikisha chama katika hatua mbaya.
Hakuishia hapo, alikwenda mbele zaidi na kusema, imekuwa ni hulka sasa
hasa baada ya kumalizika chaguzi kwa wanachama kuendeleza na kuwekeana
uhasama kama uliokuwepo wakati wa kampeni na wengine kuwaadhibu ambao
hawakuwachagua hali ambayo ni mbaya sana kwa mustakabali wa chama.
Rais Kikwete aliwaasa wagombea wa nafasi mbalimbali wa UWT
walioshindwa kutoweka visasi na walioshinda kutowapiga vijembe
walioshindwa kwani kazi iliyo mbele ni kubwa kutokana na CCM hivi sasa
kukabiliwa na hali ngumu ya ushindani wa kisiasa.
“Kweli tusipokemea vitendo hivi na kuviacha vikiendelea, tutakipeleka
chama mahali pabaya, ninasikitika sana kusikia hata wanawake sasa
wanajihusisha na utoaji rushwa ili kununua nafasi za uongozi kitu
ambacho ni hatari sana,” alisema Kikwete.
Alifafanua kuwa chama kinapoelekea si kuzuri ni lazima zifanyike jitihada za mabadiliko.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ameonyesha kutishwa na nguvu na kasi kubwa ya vyama vya upinzani.
Alisema wakati CCM ikichafuka kwa rushwa, vyama vya upinzani vimekuwa
vikijiimarisha kisiasa hali ambayo inakifanya chama chao kiwe katika
wakati mgumu.
Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete alizihimiza jumuiya za chama hicho
kuongeza juhudi na kujipanga kupambana na hali hiyo kwa lengo la
kuiwezesha CCM kushinda uchaguzi wa mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment