Hadithi hadithi!
Hapo zamani za kale paliondokea kitumbili. Kitumbili majaliwa.
Kitumbili huyu alikuwa na rafiki yake ambae ni jirani wa nyumba ya pili
tu kutoka kwao. Sasa wakati wa kula kitumbili akila kwao bila kumuita
rafiki yake. Lakini wakati wa kula kwa rafiki yake Kitumbili majaliwa
alikuwa ndie wa kwanza kudaka tonge. Na kwa maana hii dadithi yangu
imekomea hapa.
Hadithi hii ya kale imepata kuimbwa sana. Na kwa wenye kumbukumbu
nzuri wanakumbuka kuwa Bi Shakila kule Tanga enzi zile, aliimba
‘Kitumbili majaliwa, wala kwenu nala kwetu, na kwetu wajajaliza’.
Taswira hii ya kisanaa inajitokeza tena machoni mwetu mara tu Waziri wa
Elimu wa Zanzibar Mh. Shamuhuna anapotangaza kuleta Walimu wa Sayansi
kutoka Nigeria.
Tamko la Waziri Shamuhuna linanipa mashaka mengi . Shaka ya kwanza ni
kuwa sioni haja ya mwiba uliochomea mguuni kutolewa ulimini. Na hivi
ndivyo anavyofanya Shamuhuna sasa. Kabla hajsema mwiba ulipochomea
anautafuta kwenye ulimi autoe ilhali akijuwa kuwa huko siko ulikochomea.
Tukubaliane kuwa taifa letu hili dogo, Zanzibar, lina uhaba wa
Walimu. Nani asiejuwa. Lakini kwanza hili la uhaba wa walimu
linashuhulikiwaje kabla ya kuomba kwa jirani tena kwa gharama gharika?
Kuna haja ya kujiuliza kuwa jee ni kweli walimu ni haba au kuna jengine?
Maana nionavyo, walimu wapo lakini kutokana na sera duni na mishahara
vibutu, ukikorogea na siasa potofu, walimu hao wengi hukimbilia nchi
jirani au ughaibuni kusomesha. Hili halijapatiwa ufumbuzi tunatafuta
gharama nyengine zisizo na sababu wala adabu.
Wahitimu wa shahada na diploma pale SUZA na Chukwani, ukiachilia walio
na vyeti vya ualimu kule Mkapa, Chuo Cha kiislamu Mazizini, na Kule
Pemba Kiuyu, wangetosha tangu kuanzishwa vyuo hivyo vikuuu mapema miaka
ya 2000 hapa nchini. Lakini kinachojitokeza hapa ni kuwa wahitimu kadhaa
waliondoka kwenda bara na huku Serikali ikijua lakini ikanyamza kimya.
Jirani (Bara) kajaza kijungu kwa makopa yatokayo nyumbani kwetu. Hii
ndio ajizi ya viongozi vitumbili majaliwa. Tuliache la walimu wetu
wanaokimbia kwetu kwenda kwa jirani.
La kusikitisha zaidi hapo katikati tulikuja kufanya mchezo mmoja
mchafu wa kijinga wa kuajiri walimu kiudalali. Walimu kadhaa hasa wa
shule za msingi hapa Zanzibar ambao ni wapya kidogo wengi wao
wameajiriwa kwa mlango wa nyuma bila kuwa na sifa, kwa makubaliano na
maafisa wa juu wa Wizara ya elimu wa kugawana mshahara kwa miezi sita na
kisha mwalimu huyo ‘pyoro’ anaendelea kusomesha kama mwalimu halali.
Hivi kuajiri wasiokuwa walimu huwa tunamdanganya nani na tunategemea
nini? Hivi ndio tutapata walimu wa sayansi kwa kuajiri ndugu zetu
walitoroka chuoni na skuli wakiwa darasa la sita? Hili mbona
halijashuhulikiwa tunatafuta walimu kwengine wakati tumewaajiri wengi
kama hawa?
Kwa upande mwengine,si vibaya hata kidogo kuleta walimu wa kigeni
hapa nchini lakini shaka yangu nyengine iko hapa. Kwanini tuagizie
walimu wa Sayansi badala ya kutayarisha wetu wenyewe na kuwajengea
mazingira mazuri badala ya kutumia gharama nyingi kuleta wageni kwa
mambo ambayo sisi wenyewe tunaweza kuyafanya kwa gharama nafuu na hata
kwa kujitolea? Pili, ikibidi lazima tulete walimu wa Sayansi, kwanini
lazima iwe Nigeria? Kunani Lagos na Abuja? Nanusa harufu ya kivundo
fulani hivi Wizara ya Elimu kwa hili.
Tunaelewa fika kuwa Nigeria wenyewe yao yanawashinda na dunia nzima
inawatambua kama ni watu wasio na radhi wala kubadhi, na isitoshe
hawasarifiki kama ngozi ya futi. Juu ya hayo, sioni kama ni mabingwa wa
sayansi wa kiasi cha Shamuhuna kuona lazima wawe wao tu na awaajiri kwa
magharama na karama. Kuna kitu kimejificha hapa. Kipapo hatukiona lakini
tuendelee kunukiliza harufu itatoka tu.
Kwa upande mwengine, naamini kuna masomo yanahitaji walimu kutoka
nje. Kwa mfano, masomo ya lugha ya kiingereza na zile lugha za kigeni
ingekuwa vyema tukifunga mikataba na balozi zilizopo nchini wakawa
wanatuletea wataalamu wa kufundisha lugha kama ilivyokuwa zamani.
Tuliweza na tukapata vijana wazuri wasiofanana na Mulugo kwa kujua
lugha. Hili Shamuhuna hakuliona au tuseme halitaki.
Kwa sasa suala liko wazi, kuita walimu hao wa kigeni ambao sijui kama
watatosha kwa skuli zote hizi za hapa kwetu, na hata wakitosha bado ni
gharama kubwa kwa taifa ambalo linahangaika kutafuta suluhisho la tatizo
kwa mbinu zisizohusiana na tatizo lenyewe. Kama tunaona kuna uhaba wa
walimu wa Sayansi, jee hili tumeanza kuliona lini? Hakuna mpango wa
elimu wa muda mrefu huko Wizarani? Na kama hauko jee hata tathimini ya
miaka kumi hadi ishirini iliyopita haikutoa bishara ya kuwepo kwa
uwezekano huu wa kujitokeza tatizo hili? Ukweli ni kwamba hakuna lolote
linalofanywa na ndio sasa tunashika hili na lile, mambo yameshaharibika.
Kwa uoni wangu, mie sioni haja ya kuleta wataalmu hao kutoka Nigeria
kwani bado tunahitaji muda wa kutathimni na kuangalia undani na chanzo
cha tatizo hili. Tunahitaji kuandaa mipango bora ya utatuzi wa matatizo
kama haya na pia kuhakikisha kuwa tunabuni mkakati na pembejeo za
kuwafanya walimu wetu wa hapa ndani na walio nchi jirani kuvutika kuja
kusomesha kwetu kwa hiari zao na sio kuletwa hapa kama wataalamu wasio
kuwa na taaluma chochote. Naamini cha thamani au kizuri hakupi jirani
yako. Na mtaalamu wa kweli wa Sayansi hakai tu kule Kaduna, Umuofia,
Lagos, au Kano Nigeria akisubiri Shamuhuna aje amuajiri.
Wataalamu wa nchi zote duniani hasa hasa waNigeria, ni ngumu kuwapata
kirahisi kama anavyofikiri yeye Shamuhuna. Na hili wenzetu wa ulaya
wanalijua vyema na ndio ukaona kila mtaalamu huchukuliwa hapa Afrika
akatumikie Ulaya na Marekani. Sasa leo unaposema unaenda Kaduna, Abuja,
Kano ukamchukuwe mwalimu wa Sayansi mtaalamu umlete Zanzibar, ambapo
mwalimu hulipwa chini ya dola 100 kwa mwezi, sipati picha. Na isitoshe
Muheshimiwa Shamuhuna kama hujashiba kwako, na kwa jirani hushibi.
Tuachie kwa hili, kuna mengi ya kufanya sema tukusaidie.
No comments:
Post a Comment