NJOMBE

NJOMBE

Thursday, May 3, 2012

Vijana Nguvu ya Mabadiliko

Wimbi kubwa la vijana kuamua kujihusisha na “siasa” limekuwa gumzo kwenye miaka ya hivi karibuni. Lakini gumzo na maswali yanazidi hususan katika zama hizi za siasa za vyama vingi.
Ikumbukwe katika siasa za chama kimoja, TANU na baadaye CCM ilihakikisha kila rika linashiriki kikamilifu. Hata watoto wadogo na hapo ndipo tunaona uwepo wa “chipukizi”.
Lakini pindi mabadiliko na kuimarika kwa siasa za vyama vingi, wingi wa vijana (hasa vijana makini) kukimbilia na kujiunga na vyama vya upinzani na kuendesha mabadiliko kama nchi ilivyopitia katika uchaguzi wa mwaka jana, 2010, unachochea uchambuzi wa kina.
Uungwaji mkono wa siasa unaweza kuchambuliwa kuwa unaambatana na mambo makuu mawili; mosi ni msukumo binafsi wa kijana wa Kitanzania wa uhitaji wa mabadiliko.
Pili ni mhemko wa majira (seasonal emotions/exctitement). Mhemko huu ni kama kilevi ama pombe na vijana ndio wanjwaji ama walevi wakuu wa pombe hii kali, nitachambua kwa kina katika makala ijayo.
Wimbi hili kwa ujumla wake linatokana na “maisha magumu” yatokanayo madhara hasi ya utawala, uongozi, dira ya chama tawala CCM uliodumu kwa zaidi ya miaka 50.
Katika makala haya tatawamulika vijana kupitia mtazamo wa falsafa ya vijana nguvu ya mabadiliko na kuchambua kwa kina juu ya msukumo binafsi wa kijana wa Kitanzania juu ya uhitaji wake wa mabadiliko na nafasi yake katika kuleta na kuendeleza hayo mabadiliko kwa kuzingatia misingi ile ile ya falsafa ya vijana nguvu ya mabadiliko.
Hapa ieleweke kwamba katika makala haya kuwa falsafa ya vijana nguvu ya mabadiliko sio mali ya chama kimoja cha siasa hapa nchini. Pia falsafa hii katika makala haya haihusiani na ushawishi wa aina fulani ya itikadi ya kisiasa, dini, rangi ama kabila. Misingi ya falsafa hii unatokana na uhalisia wa dhana kuwa vijana katika karne hii ya 21 ni nguvu ya mabadiliko kutokana na hoja kadha wa kadha.
Lakini pia daima sifa kuu ya “ujana” kama rika ni kuwa na mapenzi katika mabadiliko. Kufanya mambo au kuwa na vitu tofauti na mazoea. Huo ndio ujana daima!
Ulimwengu unakadiriwa kuwa na idadi ya watu zaidi ya bilioni 6, kati ya hao asilimia 80 ikiwa ni vijana. Kwa kigezo cha wingi pekee hatuwezi kupuuza kuwa vijana hawawezi kuwa nguvu ya mabadiliko. Mathalani Afrika Mashariki tu ina jumla ya watu wapatao 126 milioni, kati ya hao asilimia 70 ni vijana.
Tanzania inakadiriwa kuwa na watu wapatao milioni 46, kati ya hao zaidi ya 35 asilimia ni vijana. Takwimu hizi ni kutokana na sensa ya mwaka 2002, panapo majaliwa baada ya sensa ya mwaka 2012 kufanyika huenda idadi hiyo ya vijana ikaongezeka na kuwa kubwa zaidi ya tunavyotazamia.
Hoja ya pili, pamoja na ongezeko la idadi ya watu hapa nchini na kusemekana kuwa vijana ni zaidi ya asilimia 50 ya watu wote hapa nchini, pia wanatambulika kuwa asilimia 65 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana. Nguvu kazi hii haiondoi ukweli kuwa wengi wao vijana hufariki kabla ya kutimiza miaka 30/40. Kama vijana wote wangepata ajira au wasipate ajira, wafanye kazi ama wasifanye kazi, muda wao wa uhai kazini unakadiriwa kuwa jumla ya miaka 8 tu.
Hoja ya tatu ni tafasiri ya neno ‘kijana’. Mwanazuoni nguli Prof. Issa Shivji aliwahi kusema katika moja ya mijadala ya vijana kuwa yeye ni kijana kutokana na kuwa upeo wake wa kufikiri bado una nguvu na hutenda kazi zaidi ya ambavyo vijana kwa mujibu wa umri wao wangeweza kufanya.
Kwa muktadha huo tafsiri ya ujana inaweza pia kuwa kwa mujibu wa fikra na sio umri pekee.
Bado wapo vijana japo ni wachache ambao hutumia fikra zao vyema na kufanya vizuri zaidi ya vijana wenzao kwa mujibu wa umri na pia zaidi wa watu wazima kuwapita umri.
Sera ya maendeleo ya Taifa ya vijana imetoa dira ya kitaifa katika kutafsiri neno kijana kwa kusema kuwa vijana ni wale wenye umri kati ya miaka 18 na 35. Pamoja na kuwa ulimwengu haukubaliani juu ya nani hasa awe kijana kwa mujibu wa umri, Umoja wa Mataifa wao husema kijana ni yule aliye kati ya umri wa miaka 18 na 24. Wakati programu ya Jumuiya ya madola ambayo Tanzania ni mwanachama inasema ni kati ya miaka 16 na 29. Nchi nyingine kama Malaysia inasema vijana ni kati ya miaka 15 na 40. Umoja wa Afrika kupitia makubaliano ya vijana “Youth Charter” wao husema vijana ni kati ya miaka 15 na 35. Hakika huu ni mkanganyo.
Ujana kwa mujibu wa umri sio kitu cha kukitazamia na kukitegemea sana kwa kuwa umri huwa unaongezeka na hatimaye mtu hustaafu ujana kwa mujibu wa umri. Katika Taifa changa kama Tanzania kuendelea kuutafsiri ujana kwa mujibu wa umri hakutaleta tumaini jipya la mabadiliko ya kweli. Hatupaswi kuutafsiri ujana kwa mujibu wa umri kwa kuwa wenye umri wa ujana unaweza usiwe na manufaa sana kwa Taifa kutokana na kufungiwa ndani ya umri. Mfano rahisi ni serikali iliyopo madarakani na Taifa kwa ujumla kushindwa kutumia kile inachokiita asilimia 65 ya nguvu kazi ya Taifa — vijana — katika uzalishaji ili kuongeza ajira, kukuza teknolojia na kufanya mapinduzi ya kimaendeleo.
Vijana, ujana sio umri, ujana ama kijana ni upeo wa fikra pevu. Hii ndio tafsiri ya neno kijana ambayo taifa inapaswa kuichukua na kuifanyia kazi. Upeo wa fikra pevu ndio unaotofautisha maendeleo katika nchi zilizoendelea na nchi za dunia ya tatu, mahali ambapo Tanzania ipo.
Upeo wa fikra pevu ndio utakao wafanya vijana kuwa “nguvu ya mabadiliko”. Bongo za vijana ndio chachu ya mabadiliko, na ndio chemchem ya fikra mpya na mbadala zinazotarajiwa kulitoa Taifa katika usingizi mzito wa kifikra kwa kuwa umri wao wa ujana kwa mujibu wa sera yao, ukipita hautabadilisha chochote endapo hawatatumia vema uwezo wao wa kufikiri na kutenda mambo katika shughuli zao za kila siku.
Tukiisha kufahamu kuwa ujana wetu hautokani na umri wetu bali ujana wetu unatokana na nini tunafikiria na nini tunatenda sawasawa, itatusaidia kudhihirisha kuwa kweli vijana ni nguvu ya mabadiliko.
Ufahamu wetu wa ujana sharti utokane na upeo wa fikra zetu pevu. Fikra zetu zinaweza kuwa na nguvu zaidi ya umri wetu zaidi ya ukomo wa miaka 35. Ili tuone umri wetu hautusaidii ni vema kujiuliza swali moja, je, kwa nini nchi kama Malaysia wao husema ujana unaisha pale mtu anapotimiza miaka 40? Na je, kwa nini ulimwengu haukuwahi kuwa na tafsiri moja ya neno ujana? Matokeo yake sasa nchi zilizoendelea kama Ujerumani, Uingereza na nyinginezo zimeendelea, sio kwa kigezo cha umri wa watu wao, bali kwa mapinduzi ya kifikra tangu kuwekwa kwa misingi ya mataifa yao.
Tafsiri hii mpya ya ujana itatusaidia kuweka dira sahihi ya kujitambua na kuichambua dhana ya “vijana nguvu ya mabadiliko”. Itatusaidia kuondokana na mhemko wa majira ambao nitauelezea vema huko mbele. Itatusaidia kujua tuwe na msukumo binafsi ama wa pamoja katika kudai na kuleta mabadiliko. Mwisho itatusaidia kuweka mustakabari mpya wa Taifa letu Tanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Frederick Fussi ni Katibu Mtendaji katika shirika lisilo la kiserikali la TYVA. Barua pepe: frdmbimbi (at) yahoo (dot) ca. Blog: www.frederick-fussi.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment