NJOMBE

NJOMBE

Saturday, May 5, 2012

Madaktari wafurahia Dk Mponda, Nkya kuondolewa


Aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda
CHAMA cha Madaktari  Tanzania (Mat) kimeeleza kufurahishwa na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuwaondoa aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya, kuwa ametekeleza madai yao.

Pia, chama hicho kimesema kimefurahishwa na uteuzi wa Dk Hussein Mwinyi kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kwa sababu, ni mtendaji anayeaminika.

Katibu Mkuu wa Mat, Dk Rodrick Kabangila, alisema madaktari wamefurahi kuondolewa kwa mawaziri waliokuwapo kwa sababu walikuwa kikwazo kwenye utekelezaji wa madai yao.

“Kwa sasa tuna imani na Serikali, madai yetu na hata yale tunayojadili baina yetu na Serikali yatatekelezwa, tunasema hivyo kwa sababu kama wangeendelea kubaki mawaziri wa awali utekelezaji wake ungekuwa na mashaka,” alisema Dk Kabangila.

Kabangila alisema mawaziri hao walikuwa wagumu wa kutekeleza madai yao na wakati mwingine, walioonekana kuwadharau hali iliyosababisha waingie kwenye mgomo.

“Dk Mwinyi tunamfahamu, wakati madaktari tulipogoma mwaka 2004/05 alikuwa Naibu waziri alikuja kutusikiliza, yapo mambo alichukua hatua kwa wakati,” alisema Dk Kabangila na kuongeza:

“Akiwa Naibu waziri wakati huo alionyesha tofauti kubwa na Naibu waziri aliyeondolewa Dk Nkya, kwani amekuwa na kiburi hata madaktari walipogoma aliendelea na msimamo wake.”

Kuhusu uteuzi wa mawaziri wapya kwa jumla, Dk Kibangila alisema unaleta matumaini kwa sababu una sura nyingi mpya na zenye majina yanayoonyesha uadilifu.Chanzo ni Mwananchi
  

No comments:

Post a Comment