NJOMBE

NJOMBE

Thursday, May 3, 2012

Unajua kipaji chako?

Utambuzi wa vipaji hula fikra.
Vijana wengi tumeshapitia au tunapitia kwenye kipindi kigumu sana maishani. Nina uhakika wengi wetu tumeshawahi kukosa usingizi wakati tupo kitandani na kubaki tu kuangalia dari na kujiuliza maswali mengi sana; nitafanya nini maishani? Mustakabali wa maisha yangu ni upi? Nitakuwa wapi baada ya miaka miwili, mitano au hata kumi?
Bahati mbaya Watanzania hatuna hulka ya kujadili mambo kama haya kwa uwazi tukiwa na ndugu, jamaa na marafiki zetu. Na matokeo yake (tunaonekana kama) hatujifunzi kutoka kwa wenzetu — hili suala ndilo linalonipa misongo kwenye mijadala mbalimbali. Kwahiyo, ni matumaini yangu kuwa nasaha zilizopo kwenye makala hii zitabadilisha fikra za angalau kijana mmoja na kutambua kuwa maisha yake ya baadae yako kwenye viganja vyake! Kwa maneno mengine, wewe msomaji ndio mwenye uwezo mkubwa wa kuamua maisha yako huko mbeleni yaweje.
Je, unajua una kipawa, kipaji au talanta ipi? Baada ya kumaliza elimu ya sekondari au chuo kikuu, ulikuwa au unajua unataka ufanye nini; uwe mtu wa aina gani kwenye jamii?
Kama unashindwa kujibu hayo maswali haraka na kwa ufasaha, usiogope na wala usitetereke. Hauko mwenyewe, kijana. Wengi tumeshapitia na tunaendelea kupitia kwenye kipindi ambacho fikra zetu zinakuwa zimejawa na mawazo ya utata. Lakini utakubaliana nami kuwa wenzetu ambao tayari wanajua wana vipaji fulani na kuvifanyia kazi, maisha yao huonekana marahisi machoni mwa wengi.
Amini usiamini, majibu ya maswali mengi hupatikana hapa — kwenye tovuti ya Bongo Celebrity. Jeff na timu yake wamekuwa wanajitahidi kutuletea mahojiano murua ya watu maarufu wanaofanya vizuri Bongo kwenye nyanja mbalimbali, ili mimi na wewe tujifunze mawili matatu kutoka kwao na kutumia ‘maujanja’ kwenye maisha yetu; kukuza vipaji vyetu na kuviendeleza.
Jifunze kutoka kwa waliofanikiwa
Kwa mfano, Profesa Jay akihojiwa huwa anatoa nasaha nyingi sana ambazo binafsi naamini zinatakiwa kuhamasisha kila kijana anayezisikia kwa namna moja au nyingine. Cha kusikitisha wengi wetu tutakumbuka tu ni lini Mzee wa Mitulinga atatoa album mpya. Basi.
Mmoja wa waliofanikiwa.
Sielewi kwanini tunafumbia macho ukweli kuwa Jay huwa anatembea na karatasi na kalamu karibia muda wote, na akiona kitu ambacho anadhani kitakaa vizuri kwenye mashairi yake huwa anakiandika papo kwa papo. Muda mwingine hata akiwa na marafiki zake. Kama bado hujanielewa, Jay ni mwandishi mzuri sana na huwa anaandika mashairi muda wote! Na suala la kipaji chake kukua, kupevuka na kukomaa linajidhihirisha kila kukicha. Kasikikilize wimbo unaoitwa Chuzi limekubali wa Hard Blasters Crew, halafu linganisha na mashairi yaliyojaa busara kwenye wimbo Machozi, Jasho na Damu aliouimba takribani miaka miwili baadae.
Ninachojaribu kukuasa kijana mwenzangu ni kama ifuatavyo: Fungua macho ukiwa kwenye pita-pita na mihangaiko yako; ukiona kichuguu kizuri angalia kwa makini na jifunze jinsi kinavyojengwa na siafu, badala ya kukisifia tu na kuendelea na safari.
Tambua una vipaji

Safari ya kutambua una kipaji au vipaji gani, kuvikuza na kuvifanyia kazi inaweza ikawa ngumu au rahisi kutegemeana na mazingira na mazingara uliyokulia na uliyomo. Huo ni mjadala mrefu sana ila sitaki kuzama huko, kwasababu naamini vitu ambavyo vinampa mtu motisha vina nguvu zaidi.
Kama nilivyosema hapo awali, usikubali mtu mwingine akuamulie maisha yako ya baadae yaweje kwasababu tu amekuzidi umri au ana mamlaka fulani. Aghalabu kauli zenye mamlaka zinaweza kukufunga mawazo yako na kukusukuma kufanya jambo ambalo labda sio ile kitu roho inapenda. Pia, usifuate mkumbo; jaribu kufikiria mustakabali wako binafsi kwanza.
Kwa mantiki hiyo, ni jukumu lako kugundua una vipawa gani. Sidhani kama kuna njia rahisi ya kukwambia, “Aisee, bwa’ mdogo una kipaji (fulani)! Kifanyie kazi.” Njia pekee itakayokuwezesha kufaulu huo mtihani ni kujaribu kufanya na kufuatilia mambo mbalimbali — iwe kwa kusoma vitabu vya taaluma au magazeti, kuongea na kubadilisha mawazo na watu n.k. Huwezi kung’amua kuwa wewe ni mchezaji mzuri wa mpira kwa kukaa kijiweni, wakati u mvivu wa hata kupiga danadana tu.
Wewe imba, mimi nitadonoa nyuzi za gitaa.
Jiulize, ingekuwa vipi kama Man Dojo na Domo Kaya wangekaa tu vijiweni Arusha na kutothubutu kujaribu kupiga gitaa na kuimba?
Usiogope kukosolewa
Changamoto kubwa mwanzoni ni kuondokana na hofu ya kufanya makosa au kuogopa kukosolewa. Ni kawaida kila  binadamu kuogopa, ila kinachotufautisha ni jinsi tunavyokivuka hiki kihunzi. Unadhani sikujawa na hofu hata chembe nilipopewa fursa ya kuandika hii makala na kuanika mawazo yangu hadharani? Kilichonipoza ni ile motisha ya kutumia kasoro zozote zitakazojitokeza na kuhakikisha naandika makala nzuri zaidi nitakapopewa fursa nyingine.
Lengo langu kubwa ni kuanzisha mjadala mzuri, kwasababu ninaamini kuna Watanzania wengine wengi wenye uzoefu na mawazo mazuri zaidi yangu, na nina kiu na njaa ya kujifunza kutoka kwao!
Ukiacha kipaji, huyu ana 'kismati' cha kupendwa kutokana na tabia yake.
Hadithi nzuri kuhusu kujua jinsi ya kutumia vema ukosolewaji inatoka kwa Sir Juma Nature. Sir Nature alitoka kwa njia ya kushirikishwa kwenye nyimbo kama Mtani Jirani, Mtulize na Maskini Jeuri. Mimi ni mmojawapo wa mashabiki wake wakubwa na nilivutiwa sana na kisa alichokiimba kwenye wimbo Mtani Jirani. Ila Juma wa kipindi kile ni tofauti na yule Juma aliyetikisa na Hili Gemu, Kighetto-ghetto (remix), Jinsi Kijana na nyimbo nyingine lukuki.
Juma alikuwa anatumia lugha ‘ngumu’ iliyokuwa inaeleweka kwa vijana wa Kurasini, Keko, Temeke, Tandika, Mtoni na Mbagala. Nakumbuka P-Funk, Bonny Luv, Sebastian Maganga na wengine wengi walimkosoa na kumshauri ‘alainishe’ mashairi yake. Kijana hakuzira wala kunywea, akaufanyia kazi ushauri.
Jiamini na amini unachofanya
Rock City sasa inaitwa Rap City.
Labda hii ndio nguzo kubwa kuliko zote. Sijui kama inajengwa kwa mambo niliyoyajadili kwa kifupi hapo juu, au ndio msingi unaohimili niliyoyataja. Kama wewe hujiamini na wala huamini kuwa unachofanya ni kizuri na kina manufaa kwa jamii, unategemea wanaokuzunguka wakuamini?
Hakika kauli za kutia moyo kutoka kwa wazazi, ndugu, marafiki na watu ulio nao karibu zinaweza kukusaidia. Ila huwa napenda kusisitiza zaidi ile motisha mtu binafsi aliyonayo.
Huyu Fid Q kipenzi cha wengi, safari yake haikuanzia na wimbo Mwanza au FidQ.com. Kijana ilibidi atoke Mwanza kwa hela ndogo aliyokuwa nayo hadi Dar ili aje kufanya alichoamini ni kipaji chake. Unaweza ukadhani  alikuwa anacheza karata tatu au kamari, kwasababu lolote lile lingeweza kutokea kwenye safari yake na labda tusingepata kumsikia hata mara moja.
Bahati mbaya (kwa wapinzani wake) na nzuri (kwa mashabiki wake), alipewa nafasi ya kughani kwenye wimbo mmoja unaoitwa Ukweli na Uwazi uliopo kwenye album ya Wachuja Nafaka. Fid Q akatoka rasmi. Ukisikiliza nyimbo zake mbili za kwanza, utaafiki kuwa alikuwa anajiamini na anaamini alichokuwa anafanya.
Sio kazi na dawa, bali ni kazi na kazi
Ingawa sipendi kurusha mawe ya lawama, nitajiona mwenye hatia kama nisiposema haya yafuatayo kwa wale ma-DJ na waandishi wa habari wanaopata fursa ya kuwahoji watu waliofanikiwa kwenye fani mbalimbali.
Waandishi hamna budi kuuliza maswali yatakayozaa majibu yenye manufaa.
Wachache wenu mmesahau kuwa kazi mliyokuwa nayo ni dhamana. Mna zana zote za kubadilisha fikra za watu wanaosikiliza vipindi vyenu. Mimi siridhiki mnapotaja tu wimbo au kitabu fulani cha mhusika kitatoka lini na mambo mengine kama hayo kwa dakika thelathini!
Mnasahau kuwa kazi mnazoletewa ni matunda yanayotokana na juhudi, jasho na uwajibikaji wa wahusika. Kwanini mnashindwa kusisitiza kazi nzuri hutokana na watu kujituma? Vipi, mbona mnashindwa kutuambia zile shows nzuri za Waunaume Halisi au TMK zinatokana na vijana kufanya mazoezi kila siku?
Ukiongea na watu waliofanikiwa utagundua kuwa, ukiacha vipaji walivyonavyo, ni wavumilivu na wanajituma. Kwahiyo, kijana mwenzangu, ukishagundua kipaji chako, huna budi kukilea, kukitunza na kukilinda kama mboni za macho yako. Na muhimu zaidi ni kukifanyia kazi kila siku; hakika hiyo ndio njia pekee itakayokuletea matunda.
Ukiangalia kulia, kushoto, mbele na nyuma utaona ‘vita baridi’ kati ya kizazi cha vijana wa sasa na wa zamani. Bahati mbaya vijana wa sasa (wanaonekana) wamepoteza matumaini na wamebakia kulaumu, ilihali wanaweza kuamka, kugundua vipaji vipaji vyao, kujenga moyo wa kujiamini na kufanya kazi ili kuleta mabadiliko.
Kila mkoa unatakiwa kuwa na vijana kama hawa!
Kila mkoa unatakiwa kuwa na vijana kama hawa!
Nchi inahitaji kina Modesta, Zitto na January kwenye kila mkoa; viongozi wapya wanahitajika. Magazeti yanahitaji waandishi wanaoweza kuakisi mawazo yetu. Jenerali Ulimwengu akistahafu, hatuna budi kuliziba pengo lake kwa kuwa tutaendelea kuhitaji makala zitakazotufanya tufikirie. Wahandisi na wanasheria wanahitajika na wataendelea kuhitajika.
Kijana, huu ni waraka kwako: Tambua na tumia kipaji chako ipasavyo — usijidharau.

No comments:

Post a Comment