Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, ninapenda kuchukua fursa hii
kukaribisha tena katika makala hii ya ndoa na familia. Juma lililopita
tuliangalia kwa pamoja nafasi ya mwanamke na mama katika Familia.
Tukahitimisha kwa kukumbusha kwamba, Bikira Maria, Malkia wa Familia ni
mfano bora wa kuigwa kwani, kutokana na kuukubali mpango wa Mungu katika
maisha yake, amekuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu.
Leo
tunaendelea kupembua kuhusu hati ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Yohane
Paulo wa pili kuhusu wajibu wa familia za kikristo katika ulimwengu
mamboleo. Hati hii ya familiaris consortio no. 25 inasema katika
muungano wa ndoa mume anaitwa pia kuwa baba katika familia yake.
Upendo
wa kweli wa Wanandoa unadai mwanamume atambue kuwa mke wake ni msaidizi
ambaye katika sura na mfano wa Mungu wako sawa sio mtumwa wake hivyo
ampokee kwa upendo, kama zawadi na awe na shukurani kwa zawadi ya hii.
Mfano wa upendo unaodaiwa kati yao ni kama ule wa Kristo kwa kanisa lake
(Efeso 5:21-33)
Mwanamume anapaswa kuwa baba wa watoto kibalojia,
kisaikolojia, kijamii na kiroho hivyo huyu ni mlezi halisi wa watoto
wake katika nafasi yake. Mwana shairi mmoja analinganisha nafasi ya baba
katika malezi ya watoto na mwalimu anayemfundisha mwanafunzi wake
kuogelea. Anasema endapo mwalimu atamshikilia sana mwanafunzi kwa hofu
ya kuzama basi mwanafunzi hatajifunza kuogelea kabisa.Lakini endapo
atamwachia sana bila kumpa uangalizi katika maji basi mwanafunzi
atazama.
Ndivyo ilivyo kwa baba endapo atakuwa mkali mno mtoto wake
hataweza kujifunza kujitegemea kabisa kwani atashindwa kutumia uhuru
wake. Lakini akimwachia tu bila kumwelekeza uhuru utazidi na mtoto wake
atakuwa mtoto aliyekosa malezi ambayo ni hatari sana kwa makuzi yake.
Tujifunze nini katika hayo yote tuliyosema? Kwanza kila mmoja ajitahidi kuimarisha upendo kwa mwenzake katika nafasi yake.
Pili
ni ukweli kwamba katika familia nyingi kuna kilio cha kutoweka kwa
akinababa. Wapo akina baba ambao wamebaki baba wa uzazi tu lakini
ukiwauliza kuhusu watoto wao watasema mama yao ndiye anajua. Na bahati
mbaya zaidi wapo watoto ambao hata hawawafahamu baba zao. Tukumbuke
mtoto aliyekosa malezi ya baba hupungukiwa mengi. Ni vizuri akina baba
tujitahidi kumwiga Mt. Yosefu ambaye wakati wote alijitahidi kuwa karibu
na mama Maria katika makuzi ya mtoto Yesu.
Tumalizie tafakari yetu
kwa maneno ya Yoshua bin Sira sura ya 30 anayesema, Mzazi ampendaye
mwanawe, atamrudi mara kwa mara ili amwonee fahari jinsi
anavyokua...hata kama baba yake akiwa amekufa atakuwa kama hakufa maana
ameacha nyuma mtoto anayefanana naye.
Kutoka Studio za Radio Vatican,
mimi ni Padre Raphael Mwanga, toka Jimbo Katoliki Same, mwanafunzi wa
ndoa na familia, Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa,
Laterano, Roma.
Ujumbe kutoka Radio Vatican.
No comments:
Post a Comment