MGOMO wa Madaktari umeshika kasi kiasi cha kusababisha Waziri Mkuu
Mizengo Pinda kufuta ziara yake ya siku kumi iliyokuwa ikitarajiwa
kuanza mkoani Mwanza leo, huku huduma za afya katika baadhi ya
hosipitali nchini zikiathirika kwa kiasi kikubwa.
Ziara hiyo
ambayo ilipaswa kuanza leo Machi 9, mehairishwa hadi hapo itakapopangwa
baadaye huku taarifa za ndani zikieleza kuwa kuhairishwa huko kunatokana
na Waziri Mkuu huyo kuwa katika majukumu ya kushughulikia kutatua mgomo
wa madaktari ambao ulianza juzi. Mgomo wa madaktari umeshika kasi na
kuathiri huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na
Taasisi ya Mifupa (MOI) ambayo jana ilitangaza kusitishwa kwa huduma za
klinini kwa wagonjwa wa nje (OPD).
Msemaji wa Taaisi hiyo, Juma
Almasi alisema jana kwamba hatua hiyo imelenga kuwawezesha madaktari
wachache waliopo kuhudumia wagonjwa 237 waliolazwa wodini.
“Taasisi
ina wagonjwa 237 waliolazwa wodini na madaktari wanaoendela kufanya
kazi ni wakuu wa idara na wenye nafasi za uongozi ambao idadi yao
haizidi 15”alisema Almas.
Alifafanua kuwa katika siku za kawaida
huduma za Kliniki kwa wagonjwa wa nje hutolewa na zaidi ya Madaktari 20
huku idadi ya wagonjwa ikitofautiana kutokanana na aina ya kliniki
zilizopangwa kwa siku husika.
“MOI inamadaktari zaidi ya 70 na
kila siku huduma za Kliniki za nje hutolewa na Madaktari zadi ya
20,kutokana na mgomo huu tumeamua kusitisha huduma za wagonjwa nje
wanaokuja kwa ajili ya Kiliniki na kwamba tutaendelea kuwahudumia
walioko wodini”.
Pia msemaji huyo alisema huduma nyingine zitakazopatikana katika Taasisi hiyo ni katika kitengo cha dharura.
Wagonjwa walalama
Wagonjwa
wote waliofika MOI jana kupata huduma za vipimo mbalimbali katika
Kliniki waliamriwa kurejea nyumbani kwao hadi watakapopata taarifa za
kumalizika kwa mgomo huo kupitia vyombo vya habari.
Wakizungumza
na Mwananchi baadhi ya wagonjwa na wauguzi waliitupia lawama serikali
kwa kushindwa kutatua tatizo hilo ambalo walidai dalili zake zilionekana
tangu mwanzo.
Mmoja wa wagonjwa hao, Kulwa Amiri (30) Mkazi wa
Dar es Salaa alimtaka Rais Jakaya Kikwete,Waziri Mkuu Mizengo Pinda na
Mawaziri wanaokataliwa na madaktari kutafakari na kuchukua hatua zaidi
ili kunusuru maisha ya wagonjwa.
“Katika mgomo wanaoathirika ni
wengi siyo tu mgonjwa,wapo waangalizi wa wagonjwa nao wanapoteza muda
kwa kumsindikiza mgonjwa,nauli na pia hata kazi wanazozifanya
zinasimama”alisema Amiri na kuhoji:
“Hivi ni kweli serikali
haioni mateso tunayopata?,inashindwa nini kuwawajibishwa hao mawaziri
hao, hata kutaka kututoa sisi kafara?mbona Mh Edward Lowasa alipokuwa
waziri Mkuu alijiuzulu, tunaomba watafakari kwa makini kwani tunaoteseka
ni sisi”alisema Amiri ambaye alivunjika uti wa mgongo.
Wakati
mgonjwa huyo akilalamikia kitendo hicho,baadhi ya ndugu wa wagonjwa
wengine waliokuwa wamelazwa Wodini walifika hosptalini hapo na kuanza
kuahamisha wagionjwa wao.
Marwa Chacha na ndugu zake
walimhamisha, Edina Kimeta aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Mwaisela
huku akieleza kufikia uamuzi huo kuwa imetokana na hali ya kutisha na
isiyotabirika iliyopo katika eneo hilo.
“Tumeamua kumchukua bibi
yetu Edina na kumhamishia katika hosptali ya binafsi ya Regency sababu
tumeona hali katika eneo hili inatisha,kwanza mambo yanaingiliana wapo
wanaofahamu na wengine hawafahamu”alisema Marwa.
Bugando nako moto
Madaktari
katika hospitali ya rufaa ya Bugando jana waliingia siku ya pili katika
mgomo wao na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa waliofika kwenye
hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu. “Leo tuliitwa kwenye kikao na
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, lakini tulikubaliana
tusifike kwenye kikao hicho hivyo hatutakwenda,” alieleza mmoja wa
madaktari hao ambaye hakutaka kuandikwa gazetini kwa kile alichoeleza
kuwa sasa sio wakati wa kuandikana majina kwenye vyombo vya habari.
Huduma katika hiospitali hiyo jana zilianza kuzorota kwani licha ya
baadhi ya madaktari kutogoma hali ilikuwa ikionyesha kuzidiwa kwa
madaktari waliokuwa wakiendelea na kazi.
“Unajua hapa kuna
madaktari wa aina mbili wapo wale wa kanisa na wale wa wizara. Sasa hawa
wa kanisa wanaendelea na kazi, lakini kwa vile wale wa wizara ni wengi,
imekuwa vigumu kuendana na mahitaji,” alifafanua mmoja wa wauguzi wa
hospitali hiyo. Hata hivyo uongozi wa hospitali hiyo haukupatikana jana
kuzungumzia suala hilo baada wengi wao, akiwamo mkurugenzi, Dk Charles
Majinge kuwa kikaoni.
Tamko la Tughe
Ikiwa ni siku ya pili tangu
mgomo kuanza Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe)
kimetoa tamko la kuzitaka pande mbili zinazolumbana kutumia busara
kumaliza mgomo huo.
Katibu Mkuu wa Tughe , Ali Kiwenge alisema
jana Dar es Salaam kwamba mgomo huo ni matokeo ya pande hizo mbili
kutegemeana na kutoaminiana katika kufikia mwafaka juu ya suala hilo.
“Sisi
tunasema Serikali na Madaktari, hayo yanayoendelea wananchi
wanawashangaa, tunasema hivyo sababu wanajua madai ya Madaktari Serikali
iliyapokea na kuahidi kuyafanyia kazi, na ndiyo sababu Waziri Mkuu
Pinda aliunda tume, lakini nao madaktari wakakubali kutoa nafasi ili
madai hayo yafanyiwe kazi”alisema Kiwenge.
Alisema kufuatua hatua
hiyo Tughe wanasisitiza kuwa suluhu lazima ifikiwe kupitia kwenye vikao
na kuonya kila upande kutumia busara kunusuru maisha ya Watanzania.
Kiwenge
aliitaka serikali kufanya kazi kama chombo cha umma ikiwa ni pamoja na
kushughulikia masuala mbalimbali kwa kufuata sheria,taratibu na kananuni
zilizopo.
Alisema ni jambo la kawaida kwa serikali nyingi
hususani za kiafirika na Tanzania ikiwamo kufanya kazi kinyume na
taratibu jambo ambalo husababisha manungĂșniko, mgogoro, migomo baridi na
baadaye migomo kamili na maandamano.
Pinda afuta ziara
Waziri
Mkuu Mizengo Pinda ameahirisha ziara ya siku kumi mkoani Mwanza
kutokana na mgomo wa madaktari, imethibitishwa. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
Evalist Ndiliko ingawa hakueleza wazi iwapo ziara hiyo imehairishwa
kutokana na mgomo wa Madaktari, alidai kuwa ziara hiyo imesogezwa mbele
kutokana na waziri mkuu kuwa na majukumu mengine ya kitaifa ambayo
anapaswa kuyashughulikia. “Ni kweli ziara hii imesogezwa mbele kutokana
na Mheshimiwa waziri mkuu kuwa na majukumu mengine, kwa sasa tunangoja
taarifa itaanza lini,” alisema Ndikilo jana.
Hata hivyo,
Mwandishi Msaidizi wa waziri Mkuu, Irene Bwire alithibitisha kuahirishwa
kwa ziara hiyo kutokana na mgomo huo wa madaktari na kueleza kuwa ziara
hiyo itafanywa hapo baadae. “Ni kweli tumeelezwa kuwa ziara
imeahirishwa kwa ajili hiyo na tumetangaziwa kuwa ziara hiyo itafanywa
wakati mwingine” alisema Bwire.
Katika ziara hiyo Waziri Mkuu
alitarajiwa kutembelea wilaya zote nane za mkoa wa Mwanza ambazo ni
Ilemela, Nyamagana, Magu, Kwimba, Misungwi, Ukerewe, Geita na Sengerema
ambako angekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na
kuzungumza na viongozi wa Halmashauri hizo. Ziara hii ilikuwa ni ya
pili kwa Waziri Mkuu tokea alipoteuliwa kushika wadhifa huo, ambapo
ziara ya kwanza alifika Jijini mwanza wakati wa maadhimisho ya miaka 40
ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Madaktari juzi walitoa tamko linaloeleza msimao wao wa kuendelea na mgomo usiokoma nchi nzima.
Habari na Mwananchi
No comments:
Post a Comment