Malezi huweza kuwaathiri!
Mwanamke
ambaye ana tabia a kujilaumu yeye kama mwanamke na kulaani kuwa kwake
mwanamke, yuko kwenye nafasi kubwa ya kumuuwa mtoto wake wa kike
kisaikolojia. Kuna wanawake ambao kwa kuudhiwa na waume zao au hata na
wanawake wenzao huwa wanapenda sana kuropoka kauli za kudhalilisha
jinsia ya kike.
“Mimi
nakwambia sisi wanawake hatufai kabisa, kuzaliwa mwanamke ni jambo baya
sana………ningekuwa naweza nimwombe Mungu anibadilishe niwe mwanaume ….
Wanawake ni wajinga sana….” Kauli za aina hii zinaporudiwa mara mbili au
tatu humfanya mtoto wa kike kuziamini na huanza kuwa na wasiwasi na
jinsia yake. Hata watoto wa kiume nao huziamini kauli hizi na kuanza
‘ubabe’ wa kiume kuanzia hapo.
Mtoto
wa kike anapozisikia kauli hizi kutoka kwa mama yake na kwa sababu mama
yake ndiye ‘shujaa’ wake, huanza kujenga dhana kwamba, kama mama yake
hapendi kuwa mwanamke, kwa sababu mwanamke ni mjinga na dhaifu, naye
hana budi kuikimbia hali hiyo.
Anaikimbiaje?
Kuna
njia nyingi za kukimbia hali hiyo, lakini kubwa na ya karibu ni kwa
mtoto huyu kuanza kujibainisha na jinsia ya kiume. Kwa sababu akili ya
mtoto haichuji, huanza kuhisi vibaya kuwa kwake mwanamke mbele ya
wenzake, hasa wanaume. Kujibainisha na jinsia ya kiume ni pamoja na
kufuatana na wanaume, kuvaa kiume, kuongea kiume, kutembea kiume na
kufanya kazi za kiume.
Siyo
lazima, lakini mtoto huyu anaposhindwa kupata mahali ambapo atadondosha
dhana au imani hii, ni wazi atakuja kujibainisha kimapenzi,
atajibainisha kama mwanaume. Matokeo ya jambo kama hili ni kuwa na
mwanamke ambaye anataka kuwa mwanaume kwa wanawake wenzake kimapenzi.
Kama
sio kauli za akina mama kujilaumu, kauli za akina baba kuwalaumu
wanawake pia na akina mama kuzikubali kivitendo, zinaweza kuwaathiri
watoto wa kike kimakuzi. Baba anapokuwa na tabia ya kutoa kauli kali na
chafu dhidi ya mama, na mama kuonyesha kukubaliana na kauli hizo kwa
vitendo ni hatari sana.
Hebu sikia kauli kama hii kutoka kwa baba: “Mwanamke gani anayezaa mitoto ya kike tu, ni afadhali kuoa mke mwingine…..” majibu
ya mwanamke anayekashifiwa ni haya: “Kwani mimi nimetaka, si Mungu
mwenyewe, kwani hata mimi si ninapenda watoto wa kiume……” Kwa mtoto wa
kike majibu kama haya, huwa yanasikika masikioni mwake kama, “Hata mimi
sitaki watoto wa kike kwa sababu hawana thamani, lakini sina uwezo wa
kuwakataa..”
Akina mama, yawapasa kuelewa kwamba, kauli zao na kuzipa kauli za waume zao nguvu, huweza kuwaathiri sana watoto wao. Kila neno wanalotamka kwa watoto ni lazima walikague mara mbili. Waume zenu wanapotoa kauli zinazobagua watoto kijinsia mbele ya watoto hao ni lazima mzikanushe sawia na kuwaeleza watoto ukweli utakaowapa nguvu ya kufurahia jinsia waliyonayo.
No comments:
Post a Comment