MWENYEKITI wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho
hakijutii kumfukuza kwenye chama hicho Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid
Mohammed na washirika wake kwa kuwa ni waasi na uamuzi huo umefanywa
kulinda nidhamu ndani ya chama.
Uamuzi wa kuwavua uanachama Hamad
Rashid na wajumbe wenzake watatu wa Baraza Kuu la CUF, Doyo Hamis Doyo,
Juma Saanani na Shoka Khamis Juma, umekuwa ukitajwa kama sababu ya
kuanza kuanguka kwa himaya ya kisiasa ya chama hicho kwa upande wa bara.
Lakini,
jana, Profesa Lipumba akizungumzia mwelekeo wa chama hicho alipokutana
na waandishi wa habari Dar es Salaam, alisema CUF ni chama imara hivyo
lazima kifanye uamuzi kwa kufuata vikao na katiba yake.
“Uamuzi wa
kuwafukuza uanachama hatuujutii, ulifanywa kwa umakini kwa kufuata
taratibu za kufanya uamuzi kwa njia ya vikao na katiba. Nikiwa Marekani
nilikuwa nawasiliana na viongozi wenzangu na uamuzi waliofikia ulikuwa
na lengo la kukiimarisha chama,” alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu
wanachama kukihama chama hicho baada ya kuwafukuza kina Hamad, Profesa
Lipumba alisema: “Watu wanaweza kuchapisha kadi nyingi na kusema ni za
wanachama waliohama kumbe si kweli. Hatuwezi kuchapisha kadi kama
zilivyo noti kwa kuwahofia wahalifu wanaozichapisha, jambo la msingi ni
kuwafahamu wanachama wetu.”
“Kuna utata katika takwimu za watu
wanaokihama chama, maeneo mengine idadi ya wanachama wanaohama inaelezwa
kuwa ni kubwa kuliko idadi wanachama tuliowahi kuwa nao. Hizi ni mbinu
zinazotumiwa kuonyesha kwamba chama kinaelekea kufa lakini, ukweli ni
kwamba kipo imara na kitaendelea kuwepo.”
Jana Hamad Rashid
hakupatikana kutwa nzima kujibu tuhuma hizo. Lakini aliwahi kukaririwa
akieleza kuwa uamuzi kumfukuza uanachama ulifanyika kwa mizengwe na
chuki.
Alithibitisha madai yake hayo kwa kufungua kesi Mahakama
Kuu kupinga uamuzi huo na kuiomba Mahakama imtake Katibu wa chama hicho,
Maalim Seif Shariff Hamad na Baraza la Wadhamini la chama hicho kueleza
kwa nini wasichukuliwe hatua kwa kukiuka amri iliyozuia mkutano wa
kumfukuza.
Barua pepe
Akijibu tuhuma za Hamad Rashid kwamba
aliwahi kunasa waraka wa barua pepe unaoonyesha mawasiliano kati yake na
Maalim Seif, Profesa Lipumba alisema kitendo cha kuanika hadharani
mawasiliano binafsi ni kosa la jinai... “Hili ni kosa la jinai mtu
anatamba hadharani akionyesha mawasiliano ya barua pepe za watu kinyume
na taratibu!”
Mwishoni mwa mwaka jana, Hamad Rashid wakati akiwa
katika mvutano na uongozi wa juu wa chama chake, alitoa nakala kwa
waandishi ukionyesha kile alichodai kuwa ni waraka wa mawasiliano ya
barua pepe kati ya Profesa Lipumba na Maalim Seif ukitaja mbinu za
kumng’oa katika CUF.
Azungumzia uchumi
Katika mkutano huo,
Profesa Lipumba ambaye ni mchumi aliyebobea, pia alizungumzia hali ya
uchumi nchini na kusema chama chake kinafanya uchambuzi na hivi karibuni
kitakuja na mkakati kuitaka Serikali kuwafungulia akaunti wananchi na
kuwaingizia fedha zinazotokana na rasilimali za taifa.
“Tunaamini
kwamba wananchi wakiingiziwa mgawo wa fedha kwenye akaunti zao na
kukatwa kodi itakuwa rahisi kufuatilia matumizi ya fedha yanayofanywa na
Serikali. Watu wakikatwa kodi watakuwa na uchungu na hizo fedha,
watafanya kila njia kuhakikisha kwamba zinatumika vizuri kwa ajili ya
maendeleo.”
Profesa Lipumba alisema ili hayo yafanyike, ni lazima nchi iwe na utawala bora wenye kusimamia kikamilifu rasilimali za taifa.
Akizungumzia
kilimo, alisema asilimia 80 ya watu wanategemea sekta hiyo lakini bado
hakijamsaidia Mtanzania... “Tanzania ina ardhi kubwa, lakini wananchi
wanategemea chakula cha aina moja hali ambayo inawafanya wengi wao
kuugua utapiamlo.”
Profesa Lipumba alisema suala la kuendeleza
kilimo lina umuhimu mkubwa kwa sababu ni eneo linaloweza kutoa ajira kwa
wananchi hasa vijana.
No comments:
Post a Comment