MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, jana aliiomba mahakama
kutupilia mbali tuhuma dhidi yake kwa sababu ni za uwongo, chuki na
fitna.
Amedai kuwa hali hiyo ndiyo iliyowafanya Waziri mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowasa na aliyekuwa mgombea kupitia CCM, Dk Batilda
Burian, hawakufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kutajwa mara
kadhaa.
Akiongozwa na wakili wake, Method Kimomogoro katika kutoa
ushahidi, Lema alidai kuwa kesi hiyo iliyofunguliwa na wapiga kura
watatu, imetokana na chuki za mlalamikaji wa kwanza, Mussa Mkanga baada
ya kukosa udiwani katika Kata ya Sombetini.
Alimwomba Jaji
Gabriel Rwakibarila kuwaamuru wadai kumlipa ghrama zote alizoingia na
muda wake aliopoteza tangu alipoanza kuhudhuria shauri hilo lililoanza
kuunguruma Julai mwaka jana, ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Alimweleza
jaji kuwa kwa kipindi cha miezi mitatu sasa ameshindwa kutekeleza
majukumu yake ya kibunge, kwa sababu ameazimika kuhudhuria mahakamani
kushughulikia kesi hiyo.
Alidai kuwa kesi hiyo imetokana na madai
ya uwongo uliotungwa na wadai Mkanga na wenzake Agnes Mollel na Happy
Kivuyo wanaowakilishwa na mawakili Alute Mughwai na Modest Akida.
Aliieleza
mahakama kuwa kama tuhuma dhidi yake zingekuwa za ukweli, Lowasa na Dk
Burian waliotajwa kwa namna ya kuonekana kudhalilishwa na kushushiwa
hadhi yao mbele ya jamii, wangefika mahakamani kutoa ushahidi ili
kuthibitisha tuhuma dhidi yake.
Lema alidai viongozi hao wameacha
kwenda mahakamani kutokana na ukweli kwamba maneno yanayodaiwa kuwa
aliyatamka dhidi yao si ya kweli.
Alidai kuwa hiyo pia ndiyo sababu ya Dk Burian kutofungua kesi dhidi yake baada ya uchaguzi mkuu uliopita.
Aliieleza
mahakama iliyojaa wasikilizaji kuwa hata katika barua yake ya
malalamiko kwa msimamizi wa uchaguzi, Dk Buriana alishindwa kuorodhesha
au kutoa mifano ya kauli za matusi, kashfa na udhalilishaji alizodaiwa
kuzitoa.
Lema alidai kuwa kitendo hicho ndicho kilichomlazimisha
msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Arusha Mjini, Raphael Mbunda
kumruhusu kuendelea na kampeni.
Shahidi hiyo alidai hata vielelezo
vya nakala ya CD zizodaiwa kurekodiwa maneno yake ya matusi
hayakuwasilishwa mahakamani kuthibitisha tuhuma dhidi yake.
Alidai kuwa CD hizo zingewasilishwa mahakamani kesi hiyo ingekuwa imeisha mapema kwa sababu ukweli ungedhihirika.
Katika
hatua nyingine, Jaji Rwakibarila aliendelea kuwavunja mbavu kwa vicheko
wananchi wanaohudhuria mahakamani baada ya jana kuanza mtindo mpya ya
kudhibiti wanaosinzia wakati kesi inaendelea kwa kuwaamuru kusimama kwa
dakika kadhaa kabla ya kuwaruhusu kuketi tena.
Habari na Mwananchi
No comments:
Post a Comment