PINGAMIZI lililowekwa na Chadema kwa mgombea ubunge wa CCM katika
uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha, Siyoi
Sumari, limezua utata baada ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kudaiwa
kuvujisha barua ya siri kwa chama hicho cha upinzani.
Vyanzo vya
habari vya gazeti hili, vimeeleza kwamba barua hiyo ya siri ilivujishwa
na kigogo mmoja wa Serikali mkoani hapa, kwa kile kinachodaiwa, chuki za
kisiasa ambapo aliwaagiza makada wa CCM kuifikisha Chadema, ili Siyoi
awekewe pingamizi.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa
Mulongo alipoulizwa na mwandishi wa gazeti hili kwa njia ya simu jana,
alikanusha vikali ofisi yake kuvujisha barua hiyo kwa Chadema, huku
akisema kwamba Serikali imeanza uchunguzi wa kina kubaini Chadema
walikoipata barua hiyo.
“Mimi kwanza situnzi nyaraka za Serikali
na siwezi kutoa nyaraka za Serikali lakini ni lazima tuchunguze Chadema
wameipata wapi hiyo document (waraka),”alisema Mulongo.
Chanzo cha mvutano
Juzi
wakati Chadema wakitangaza uamuzi wa kumwekea pingamizi mgombea ubunge
wa CCM, Sumari, walitumia barua iliyoelezwa kuwa ya siri, ambayo Mulongo
aliandikiwa na Idara ya Uhamiaji mkoani hapa kuhusiana na utata wa
uraia wa mgombea huyo.
Hata hivyo katika mchakato wa kura za
maoni za CCM, Mulongo anadaiwa kuwa katika kundi lililokuwa likimpinga
Sumari kupitishwa kugombea na chama hicho tawala.
Mkurugenzi wa
Bunge na Halmashauri ya Chadema, John Mrema alisema kwamba barua hiyo
yenye kumbukumbu namba AR/32/ VOL.1/85 iliyoandikwa na Mkuu wa Uhamiaji
mkoani Arusha, Daniel Namomba kwenda kwa Mkuu huyo wa Mkoa, ilieleza
taratibu mbalimbali za kisheria za mtu kuwa raia au la.
Katika
barua hiyo iliyoandikwa Febuari 29 mwaka huu, Namomba alitoa ufafanuzi
wa sheria hiyo kutokana na maombi ya kufanya hivyo aliyotakiwa na
Mulongo kupitia barua yenye kumbukumbu namba CFAl18l114l01l20 .
Katika
barua hiyo Mkuu huyo wa Idara ya Uhamiaji alieleza kwamba mgombea huyo
alizaliwa eneo la Thika nchini Kenya Mei 11 mwaka 1979 na kwenda mbali
zaidi kufafanua kwamba, kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji namba 7 ya
mwaka 1995, kuna uraia wa aina tatu ambao ni wa kuzaliwa, kurithi na
kuomba.
Ndani ya barua hiyo, Namomba alifafanua kifungu ambacho
mtu anayezaliwa nje ya nchi kama atarithi uraia wa wazazi wake, mmoja au
wote, ukomo wake ni miaka 18 na kama atakuwa amezaliwa nje ya nchi, na
amefikisha miaka 18 anapaswa kuukana uraia alionao na kuomba uraia wa
nchi ambayo anaishi kwa kuapa kiapo cha utii, jambo ambalo Idara hiyo
haina kumbukumbu kama Siyoi aliukana uraia wa nchi alikozaliwa.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa
Kufuatia
utata wa sakata hilo, Mkuu huyo wa Mkoa alipoulizwa juu ya taarifa
hizo, aliendelea kukanusha madai ya ofisi yake kuvujisha barua hiyo huku
akisisitiza kwamba ana uhakika barua hiyo haijatokea ofisini kwake naye
hahusiki kwa namna yoyote na kuvuja barua hiyo.
“Mimi
nakwambia sihusiki kabisa na hilo jambo na nina uhakika kwamba hiyo
barua, Chadema hawakuitoa ofisini kwangu, waulizeni Chadema wameitoa
wapi ? ”Alihoji na kusisitiza Mulongo
Alikituhumu Chadema kuzua
habari hiyo na kudai kwamba wakati fulani, waliwahi kuibuka na nyaraka
ambazo wanadai walizitoa Idara ya mambo ya ndani na kumbe si kweli.
Alisema ofisi yake itachunguza kwa kina kujua chama hicho kilikopata
barua hizo.
Hata hivyo alipotakiwa kujibu madai kwamba ndiye
aliyeagiza Idara ya Uhamiaji ichunguze uraia wa Siyoi, Mulongo alisema
ni lazima watu wafahamu ya kwamba CCM ilihitaji vielelezo vya mgombea
yeyote ambaye alikuwa na mashaka, ili vifikishwe mbele ya chama hicho.
Habari zaidi na Mwananchi
No comments:
Post a Comment